HABARI MPYA

Home Top Ad

Post Top Ad

Thursday, 22 February 2018

VITUO MAALUM VYA UCHENJUAJI KUJENGWA KATIKA MAENEO YA WACHIMBAJI WADOGO NCHINI.

Na Zuena Msuya, Geita
Serikali  inadhamiria kujenga vituo maalum vya uchenjuaji na kuvizungushia ukuta katika kila eneo lenye wachimbaji wadogo ili kudhibiti wizi na uuzwaji holela wa madini ya dhahabu katika maeneo hayo.
Katibu Mkuu wa Wizara ya Madini Profesa Simon Msanjila alisema hayo Februari 20, 2017 mkoani Geita ,wakati wa ziara ya kikazi ya kukagua maendeleo ya ujenzi wa Kituo cha Mfano na Mafunzo kwa wachimbaji wadogo kinachojengwa katika eneo la Rwamgasa mkoani humo.
Prof. Msanjila alisema kuwa vituo hivyo vitakapojengwa vitarahisisha ukusanyaji wa mapato na kuwasaidia wachimbaji kuuza dhahabu yao kwa bei halisi na kudhibiti walanguzi katika maeneo ya wachimbaji.
Vilevile alifafanua kuwa utaratibu unaotumiwa na wachimbaji wadogo hivi sasa kuchenjua dhahabu, umekuwa ukipoteza dhahabu nyingi ikilinganishwa na utumiaji wa njia za kisasa: Pia hakuna kumbukumbu sahihi na taarifa zilizo wazi zinazoonyesha soko halisi la uuzaji wa dhahabu inayochimbwa na wachimbaji wadogo katika maeneo mbalimbali nchini.
"Tunawachimbaji wadogo wa dhahabu wengi sana nchini hii, na wanapochimba wanapata dhahabu lakini ukiwauliza wanauza wapi dhahabu yao hakuna majibu sahihi, pia ukiuliza bei kila mmoja anamajibu yake, na kwa mtindo huu wanaikosesha serikali mapato, hali hii haikubaliki lazima idhibitiwe" alisisitiza Msanjila.
Profesa Msanjila alisema kuwa lengo la serikali ni kuwaewezesha na kuwaendeleza wachimbaji wadogo ili wanufaike na rasilimali hiyo ya madini hivyo ni wajibu wao pia kuilinda sekta hiyo kwa kuzingatia kanuni na sheria za madini ili kuleta maendeleo yenye tija.
Akizungumzia Kituo cha Mfano na Mafunzo kwa wachimbaji wadogo kilichopo Rwamgasa, Msanjila alisema ameridhishwa na maendeleo ya ujenzi wa kituo hicho hadi ulipofikia sasa na kuwaeleza wasimamizi wa ujenzi wa kituo hicho kuwa wahakikishe kinajengwa katika ubora unaotakiwa ili kukidhi mahitaji husika.
Pia alimuagiza mkandarasi anayejenga kituo hicho kuwashirikisha wachimbaji wadogo kuanzia hatua za awali ili waweze kupata elimu ya kutosha na pia watoe mafunzo kwa vitendo kwa wanafunzi wanaosomea elimu hiyo kwa kuchukua wanafunzi kutoka vyuo mbalimbali.
Aidha Msanjila, aliwataka viongozi wa serikali ya kijiji pamoja na wale wa wachimbaji wadogo wa mkoa wa geita( GEREMA) kuwasisitiza wachimbaji wao kufuata kanuni na sheria za uchimbaji madini ili kundoa adha ya kubughudhiwa na serikali.  
Eneo la ukubwa wa hekta 19 litatumika kutekeleza mradi wa  Kituo cha Mfano na mafunzo katika eneo la Rwamgasa Mkoani Geita ambapo kwa sasa ni hekta tano tu ambazo zimetumika katika ujenzi wa kituo hicho, pia vituo vingene saba kama hivyo vitajengwa katika Mikoa tofauti hapa nchini.
 Katibu Mkuu wa Wizara ya Madini Profesa Simon Msanjila, akishuka chini ya mgodi uliojengwa katika Kituo cha Mfano na Mafunzo ili kujiridhisha na ujenzi huo.
 Katibu Mkuu wa Wizara ya Madini Profesa Simon Msanjila( katikati) akiwa chini ya mgodi uliojengwa katika kituo cha Mfano na Mafunzo kilichopo Rwamgasa, mkoani Geita.
 Katibu Mkuu wa Wizara ya Madini Profesa Simon Msanjila, akipata maelezo namna ya mtambo wa uchenjuaji utakavyofanya kazi katika Kituo cha Mfano na Mafunzo, kutoka kwa Mkandarasi anayejenga Kituo cha Mfano na Mafunzo, Mhandisi Rogers.
 Katibu Mkuu wa Wizara ya Madini Profesa Simon Msanjila,( tatu kulia) na maafisa kutoka wizara ya madini na serikali ya kijiji waakiwa juu ya sehemu ya mtambo wa uchenjuaji katika Kituo cha Mfano na Mafunzo ,wakifanya ukaguzi.
Katibu Mkuu wa Wizara ya Madini, Profesa Simon Msanjila, (tatu kushoto) na alipotembelea mgodi wa Mwenyekiti wa Wachimbaji Wadogo mkoani Geita (GEREMA) Christopher Kadeo( tatu kulia).

No comments:

Post a comment

Post Bottom Ad