HABARI MPYA

Home Top Ad

Post Top Ad

Friday, February 16, 2018

MAFUNZO YA UONGOZI KWA WALIMU WA SHULE ZA MSINGI NA SEKONDARI YAFANYIKA JIJINI DAR

Na Said Mwishehe,Globu ya jamii
BRITISH Council kupitia mradi wa Connecting Classrooms umetoa mafunzo ya uongozi kwa walimu wakuu wa shule za msingi na sekondari 100 kutoka Wilaya zote za Mkoa wa Dar es Salaam.

Kwa mujibu wa British Council lengo la mafunzo hayo ni kuendelea kuwajengea uwezo walimu hao katika masuala ya uongozi, ufundishaji bora  na mbinu bora za kufundisha wanafunzi ili wafaulu kwenye masomo yao.

Akizungumza  katika Shule ya Sekondari Mzimuni ambako ndiko mafunzo hayo yalikuwa yakitolewa kwa siku tatu, Meneja Mradi wa Connecting Classrooms Ephraim Kapungu amesema kupitia mradi huo wamefanikiwa kufikia walimu wengi 100 kwenye mkoa wa Dar es Salaam.

"Tumetoa mafunzo haya kwa walimu wakuu shule za msingi na sekondari kwa walimu hao.Lengo letu ni kuwajengea uwezo katika masuala ya uongozi hasa kwa kuzingatia mradi huo unatambua umuhimu wa walimu wakuu kuwa na mafunzo ya aina hiyo.

"Tunaamini kupitia mafunzo haya ya uongozi walimu wakuu watakuwa na fursa ya kuweza kuongoza shule zao kwa umakini wa hali ya juu na kufanya shule hizo kuwa watulivu na kujikita kwenye kutoa elimu iliyo bora,"amesema Kapungu.

Amesema wamekuwa wakitoa mafunzo hayo tangu mwaka 2015 na kwa mradi wa sasa ni wa mwaka mmoja na wanaamini watafikia walimu wengi zaidi hadi utakapomalizika.

Ameongeza mbali ya walimu hao 100 waliopata mafunzo hayo kwa Mkoa wa Dar es Salaam , pia wamefanikiwa kutoa mafunzo ya aina hiyo kwa walimu wakuu  1500 na walimu wa darasani 3000 na kuongeza wanamini idadi itaongezeka kwa kuwa mradi huo n endelevu.

"Tumekuwa tukifanya kazi na Serikali tangu mwaka 2015 hadi mwaka huu 2018.Tueleze tu tutakuwa na miradi endelevu kwani dhamira ni kuona walimu wetu wanakuwa na uelewa kwenye masuala Pia amesema wamekuwa wakifanya kazi na Serikali tangu mwaka 2015 na utaisha mwaka 2018 ila mradi endelevu,"amesema Kapungu.

Amesema mikoa mingine ambayo wamefika kutoa mafunzo hayo ni Dodoma, Kigoma, Lindi na Mtwara na kote huko ambako wamekwenda ni maeneo ya vijijini.Zamani walikuwa wanatoa mafunzo hayo kwa walimu wakuu walioko mijini tu lakini sasa wameamua kwenda hadi vijijini.

Ameongeza baada ya kutoa mafunzo hayo watakuwa wakishirikiana na maofisa elimu wa wilaya na mkoa katika kufuatilia walimu waliopata mafunzo hayo kwani lengo lao ni kuona wale ambao wameyapata nao wanafundisha walimu wengine.

"Hatuwezi kutoa mafunzo kwa walimu wote, hivyo wale ambayo wanayapata basi nao wanatakwenda kutoa kwa walimu wengine.Hivyo utaratibu ulioko ni kushirikiana na maofisa elimu wa Serikali ili kufikia malengo.Wote tunajenga nyumba moja ambayo ni Tanzania lazima tushirikiane kwa maslahi ya nchi,"amesema.

Amesema wanatambua walimu wakuu wengi ni wapya na hivyo kupitia mradi huo unatoa nafasi ya kuwasaidia walimu hao kwenye kuwapatia mafunzo hayo.

Kwa upande wa Ofisa Elimu Msingi Wilaya ya Kinondoni jijini Dar es Salaam,Kaduma Mageni amesema mafunzo hayo yamekuja wakati muafaka kwao na kikubwa zaidi ni elimu ambayo wameipata katika masuala ya uongozi.

"Mwalimu Mkuu kwa nafasi yake ni kiongozi, hivyo anaongoza walimu , anaongoza wanafunzi.Kwa mazingira hayo lazima uwe na uelewa wa masuala ya uongozi kuhakikisha utulivu unapatikana shuleni,"amesema.

Hivyo Mageni anasema mafunzo hayo ya British Council yamewasadia walimu kuwambusha majukumu yao na wajibu wao wawapo mashuleni."Kwa siku tatu ambazo tumepata mafunzo hayo kuna kitu ambacho tumeongeza kama walimu wa Mkoa wa Dar es Salaam,"amesema Mageni.

Amefafanua shule moja unaweza kukuta kuna walimu kati ya 70 hadi 80 na kwa mazingira hayo ili mambo yawe sawa anayewaoongoza lazima awe na uelewa mpana kwenye mambo ya uongozi.

Wakati huo huo ,Ofisa Elimu upande wa Kilimo na Mazingira Wilaya ya Kinondoni jijini Mwalimu Kinangwida Hamida Fadhil amesema mafunzo hayo yenye lengo la kuwawezesha walimu wakuu ujuzi kwenye uongozi na menejimenti

"Mafunzo hayo yametusaidia katika kutujengea uwezo walimu.Kwa tahimini iliyopo walimu wameelewa sana .Tumejifunza tofauti ya kiongozi na meneja ambapo awali wengi hatukuweza kutofautisha nafasi hizo mbili.Kiongozi ni kuongoza na meneja ni mtendaji na ili mambo yaende unatakiwa kusimama kwenye pande zote mbili na tumejifunza kwa mapana,"amesema.

Amesema anatambua mchango wa walimu katika nchi yetu na hivyo wakiwa viongozi wazuri kwenye maeneo yao ya kufundisha na utawala maana yake kinaandaliwa kizazi ambacho kitakuwa nacho kinautulivu.

"Mwalimu akiwa nunda maana yake na mwanafunzi naye atakuwa nunda.Hivyo kufanya walio wengi nao kuwa manunda.Mafunzo haya yanatufanya walimu kuwa kwenye misingi iliyobora na maana yake tunaandaa kizazi bora kwa ajili ya Taifa letu.Ni mafunzo ya muda mfupi lakini tumejifunza mambo mengi na ya msingi,"amesema.

Naye Mmoja ya wakufunzi wa mafunzo hayo stiven Shunda amesema mafunzo hayo lengo lake ni kuwakumbusha walimu wakuu majukumu yao na wao kama British Council wamekuwa wakiyatoa kwa walimu katika mikoa mbalimbali.
 Afisa Mkuu wa Idara ya Kilimo,Umwagiliaji na Ushirika kutoka Manispaa ya Kinondoni,Saleh Hijja Mohamed (aliyesimama) akizungumza kabla ya kumalizika kwa semina ya siku tatu ya mafunzo ya uongozi kwa walimu wa shule za msingi na sekondari wa Jiji la Dar es Salaam leo. Semina hiyo imefanyika katika Kituo cha Walimu cha Mzimuni kilichopo Magomeni Mapipa. Kulia wanaoshuhudia ni Afisa Mkuu wa Miradi wa Shirika lisilo la Kiserikali la British Council,Atiya Sumar na Meneja Miradi wa Shirika hilo,Ephraim Kapungu. Picha na Elisa Shunda
 Afisa Mkuu wa Miradi wa Shirika lisilo la Kiserikali la British Council, Atiya Sumar akizungumza katika ufungaji wa semina hiyo.
 Meneja Miradi wa Shirika Lisilo la Kiserikali la British Council, Ephraim Kapungu (katikati) akielezea utendaji kazi wa shirika hilo katika uwezeshaji wa masuala mbalimbali yahusuyo elimu jinsi shirika hilo linavyofanya kazi zake kwa kushirikiana na serikali kupitia wizara ya elimu.
 Mmoja kati ya wakufunzi wa semina hiyo Ndg.Edwin Shunda akiwa katika majukumu yake ya ufundishaji na uwezeshaji wa uongozi kwa walimu wakuu wa shule za msingi na sekondari wa Jiji la Dar es Salaam.
 Washiriki wa Semina hiyo wakifuatilia mafunzo hayo kwa umakini mkubwa.
 Afisa Mkuu wa Idara ya Kilimo,Umwagiliaji na Ushirika kutoka Manispaa ya Kinondoni,Saleh Hijja Mohamed (kushoto) akigawa cheti kwa mmoja wa washiriki wa semina ya siku tatu ya mafunzo ya uongozi kwa walimu wa shule za msingi na sekondari wa Jiji la Dar es Salaam leo. Semina hiyo imefanyika katika Kituo cha Walimu cha Mzimuni kilichopo Magomeni Mapipa. Kulia wanaoshuhudia ni Afisa Mkuu wa Miradi wa Shirika lisilo la Kiserikali la British Council,Atiya Sumar na Meneja Miradi wa Shirika hilo,Ephraim Kapungu. Picha na Elisa Shunda
 Afisa Elimu Mkuu wa Manispaa ya Kinondoni,Kiduma Mageni akimpongeza mmoja wa washiriki wa semina ya siku tatu ya mafunzo ya uongozi kwa walimu wa shule za msingi na sekondari wa Jiji la Dar es Salaam leo.
Mgeni rasmi, Afisa Mkuu wa Idara ya Kilimo,Umwagiliaji na Ushirika kutoka Manispaa ya Kinondoni,Saleh Hijja Mohamed (katikati) akiwa na viongozi wa shirika la British pamoja na walimu wakuu wa shule za msingi na sekondari katika picha ya pamoja baada ya kumalizika kwa semina ya siku tatu ya mafunzo ya uongozi kwa walimu hao wa Jiji la Dar es Salaam.

No comments:

Post a Comment

Post Bottom Ad