HABARI MPYA

Home Top Ad

Post Top Ad

Thursday, February 8, 2018

KESI YA WEMA SEPETU KUUNGURUMA FEBRUARI 26 MWAKA HUU

 Na Karama Kenyunko, Blogu ya jamii.

Shahidi wa pili wa Upande wa Mashtaka katika kesi ya kutumia dawa za kulevya  inayomkabili msanii Wema Sepetu ameieleza  Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu kuwa aliijaza fomu ya kupima sampuli ya mkojo wa Wema, kabla hajamfanyia vipimo.

Aidha Shahidi huyo, Inspekta Wille, alidai kuwa hajawahi kupeleka sampuli za mkojo  za washtakiwa Angelina Msigwa  na Matrida Seleman Abbas ambao ni wafanyakazi wa Wema kwenda kuchunguzwa kwa Mkemia Mkuu wa Serikali kuhusu kukutwa na dawa za kulevya aina ya bangi.

Shahidi ameeleza hayo leo mbele ya Hakimu Mkazi Mkuu, Thomas Simba alipokuwa akihojiwa na Wakili wa upande wa utetezi, Albert Msando baada ya kumaliza kutoa ushahidi wake.

Alipoulizwa muda gani alipeleka sampuli hiyo kwa Mkemia, alidai kuwa aliijaza fomu ya kupeleka sampuli ya mkojo wa Wema saa nne kamili asubuhi akiwa ofini kwao na kuandika maneno kuwa sampuli hiyo ya mkojo iko kwenye chupa ya plastiki lakini alikuwa bado hajampima mshtakiwa.

Alipoulizwa kama alijaza fomu hiyo kwa kuhisi tu, alidai, alijaza hivyo kwa kutumia uzoefu wake wa miaka 15 katika jeshi la polisi kwani alikuwa anajua taratibu za upimqaji ukifika katika ofisi ya Mkemia mkuu wa Serikali mkojo unakuwa katika chupa ya plastiki.

Aliendelea kudai kuwa Februari 8, mwaka jana alifika katika ofisi za Mkemia Mkuu wa Serikali  saa tano asubuhi na kumkabidhi Mchunguzi Elia Mulima kichupa cha plastiki ambacho ndani kilikuwa na mkojo.

Wakili Msando alimuuliza shahidi ulikuwapo wakati sampuli ya mkojo uliokuwamo ndani ya kichupa cha plastiki  unaodaiwa kuwa ni wa Wema ulipochukuliwa ambapo Inspekta Wille alidai kuwa hakuwapo.

Wakili Msando alimuuliza Inspekta Wille anaweza kusema kuwa unajua kwa uhakika kilichokuwa ndani ya chupa ya plastiki kuwa ni mkojo na je ni mkojo wa Wema? Alijibu kuwa hajui.

Msando alimuhoji Inspekta Wills kuwa walikaa kwa muda gani katika Ofisi ya Mkemia Mkuu wa Serikali, Inpekta Wille alidai kuwa hakumbuki.

Shahidi huyo alidai kuwa yeye hakupekuwa katika chupa anacholala Wema bali alipekuwa katika chumba anachohifadhia nguo ikiwamo nguo na viatu.

Alidai kuwa katika upekuzi walikuta msokoto wa bangi jikoni juu ya kabati, pia walikuta msokoto wa bangi uliotumika ukiwa ndani ya kiberiti dirishani katika chumba wanacholala wafanyakazi wa Wawili  wa Wema.

Mahakama iliipokea hati ya ukamataji mali iliyojazwa katika upekuzi uliofanyika nyumbani kwa Mlimbwende wa Tanzania mwaka 2006 na msanii wa Filamu,  Wema Sepetu  kama kielelezo.

Kesi imeahirishwa hadi Februari 26 na 27, 2018 itakapoendelea kusikilizwa kwa ushahidi wa mashahidi wa upande wa mashtaka.

Mbali na Wema, washitakiwa wengine wanaokabiliwa na kesi hiyo ya kutumia dawa za kulevya ni Angelina Msigwa  na Matrida  Abbas.

Kwa pamoja wanakabiliwa na mashitaka mawili ya kukutwa na kiwango kidogo cha dawa za kulevya na kutumia dawa za kulevya.

Inadaiwa  kuwa  Februari 4, mwaka jana katika makazi ya Wema huko Kunduchi Ununio,  washitakiwa hao walikutwa na msokoto mmoja na vipisi vya bangi vyenye uzito wa gramu 1.08.

Kwa upande wa Wema yeye anadaiwa kuwa Februari Mosi, mwaka jana katika  eneo lisilojulikana jijini Dar es Salaam,  alitumia dawa za kulevya  aina ya bangi.

No comments:

Post a Comment

Post Bottom Ad