HABARI MPYA

Home Top AdPost Top Ad

Thursday, 22 February 2018

FIRST NATIONAL BANK YAENDESHA MKUTANO KUJADILI UCHUMI

 Afisa Mtendaji Mkuu wa FNB Tanzania, Warren Adams akizungumza na wadau pamoja na waandishi wa habari jijini Dar es salaam leo kwenye mkutano wa kujadili uchumi unaofanyika kila mwaka nchini. Picha na Cathbert Kajuna - Kajunason/MMG.  Mwendeshaji wa mkutano na Mchambuzi wa Masuala ya Uchumi Barani Afrika kutoka Rand Merchant Bank ya Afrika Kusini, Neville Mandimika akizungumza na wadau kutoka sekta mbalimbali katika mkutano ulioendeshwa na First National Bank na kujadili uchumi unaofanyika kila mwaka nchini.
Wadau kutoka sekta mbali mbali wakihudhuria katika mkutano wa kujadili uchumi unaofanyika kila mwaka nchini ulioendeshwa na First National Bank Tanzania jijini Dar es salaam leo.

Na Cathbert Kajuna - Kajunason/MMG. First National Bank Tanzania (FNB) leo imefanya mkutano wake wa kujadili uchumi unaofanyika kila mwaka nchini, na kuwaleta pamoja wadau kutoka sekta mbalimbali.

Mada kuu katika mkutano huo ikiwa ni “Mtazamo wa soko la kiuchumi na kifedha la Tanzania mwaka 2018 na zaidi” mkutano huo umetabiri ukuaji na kuimarika kwa uchumi wa Tanzania kwa mwaka 2018 na 2019.

 Mwendeshaji wa mkutano huo ambaye pia ni Mchambuzi wa Masuala ya Uchumi Barani Afrika kutoka Rand Merchant Bank ya Afrika Kusini, Neville Mandimika amesema Tanzania ni moja kati ya nchi kumi za Kusini mwa Jangwa la Sahara ambazo uchumi wake unakua kwa kasi kubwa kutokana na kuimarika kwa sekta za kilimo, ujenzi na sekta ya bidhaa mbali mbali.

 Matarajio ya kuimarika kwa uchumi yanatokana na maboresho yanayoendelea kufanyika katika sekta za fedha na sekta za kodi na kuongeza kuwa ukuaji huu wa uchumi utaendelea kuimarika sambamba na kupungua kwa utegemezi wa fedha za misaada kutoka nje.

"Marekebisho na maboresho katika masuala ya kodi yanatarajiwa kuongeza mapato na kuisaidia Tanzania kutekeleza miradi ya maendeleo kwa fedha za ndani sambamba na ukuaji uchumi,” alisema. 

Mandimika alisema Tanzania inaendelea kuimarika kiuchumi pamoja na kwamba kuna mabadiliko kadhaa katika sheria zinazosimamia na kudhibiti utendaji katika sekta mbalimbali ikiwemo kupiga marufuku uagizaji wa makaa ya mawe, ulazima wa makampuni ya kigeni kuuza hisa kwenye soko la hisa la Dar es salaam, upigaji marufuku wa kusafirisha madini ghafi na mapitio ya mikataba ya madini. 

 Akizungumza juu ya ukuaji wa uchumi wa kimataifa, Mandimika alisema uchumi wa dunia nzima kwa ujumla unaendelea kuimarika isipokuwa China ambayo inaonekana kuwa na ukuaji mdogo kulinganisha na mataifa mengine. 

 Afisa Mtendaji Mkuu wa FNB Tanzania, Warren Adams alisema kuwa mkutano huo umewapa fursa ya kipekee washiriki kujadili mada mbalimbali za kiuchumi na kifedha kuhusu Tanzania, Afrika Mashariki, Afrika na dunia nzima kwa ujumla ikiwa pia ni fursa ya kuelewa mwelekeo wa kiuchumi ili kuweza kutumia fursa mbalimbali za kibiashara zilizopo.

No comments:

Post a Comment

Post Bottom Ad