HABARI MPYA

Home Top Ad

Post Top Ad

Tuesday, January 9, 2018

WAZIRI AAGIZA KUFUFULIWA KWA MNADA IFIKAPO FEBRUARI ILI KUDHIBITI UPOTEVU WA MAPATO YA KILA MWEZI

Waziri wa Mifugo na Uvuvi, Luhaga Mpina (mwenye kofia) akipata maelezo ya hali ya sekta ya mifugo na Uvuvi kutoka kwa Mkuu wa Wilaya ya Missenyi Kanali Denis Mwila (mwenye suti nyeusi) alipotembelea kituo cha mpakani cha Mutukula leo.
Waziri wa Mifugo na Uvuvi, Luhaga Mpina (mwenye kofia) akipokea maelezo ya changamoto za ukaguzi mazao ya mifugo na Uvuvi kutoka kwa Afisa Uhamiaji Konstabo, Rahabu Joel alipotembelea kituo cha mpakani cha Mutukula leo.
Waziri wa Mifugo na Uvuvi, Luhaga Mpina (mwenye kofia) akiangalia mabondo ya samaki aina ya Sangara yaliyokamatwa katika kituo cha mpaka cha Mutukula mkoani Kagera. Kulia ni kaimu Mkurugenzi wa Idara ya maendeleo ya Uvuvi Mwanaidi Mlolwa katikati Mkurugenzi Mtendaji wa Wilaya ya Missenyi Limbe Maurice. Kilo120 zilikamatwa katika kituo hicho.
Waziri wa Mifugo na Uvuvi, Luhaga Mpina akifungua mlango wa gari lililokamatwa na Kamati ya Ulinzi na Usalama ya Wilaya ya Ngara likiwa limepakia samaki kilo 2,000 aina ya Sangara na kilo 530 wa aina ya Sato zenye thamani ya shillingi 20,850,000/= kwenye mpaka wa Mlusagamba wilayani Ngara tarehe 03/12/2017.

Na John Mapepele

Waziri wa Mifugo na Uvuvi Luhaga Joelson Mpina ya Halmashauri ya Wilaya ya Ngara kuhakikisha inafufua mara moja mnada wa Mlusagamba ifikapo mwezi Februari mwaka huu ili kudhibiti zaidi ya milioni mia moja zinazopotea kwa wafanyabiashara wanaokwepa kulipa kodi ya Serikali ya kusafirisha mifugo nje ya nchi kwa kupita njia za panya.

Waziri Mpina aliyasema haya leo alipokutana na uongozi wa Halmashauri hiyo pamoja na Kamati ya Ulinzi na Usalama ya Wilaya ya Ngara katika kituo cha mpaka cha Rusumo baina ya Tanzania na Rwanda kukagua shughuli mbalimbali za sekta za Mifugo na Uvuvi baada ya kutokea katika kituo cha Mutukula mkoani Kagera ambapo pia alifanya ukaguzi kama huo na kukamata kilo 120 za mabondo ya samaki aina ya Sangara yaliyokuwa yakitokea nchi jirani ya Uganda bila kufuata utaratibu.

“Mimi kama Waziri mwenye dhamana ya sekta ya mifugo na uvuvi naelekeza kwamba ifikapo Februari mwaka huu nataka miundo mbinu yote iwe imeboreshwa na mnada wa Mlusagambo uwe unafanya kazi katika kiwango cha mnada wa upili na mimi mwenyewe nitahakikisha ninakuja kuuzindua”lisisitiza Mpina

Waziri Mpina alisema kutokuwepo kwa Mnada wa Mlusagambo kunaipotezea Serikali mapato makubwa ambapo mifugo mingi imekuwa ikiuzwa katika nchi jirani na Serikali kuambulia kiasi kidogo cha fedha kutokana na wafanyabiashara kupita njia za panja na kufanikiwa kukwepa kulipa kodi malimbali za Serikali. Alisema taarifa inaonyesha kuna idadi kubwa ya Ng’ombe wanaopita njia za panya ambao hawatozwi ushuru wa kushafirishwa jambo ambalo amelilalamikia kuwa ni hujuma na kuendekeza rushwa baina ya watendaji wa Serikali.

Aidha amesema Wizara inakusudia kuomba Serikali kupandisha ushuru wa kusafirisha mifugo (movement permit) kufikia shilingi 50,000/= badala ya shilingi 20,000/= ya sasa kwa kuwa hailingani na hali halisi ya soko na gharama za utunzaji wa mifugo hiyo.

“Tutahakikisha tunaiomba serikali ibadili ushuru huu kwa kuwa mfugaji anatumia gharama kubwa za kumfuga na kumnenepesha mfugo kwa zaidi ya miaka mitano halafu anakuja kupata shilingi 20000 tu ni jambo lisilokubalika” alisisitiza Mpina Aliongeza kwamba baada ya kukamilika kwa mnada huo Serikali itaweka vizuizi katika njia zote za panya ambapo pia alisisitiza watendaji wa Serikali na wananchi kwa ujumla kuwa waadilifu na kuwa walinzi badala ya kutegemea viongozi wa kitaifa wa Serikali kulinda utoroshaji wa raslimali za taifa ikiwa ni pamoja na mifugo, samaki na mazao mbalimbali yatokanayo na sekta hizo.

Aidha alisema katika njia zote za panya inashangaza kuona kuna wenyeviti wa vijiji, watendaji wa vijiji, kata, vyombo vyote vya serikali vya ulinzi na usalama pia kuna Mkurugenzi na Mkuu wa Wilaya lakini utoroshaji unaendelea bila wahalifu hao kukamatwa, ambapo aliwataka watendaji wote kuwa waaminifu na kumwagiza Mkuu wa Wilaya kuwachukulia hatua za mara moja watendaji watakaobainika kujihusisha na vitendo viovu ikiwa ni pamoja na rushwa.

Akitolea mfano wa jinsi alivyokamata kilo 65,600 za samaki wachanga aina ya Sangara waliokaushwa kwa chumvi wenye thamani ya shilingi milioni mia tatu katika Kisiwa cha Lubili wilayani Muleba kwenye Mkoa wa Kagera baada ya wamiliki wa samaki hao kukimbia hivi karibuni, alisema zoezi hilo lilifanikiwa baada ya yeye kupata taarifa kutoka kwa raia mwema ambapo aliagiza mamlaka za Wilaya ya Muleba kufuatilia kwa karibu hatimaye kuwakuta samaki hao wakiwa wameanikwa chini katika kisiwa hicho.

“Naomba kusema raia mwema huyo alitoa taarifa siyo kwa sababu alilipwa fedha bali alikuwa na uchungu na uzalendo wa dhati kwa taifa lake baada ya kuona kwamba raslimali ya taifa inatoweka” alihoji Waziri Mpina Aidha, Waziri Mpina alisema Wizara inapambana kuhakikisha kwamba kunakuwa na kodi ya mifugo ambapo kila mfugo utatakiwa kulipiwa kodi tofauti na mfumo wa sasa ambapo hakuna kodi ya moja kwa moja inayotozwa kwa mifugo.

Alisema uanzishwaji wa kodi ya mifugo utasaidia kuleta mapinduzi makubwa ya mifugo katika kipindi kifupi kijacho kwa kuwa fedha itakayokusanywa itatumika katika kununua madawa ya ruzuku kwa mifugo, chanjo, kuboresha malisho na miundombinu mbalimbali ya mifugo ikiwa ni pamoja na majosho na malambo ya kunyweshea maji mifugo hiyo.

Alisema taarifa zilizopo zinaonyesha kuwa asilimia 30 ya mifugo yote nchini inateketea nchini wakati wa jua kali kipindi cha kiangazi kwa sababu ya kukosa maji na malisho bora jambo ambalo ni hasara kubwa kwa taifa. Mbunge wa jimbo la Ngara, mheshimiwa,Alex Raphael Gashaza alipendekeza wafugaji kutambuliwa kwa kulipa kodi ya mifugo na kuanzisha vitalu maalumu vya ranchi za mifugo ili kuthibiti magonjwa na kuinua ubora wa mifugo.

Alisema utaratibu huo pia utapunguza migogoro mingi inayojitokeza sasa baina ya wafugaji na watumiaji wengine wa ardhi ambapo ambapo pia ameipongeza Serikali kwa juhudi inazofanya katika zoezi linaloendelea la kupiga chapa mifugo.

Akitoa ufafanuzi Waziri Mpina alisema Serikali inaruhusu uanzishwaji wa ranchi ndiyo maana suala hilo limezingatiwa katika sheria mbali mbali za tasnia ya mifugo ikiwa ni pamoja na Sheria ya Utambuzi, Usajili na Ufuatiliaji Mifugo Namba 12 ya Mwaka 2010, Sheria ya Nyanda za Malisho na Vyakula vya Mifugo Namba 13 ya Mwaka 2010, na Sheria ya Taasisi ya Utafiti wa Mifugo namba 4 ya Mwaka 2012.

Wakati huo huo, Mkuu wa Wilaya ya Ngara, Luteni Kanali Michael Mtenjele alimweleza Waziri kuwa katika kipindi cha kuanzia Julai hadi Desemba mwaka 2017 jumla ya kilo 903,018 za mazao ya uvuvi kutoka katika maeneo ya Mwanza,Mganza,Kagera, Kigoma na Dar es Salaam yenye thamani ya shilingi bilioni mbili yalikaguliwa na kuhakikiwa na kuruhusiwa kusafirishwa kupitia kituo cha mpakani cha Rusumo.

Aidha alisema kituo cha Rusumo katika kipindi hicho kimekusanya shilingi 7,058,300 kama mrahaba kwa mazao ya uvuvi yanayokwenda nje ya nchi. Akiwa katika ziara hiyo Waziri Mpina alipata fursa ya kuliona na kukagua gari lenye namba za uasajili T 614 CLQ aina ya Mitsubishi Canter lililokamatwa na Kamati ya Ulinzi na Usalama ya Wilaya ya Ngara likiwa limepakia samaki kilo 2,000 aina ya Sangara na kilo 530 wa aina ya Sato zenye thamani ya shillingi 20,850,000/= kwenye mpaka wa Mlusagamba wilayani Ngara tarehe 03/12/2017 saa tatu asubuhi ambapo aliwaelekeza watendaji kuhakikisha taratibu zote za kisheria zinafuatwa ili kuweza kulitaifisha gari hilo kulingana na Sheria ya Uvuvi namba 22 ya mwaka 2003 pamoja na kanuni zake za mwaka 2009 na marekebisho yake ya mwaka 2012 na 2015.

Katika tukio hilo Afisa wa Kitengo cha Doria na Udhibiti wa Uvuvi wa mpakani katika Mkoa wa Kagera bwana Ayoub Ngoma na dereva wa gari hilo Ayoub Sanga walishikiliwa na polisi ambapo Ngoma alisimamishwa kazi mara moja kupisha uchunguzi.

Aidha Mshauri wa Uvuvi wa Mkuu wa Mkoa, Efrazi Mkama na maafisa Uvuvi wa Halmashauri ya Muleba Wilfred Tibendelana na Maengo Nchimani na Afisa Uvuvi wa Halmashauri ya Wilaya ya Bukoba vijijini Renus Ruhuzi wanaendelea kuripoti katika kituo cha polisi Bukoba kwa mahojiano ya kisheria juu ya utoroshwaji wa samaki hao.

No comments:

Post a Comment

Post Bottom Ad