HABARI MPYA

Home Top AdPost Top Ad

Wednesday, 3 January 2018

VIBWEKA, VITUKO VYATAWALA UCHAGUZI NAIBU MEYA DAR

* Meya wa Temeke, Ubungo nusura kuzichapa
 
Na Said Mwishehe, Blogu ya jamii
VITUKO, Vibweka, vitimbi na kila aina ya kejeli zimetawala wakati wa uchaguzi wa Naibu Meya wa Jiji la Dar es Salaam.

Ilikuwa kama wanaigiza filamu lakini kumbe ndio ilikuwa namna ya kufanya uchaguzi huo ambao kwa sehemu kubwa majibizano yalichukua nafasi kubwa.

Uchaguzi wa kumpata Naibu Meya wa Jiji la Dar es Saalam umefanyika leo mchana na ulihusisha mgombea wa Chama Cha Mapinduzi(CCM)Mariam Lorida na mgombea wa Chama cha Wananchi(CUF) Mussa Kafana.

ILIKUWA HIVI
Kabla ya uchaguzi huo kufanyika, vibweka, vitimbi na majibizano yalitawala kati ya Vyama vya siasa vinavyounda Umoja wa Katiba ya Wananchi(Ukawa)dhidi ya upande wa CCM.

Ukawa hawakuwa tayari uchaguzi huo kufanyika kwani mgombea wao hakuwepo ukumbini huku CCM wakiona ipo haja ya kufanyika uchaguzi wa kumpata Naibu Meya ili shughuli za kimaendeleo zifanyike.

Wakati mjadala huo unaendelea Meya wa Jiji la Dar es Salaam Issaya Mwita hakuwepo ukumbini.Hivyo CCM na Ukawa wakawa wanalumbana aidha kufanyika au kutofanyika uchaguzi huo.
Wakati wanalumbana ziliibuka baadhi ya kauli ambazo CCM hawakuridhika nayo na hasa ile iliyodaiwa kutolewa na Meya wa Ubongo Boniphance Jacob baada ya kudai huenda mgombea wao ametekwa.
Kauli ambayo iliwakera baadhi ya wajumbe wa upande wa CCM na hasa Meya wa Temeke Abdallah Chaurembo kutaka Jackob afute kauli yake.

MEYA AINGIA UKUMBINI

Baada ya malumbano ya muda mrefu kati ya Ukawa na CCM, Meya Mwita aliingia ukumbini na kisha kutaka mchakato uendelee.Hata hivyo moja ya kituko ni pale baadhi ya wajumbe wa Ukawa walipoanza kuvua sare(majoho) ili kuounguza akidi ya wajumbe na lengo ni kuhakikisha uchaguzi haufanyiki.

Meya Mwita alitumia busara kushawishi Ukawa kuvaa majoho na kuandika majina yao kwenye kitabu ili kupata idadi halisi ya watakaoshiriki uchaguzi huo.

Pamoja na jitihada hizo Ukawa hawakuwa tayari hadi pale Mkurugenzi wa Jiji la Dar es Salaam Sipora Liana aliposimama na kueleza iwe iwavyo lazima uchaguzi ufanyike.

Hivyo wakati wanaendelea kushawisihi washiriki kujiandikisha ikatakiwa pia mgombea wa Ukawa apelekwe ukumbini.

MGOMBEA AWASILI UKUMBINI
Mgombea wa CUF aliwasili ukumbini akiwa amebebwa na baadhi ya washiriki wa uchaguzi huo akiwamo mbunge wa Ubungo Saed Kubenea, Diwani wa Tabata Patrick Assenga na Meya Jackob.

WASHIRIKI WAINGIWA HURUMA
Hali ya kiafya ya mgombea wa nafasi hiyo kupitia CUF ilifanya washiriki karibu wote kuingiwa huruma kiasi cha kuanza kulaumiana kwanini ameletwa ukumbini.
Hivyo Meya Mwita akaomba ni vema uchaguzi uharishwe ili mgombea apelekwe hospitali.
Hata hivyo , CCM walitaka kabla ya mgonjwa kupelekwa hospitalini ni vema washiriki wote wakajiandikisha.Hapo ikawa kete ya kuwapata Ukawa kwani walikubali kujiandikisha.

Kitendo cha kukubali kwao kujiorodhesha ikawa nafasi kwa Mkurugenzi wa Jiji la Dar es Salaam kueleza wajumbe kuwa washiriki wamejiorodhesha na hatua inayofuata mgombea apelekwe hospitali na kisha uchaguzi uendelee.

Kutokana na mazingira hayo Ukawa wakaaamua mgonjwa asiondoke ili uchaguzi ufanyike.

KURA ZAPIGWA
Vuta ni kuvute ya muda mrefu ikafika tamati baada ya washiriki kukubali kufanya uchaguzi huo.Hivyo idadi ya wajumbe ilikuwa 22 kwa upande wa CCM 11 na Ukawa nao 11.

Baada ya matokeo kutangazwa mgombea wa CUF anayeiwakilisha  Ukawa akaibuka mshindi kwa kura 12 dhidi ya 10 alizopata mgombea wa CCM.

MEYA UBUNGO, TEMEKE NUSURA WAZICHAPE
Baada ya matokeo kutangazwa Meya Jackob alimkaba koo Meya wa Temeke Chaurembo.Sababu ni pale Chaurembo alipotaka kusogelea karatasi za kura.

Hivyo kukaibuka malumbano baina ya pande mbili, kiasi cha baadhi  askari polisi waliokuwa wamevaa kiraia kuamua kuingilia kati ili amani iendelee.

UKAWA WASHANGILIA
Matokeo ya uchaguzi huo yaliibua shangwe kwa Ukawa kwani ushindi huo wameamini umemeliza kiu yao ya kuitaka nafasi hiyo.Kwa mujibu wa nafasi ya Naibu Meya kila baada ta miezi sita wanafanya uchagizi.Hivyo Kafana amerudi tena kwenye nafasi hiyo.

CCM WATAFUTA MCHAWI
Ushindi wa mgombea wa Ukawa ukasababisha CCM kuanza kutafuta nani amewasaliti kwani kwa idadi ya washiriki walikuwa idadi sawa.Hivyo kwa matokeo hauo kuna Diwani wa CCM amewasaliti wenzake .Hali iliyoibua maswali.
  Meya wa Manispaa ya Ubungo, Boniface Jacob  na Meya wa Manispaa ya Temeke Abdalah Chaurembo (aliyekaa chini) wakiwa wanaamuliwa na madiwani wengine  wakati wa uchaguzi wa kumtafuta Naibu Meya wa Jiji la Dar es Salaam leo ambapo  uchaguzi huo ulijawa visa, vituko na vurugu za hapa na pale.
Naibu Meya wa Halmashauri ya Jiji la Dar es Salaam Mussa Kafana (CUF) akiwa amelala ndani ya ukumbi wa Karimjee wakati wa  Uchaguzi wa kumtafuta  Naibu Meya wa Jiji la Dar es Salaam uliofanyika leo jijini Dar es salaam na kuibuka mshindi baada ya kumshinda Mariam Rolida diwani wa  CCM kwa kura ya 12 dhidi ya 10.

 Meya wa Manispaa ya Temeke, Abdalah Chaurembo akizuiwa kuongoza kikao na Diwani wa Chadema Patrick Asenga wakati wa mchakato wa uchaguzi wa kumtafuta Naibu Meya wa Jiji la Dar es Salaam.
 Meya wa Manispaa ya Ubungo, Boniface Jacob (wa kwanza kulia) akizungumza na Madiwani wa Chama cha Mapindzui wakati wa mkutano wa kumtafuta Naibu Meya wa Jiji la Dar es Salaam leo.
  Naibu Meya wa Halmashauri ya Jiji la Dar es Salaam Mussa Kafana akiwa anawasili katika ukumbi wa uchaguzi huku ameshikiliwa na madiwani wenzakeili kuweza  kufanikisha uchaguzi wa Naibu Meya wa Jiji.
 Mkurugenzi wa jiji la Dar es Salaam, Sipora Liana akizungumza na madiwani sambamba na wabunge  wakati wa mkutano wa uchaguzi wa Naibu Meya wa Jiji la Dar es Salaam uliofanyika leo Jijini Dar es Salaam.
 Meya wa Jiji la Dar es Salaam Isaya Mwita akizungumza wakati wa mkutano wa uchaguzi wa Naibu Meya wa Jiji la Dar es Salaam uliofanyila leo Jijini Dar es Salaam.

No comments:

Post a Comment

Post Bottom Ad