HABARI MPYA

Home Top AdPost Top Ad

Thursday, 4 January 2018

TPA yanunua vifaa vya kisasa Bandari ya Mtwara

 Mkuu wa bandari ya Mtwara, Nelson Mlali (Kulia) akitoa maelezo kwa Wakurugenzi wa Bodi wa TPA wa Kamati za TEHAMA na Utekelezaji pamoja na ya Uwekezaji na Maendeleo ya Biashara mara baada ya wajumbe wa kamati hizo kufanya ziara ya kikazi bandari ya Mtwara hivi karibuni.
Mkuu wa bandari ya Mtwara, Nelson Mlali (Kulia) akitoa maelezo kwa Wakurugenzi wa Bodi wa TPA wa Kamati za TEHAMA na Utekelezaji pamoja na ya Uwekezaji na Maendeleo ya Biashara mara baada ya wajumbe wa kamati hizo kufanya ziara ya kikazi bandari ya Mtwara hivi karibuni.

Na Mwandishi Wetu
Mamlaka ya Usimamizi wa Bandari Tanzania (TPA) imenunua vitendea kazi vipya na vya kisasa kwa ajili ya bandari ya Mtwara ili kuongeza ufanisi.
Vifaa hivyo ambavyo tayari baadhi vimeshawasili bandarini hapo ni pamoja na mzani wa kisasa ‘Movable Weigh Bridge’ wenye uwezo wa kupima hadi tani 100 ambao tayari unatumika.
Vifaa vingine vilivyonunuliwa na vinavyotarajiwa kuwasili kuanzia mwezi Januari, 2018 ni pamoja na ‘Reach Stalker’ mbili mpya zenye uwezo wa kubeba tani 40 kwa wakati mmoja.
Mkurugenzi Mkuu wa TPA, Mhandisi Deusdedit Kakoko ameyasema hayo wakati wa majumuisho ya ziara za Kamati za Bodi za Wakurugenzi wa TPA zinazoshughulikia TEHAMA na Utelekezaji na ile ya Uwekezaji na Maendeleo ya Biashara.
Wakurugenzi wa Bodi za Kamati hizo ambazo ziliongozwa na Mwenyekiti, Dkt. Jabiri K. Bakari, ni pamoja na Jayne K. Nyimbo, Renatus Mkinga, Aziz M. Kilonge na Jaffer S. Machano.
Kamati hizo zilitembelea miradi mbalimbali iliyopo Bandari za Mtwara na Lindi na kutoa maelekezo kadhaa ambayo ni muhimu katika kuendeleza bandari hizo ili kuongeza huduma zake.
Akizungumzia vifaa vipya vilivyowasili na vinavyotarajiwa kuwasili hivi karibuni, Mhandisi Kakoko amesema ununuzi wa vifaa hivyo ni utekelezaji wa mipango ya kuifanya bandari hiyo kuwa ya kisasa zaidi.
“Ununuzi wa vifaa tunaofanya sasahivi utasaidia kuboresha na kuimarisha zaidi utendaji kazi wa bandari ya Mtwara na kuongeza ufanisi zaidi,” amesema Mhandisi Kakoko.
Mhandisi Kakoko ameongeza kwamba vifaa vingine ambavyo mchakato wa manunuzi umeshafanyika ni pamoja na mzani mwingine wa pili wa kisasa ‘Movable Weigh Bridge’ wenye uwezo wa kupima hadi tani 100 pia.
Amevitaja vifaa vingine kuwa ni pamoja na boti maalum za kuhudumia mafuta ‘Mooring Boat’ moja na boti moja ya ulinzi ‘Pilot Boat’.
Mbali ya vifaa hivyo, bandari ya Mtwara pia itapokea ‘Terminal Tractors’ 9 - matrekta maalumu yanayovuta ‘matrela’ yaliyopakiwa kontena au makontena yakiwa bandarini.
Bandari ya Mtwara pia inatarajia kupokea mashine maalum ya kubebea makontena ‘Empty Container Handler’, folklift mbili moja ya tani 16 na nyingine tani 20 pamoja na ‘Automatic Glab moja ya tani 15. 
Kama sehemu ya ziara hiyo, Mhandisi Kakoko pia alifanya kikao na maofisa wa Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA) Mtwara na kuwaagiza kukutana na Mawakala wa Forodha wa Mtwara ili kuwaelimisha umuhimu wa kutoa mizigo ya wateja kwa wakati.
Awali akitoa maelezo kwa Kamati ya Bodi ya Wakurugenzi wa TPA inayoshughulikia TEHAMA na Utelekezaji, Naibu Mkurugenzi Mkuu wa TPA (Miundombinu) Mhandisi Karim Mattaka amesema vifaa hivyo vitawasili bandari ya Mtwara kuanzia mwezi ujao.
“Tunatarajia kuanza kuwasili kwa vifaa hivyo hapa Mtwara kuanzia mwezi ujao (Januari, 2018) ili kuharakisha mpango kazi wetu wa kubadili bandari hii,” amesema.
Naye Mkuu wa Bandari ya Mtwara, Bw. Nelson Mlali amesema kwamba kuna ongezeko la mizigo la wastani wa asilimia 16.5 kwa mwaka kwa kipindi cha miaka mitano.
“Katika mwaka 2016/2017, Bandari ya Mtwara imehudumia wastani wa tani 377,590 za mizigo ambazo ni sawa na asilimia 93 ya uwezo wa bandari, ambapo uwezo wake ni kuhudumia tani 400,000 kwa mwaka” amesema.
Bw. Mlali amesema kwamba ongezeko hilo limechangiwa zaidi na ongezeko la uzalishaji wa Korosho ambalo ndilo zao kuu la biashara kwa mikoa ya kusini.
Amesema kwamba zao la Korosho ambalo hulimwa zaidi na wakazi wa mikoa ya kusini hupitishwa katika bandari ya Mtwara na kusafirishwa moja kwa moja kwenda nchi za Vietnam na India.
Kwa mwaka huu pekee bandari ya Mtwara ambayo ina uwezo wa kuhudumia meli zenye urefu hadi wa mita 211 imefanikiwa kusafirisha wastani wa tani 160,000 za Korosho hadi kufikia Disemba, 2017.
Mkuu huyo wa bandari ya Mtwara amepongeza juhudi zilizofanywa na Serikali ya Awamu ya tano inayoongozwa na Rais John Pombe Magufuli kuagiza Korosho zote zisafirishwe kupitia bandari ya Mtwara.
Mbali ya Korosho bandari ya Mtwara pia uhudumia shehena nyingine za mizigo kama vile, saruji, vifaa mbalimbali na mafuta.

No comments:

Post a Comment

Post Bottom Ad