HABARI MPYA

Home Top Ad

Post Top Ad

Monday, January 15, 2018

SERIKALI YATOA UFAFANUZI WA MATUMIZI YA FEDHA ZA KIGENI

Naibu Waziri wa Fedha na Mipango, Mhe. Dkt. Ashatu Kijaji (Mb) akifafanua kuhusu matumizi ya fedha za kigeni ambapo alieleza kuwa Serikali imedhibiti matumizi ya fedha hizo ili kulinda thamani ya shilingi wakati wa Mkutano wa Naibu Waziri huyo na Wafanyabiashara wa Mkoa wa Arusha. (Picha na Kitengo cha Mawasiliano Wizara ya Fedha na Mipango).
 Naibu Waziri wa Fedha na Mipango, Mhe. Dkt. Ashatu Kijaji (kulia) pamoja na meza kuu wakimsikiliza kwa makini mmoja wa wafanyabiashara (hayupo pichani) aliyekuwa akiuliza kuhusu matumizi ya fedha za kigeni wakati wa Mkutano kati ya Naibu Waziri huyo na Wafanyabiashara wa Mkoa wa Arusha.
 Baadhi ya Wafanyabiashara wa Mkoa wa Arusha wakiwa katika mkutano na Naibu Waziri wa Fedha na Mipango, Mhe. Dkt. Ashatu Kijaji (Mb) (hayupo pichani) kuhusu ukuzaji wa Sekta ya Biashara Jijini Arusha.

Na:  WFM
Serikali haijazuia matumizi ya fedha za kigeni nchini bali imechukua hatua ya kudhibiti matumizi ya fedha hizo ili kulinda thamani ya Shilingi ya Tanzania.
Hayo yalielezwa na Naibu Waziri wa Fedha na Mipango Mhe. Dkt. Ashatu Kijaji (MB) alipokutana na wawakilishi wa wafanyabiashara mkoani Arusha kujadiliana mambo mbalimbali kwa ajili ya kukuza sekta ya  biashara nchini. 

Amesema kuwa sheria haijazuia matumizi ya fedha za kigeni nchini lakini inasisitiza kuwa watu wanapaswa kutambua kuwa sarafu ndiyo fedha halali kwa malipo ndani ya nchi.
“Tatizo kubwa tunalokumbana nalo ni uhuru ulioachiwa ambao unasababisha kushuka kwa thamani ya Shilingi yetu kwani kila mmoja anaweza kutumia fedha za kigeni pia watumiaji wa fedha za kigeni hawafuati thamani ya fedha iliyoko sokoni kila mmoja anakuwa na kiwango tofauti cha thamani ya kubadili fedha za kigeni”. alifafanua Dkt. Kijaji.

Ili kuondoa changamoto hizo Serikali imeamua kurekebisha sheria ya matumizi ya fedha za kigeni na sheria ya Benki Kuu huku ambayo inazitaka  bei zote hapa nchini zitangazwe kwa Shilingi ya Tanzania. Bei hizi zinajumuisha kodi za nyumba za kuishi na ofisi, bei za ardhi, gharama za elimu na afya, bei za vyombo vya usafiri na vifaa vya kielektroniki. 

“Bei ambazo walengwa wake wakuu ni watalii au wateja ambao sio wakazi zinaweza kutangazwa kwa fedha za kigeni na malipo yake yanaweza kufanyika kwa fedha za kigeni. Hata hivyo kama mlengwa akitaka kulipa kwa Shilingi ya Tanzania asilazimishwe kulipa kwa fedha za kigeni” alieleza Dkt. Kijaji.

Aidha, viwango vya kubadilishia fedha vitakavyotumika katika kuweka hizo bei katika sarafu nyingine vimetakiwa kuwekwa wazi na visizidi vile vya sokoni. 
Mkazi yeyote wa Tanzania au mtu wa nje anayeishi Tanzania  asilazimishwe kufanya malipo yoyote kwa kutumia fedha za kigeni kama ana Shilingi ya Tanzania mkononi mfano gharama za shule na hoteli.

Aidha Serikali imeagiza vyombo vya dola kuchukua hatua za kisheria kwa wote watakaokiuka maagizo hayo yaliyotolewa na Serikali.
Naibu Waziri Dkt. Kijaji alitoa rai kwa wafanyabiashara nchini kuhimiza matumizi ya sarafu ili kuweza kukuza thamani ya Shilingi hivyo kusaidia kuinua uchumi wa nchi. 

No comments:

Post a Comment

Post Bottom Ad