HABARI MPYA

Home Top AdPost Top Ad

Monday, 22 January 2018

RC MARA TOKOMEZA UVUVI HARAMU ZIWA VICTORIA-MAJALIWA

WAZIRI MKUU Kassim Majaliwa amemuagiza  Mkuu wa Mkoa wa Mara, Bw. Adam Malima kwa kushirikiana na Kamati ya Ulinzi na Usalama ya mkoa  wahakikisha wanatokomeza uvuvi haramu katika ziwa Victoria.

Waziri Mkuu alitoa agizo hilo jana (Jumapili, Januari 21, 2018) wakati akizungumza na viongozi wa mkoa huo katika kikao cha majumuisho ya ziara yake ya kikazi  mkoani Mara.

“Kuna tatizo kubwa la uvuvi haramu katika Ziwa Viktoria. Fanyeni doria za mara kwa mara na watakaobainika hatua stahiki za kisheria zichukuliwe dhidi yao.”

Alisema viongozi hao wanatakiwa wahakikishe wanatokomeza  uvuvi haramu haraka iwezekanavyo na pia wasimamie ulinzi wa rasilimali za ziwa Victoria ili ziweze kuwanufaisha wananchi wa mkoa huo na Taifa kwa ujumla.

Waziri Mkuu alisema baadhi ya wavuvi wamekua wakivua kwa kutumia nyavu zilizopigwa marufuku, kokoro pamoja na mabomu jambo ambalo haliwezi kuvumilika kwa sababu zana hizo zinaharibu uhai wa viumbe hai ndani ya ziwa Victoria.

Alisena ni vema mkoa huo ukaanzisha operesheni za mara kwa mara  katika ziwa Victoria kwa lengo la kuwasaka watu wote wanaojihusisha na vitendo vya uvuvi haramu na kuwachukulia hatua kali za kisheria kwa wote watakaokamatwa.

Awali, Waziri Mkuu alizindua jengo la mama na mtoto pamoja na nyumba za watumishi katika kituo cha afya cha Murangi kilichopo Halmashauri ya wilaya ya Musoma Vijijini.

Pia Waziri Mkuu akiambatana na Mkewe Mama Mary Majaliwa walitembelea nyumba ya kihistoria ambayo Baba wa Taifa marehemu Mwalimu Julius Nyerere alifikia akiwa katika harakati za kutafuta Uhuru, 1954. Nyumba hiyo ipo kata ya Murangi.

Akizungumzia kuhusu nyumba hiyo ambayo baadae ilitumika kama ofisi ya chama cha TANU kwa upande wa Majita, alisema ni lazima eneo hilo liendelee kudumishwa kwa sababu linabeba historia muhimu kwa Taifa.

Baada ya kutembelea nyumba hiyo, Waziri Mkuu aliwahutubia wakazi wa Halmashauri hiyo katika mkutano wa hadhara uliofanyika uwanja wa Murangi,  ambapo alitumia fursa hiyo kueleza juhudi mbalimbali za kuwaletea maendeleo zinazofanywa na Serikali ya Awamu ya Tano, inayoongozwa na Rais Dkt. John Magufuli.

IMETOLEWA NA:
OFISI YA WAZIRI MKUU
JUMATATU, JANUARI 22, 2018.

No comments:

Post a Comment

Post Bottom Ad