HABARI MPYA

Home Top AdPost Top Ad

Friday, 12 January 2018

Meli ya MV Ruvuma kufungua fursa za kiuchumi Nyasa

Naibu Waziri wa Viwanda na Biashara, Mhandisi Stellah Manyanya ambaye pia ni Mbunge wa Nyasa akishangilia sambamba na Kaimu Mkuu wa Bandari za Ziwa Nyasa, Bw. Ajuaje Msese wakati wa ujio wa meli hiyo ikiwa na shehena ya mzigo wa Saruji toka Kyela.
 Meli ya MV Ruvuma ikishusha shehena ya kwanza ya Saruji katika bandari ya Mbambabay mara baada ya kufanya safari yake ya kwanza ikiwa na shehena ya mzigo kutoka bandari Kyela hadi hapo Mbambabay, mjini Nyasa.

Na Mwandishi Wetu
Naibu Waziri wa Viwanda na Biashara, Mhandisi Stella Manyanya ambaye pia ni Mbunge wa jimbo la Nyasa amesema kwamba kuanza kwa safari kwa Meli ya kisasa ya mizigo ya M.V. Ruvuma kutafungua fursa za kiuchumi za mkoa wa Ruvuma kwa ujumla.
Katika salaam zake za kumkaribisha Waziri Mkuu Kassim Majaliwa katika jimbo lake la Nyasa, Mhe. Manyanya amewataka wakazi wa Nyasa na Wilaya za jirani kutumia fursa ya uwepo wa meli hiyo kujikwamua kiuchumi.
"Kuanza kwa safari ya meli hii ndiyo ufunguo wa kufungua fursa za kiuchumi za mkoa wetu, hivyo napenda kutumia nafasi hii kuwasihi wananchi wa Nyasa watumie fursa ya kuanza safari kwa meli hii kujikwamua kiuchumi," amesema Mhandisi Manyanya.
Mhandisi Manyanya amesisitiza kwamba kama kuna mwananchi yeyote wa Nyasa ambaye ataendelea kulia njaa au hali ngumu ya kiuchumi basi huyo atakuwa amejitakia mwenyewe, aliongeza.
Meli ya mizigo ya MV Ruvuma ambayo ina uwezo wa kubeba shehena ya tani 1,000 za mizigo imefanya safari yake ya kwanza toka bandari ya Kyela hadi Mbambabay ikiwa na shehena ya Saruji.
Naibu Waziri amesema kwamba moja ya manufaa ya kuanza kwa safari za meli hizo ni pamoja na kufungua biashara kati Nyasa na mikoa jirani.
Mbali na kufungua biashara, meli hizo pia zitasadia kufanya bandari zilizo katika Ziwa Nyasa kuamka ambapo pia shughuli mbalimbali za kiuchumi zitakuwa zikiendelea katika bandari hizo.
Kuanza safari kwa meli hiyo na ile ya MV Songea pia kunatarajiwa kufungua milango ya ajira kwa wananchi wa mikoa iliyo pembezoni mwa Ziwa Nyasa.
Meli za mizigo za MV Ruvuma na MV Njombe ni moja kati ya meli tatu zilizotengenezwa na kuendeshwa na Mamlaka ya Usimamizi wa Bandari Tanzania (TPA) kwa ajili ya kutoa huduma kwenye mikoa ya Mbeya, Ruvuma, Songea na nchi jirani za Malawi na Msumbiji.
Meli hizo za kisasa zenye uwezo wa kubeba shehena yenye uzito wa tani 1,000 kila moja zimekuwa mkombozi kwa wananchi wa mikoa hiyo ambao walikuwa hawana uhakika wa usafiri katika ziwa hilo kwa kipindi kirefu.
Tangu kuzinduliwa rasmi kwa meli hizo na Waziri Mkuu Mhe. Kassim Majaliwa mwaka jana, kumekuwa na mwitikio mkubwa wa wafanyabiashara na wananchi wa kawaida kutaka kuzitumia meli kusafirisha bidhaa zao.
Bidhaa kubwa zinazotarajiwa kusafirishwa na meli hizo ni pamoja na makaa ya mawe toka Ngaka, Saruji toka kiwanda Saruji cha Mbeya na Dangote pamoja na 'Clinker'.
Ujenzi wa meli hizo mbili za mizigo ulianza Mwaka 2015, ukiwa na lengo la kutoa huduma ya usafirishaji wa shehena ya makaa ya mawe kutoka Bandari ya Ndumbi, pamoja na mizigo mingine katika Ziwa Nyasa. 
Bidhaa nyingine ni pamoja na usafirishaji wa makaa ya mawe kwenda Mbeya kupitia bandari ya Kiwira pamoja na bandari mbalimbali nchini Malawi.

Imetolewa na Mamlaka ya Usimamizi wa Bandari Tanzania (TPA).

No comments:

Post a Comment

Post Bottom Ad