HABARI MPYA

Home Top Ad

Post Top Ad

Wednesday, January 3, 2018

HESLB kuanza kuwasaka wadaiwa sugu 119,497 jumatatu ijayo

Mkurugenzi Mtendaji wa Bodi ya Mikopo ya Wanafunzi wa Elimu ya Juu Abdul-Razaq Badru akiongea na wanahabari leo (Jumatano, Jan. 3, 2018) jijini Dar es Salaam ambapo alielezea utekelezaji wa majukumu ya taasisi yake katika nusu ya mwaka 2017/2018 na kuanza kwa kampeni ya kuwasaka wanufaika sugu wa mikopo 119,497 ambao hawajaanza kurejesha. Kulia kwake ni Mkurugenzi wa Upangaji Mikopo Dkt. Veronika Nyahende na kushoto ni PHIDELIS Joseph, Mkurugenzi Msaidizi wa Urejeshaji Mikopo (Picha na Happiness Kihwele- HESLB).

*  Wanadaiwa Tshs 285 bilioni
*  Ukaguzi kwa waajiri pia kufanyika

Na Mwandishi Wetu

Bodi ya Mikopo ya Wanafunzi wa Elimu ya Juu (HESLB) wiki ijayo (Jumatatu, Januari 8, 2018) inatarajia kuanza kuwasaka jumla ya wanufaika 119,497 nchini kote ambao wamekiuka sheria iliyoanzisha Bodi hiyo kwa kutoanza kurejesha mikopo yenye thamani ya TZS 285 bilioni waliyokopeshwa tangu mwaka 1994/1995 na mikopo yao imeiva lakini hawajaanza kurejesha.

Aidha, Bodi ya Mikopo inatarajia kuanza kufanya ukaguzi kwa waajiri mbalimbali nchini kote ili kubaini kama katika orodha za waajiriwa wao (payrolls) kuna wanufaika wa mikopo ambao hawajaanza kurejesha.

Mkurugenzi Mtendaji wa HESLB Bw. Abdul-Razaq Badru (pichani) amesema leo (Jumatano, Januari 3, 2018) jijini Dar es Salaam kuwa msako huo utafanywa kwa miezi mitatu kuanzia wiki ijayo (Jumatatu, Januari 8, 2018).

Bw. Badru ametoa kauli hiyo wakati akitoa tathmini ya utekelezaji wa majukumu ya Bodi ya Mikopo kwa nusu ya mwaka wa fedha wa 2017/2018 uliomalizika Desemba 31, 2017. Katika tathmini hiyo, Bw. Badru alizungumzia mafanikio, changamoto na mipango ya kuboresha ufanisi katika utoaji wa mikopo ya elimu ya juu na ukusanyaji wa mikopo iliyoiva.

Maafisa wa Bodi kwa kushirikiana na vyombo vingine vya Serikali wamejipanga katika kutekeleza hili ili kuongeza makusanyo ya mwezi kutoka wastani wa TZS 13 bilioni hivi sasa hadi kufikia TZS 17 bilioni mwezi Juni, 2018.

Orodha kamili ya waajiri na wanufaika wa mikopo ambao wanakiuka Sheria ya Bodi ya Mikopo (SURA 178) kwa kutowasilisha makato au kurejesha mikopo ya elimu ya juu inapatikana katika tovuti ya Bodi ya Mikopo (www.heslb.go.tz) kuanzia leo (Jumatano, Januari 3, 2018).

Kampeni ya Kuwasaka Waajiri na Wanufaika wasiorejesha mikopo
Akifafanua zaidi, Bw. Badru amesema ingawa kila mwajiri ana wajibu wa kisheria wa kuwasilisha makato ya wanufaika wa mikopo ya elimu ya juu kwa Bodi ndani ya siku 15 baada ya mwisho wa mwezi, baadhi ya waajiri wamekuwa hawafanyi hivyo na kuilazimisha Bodi ya Mikopo kuanza kuwasaka kwa nguvu.

“Katika msako huu hatutamuacha mtu au mwajiri yeyote anayekiuka sheria iliyoanzisha Bodi,” amesema Bw. Badru katika mkutano na wanahabari na kufafanua kuwa sheria iliyoanzisha Bodi ya Mikopo inawapa mamlaka ya kufanya ukaguzi na ni kosa kisheria kwa mtu yeyote kuzuia ukaguzi huo.

“Tayari tumeziongezea nguvu ofisi zetu za Kanda zilizopo Mwanza, Arusha, Dodoma na Zanzibar ili kuendesha ukaguzi na msako katika mikoa yao na ile iliyo karibu nayo ili kuhakikisha kazi hii inafanyika kwa ufanisi,” amesema Bw. Badru na kuongeza kuwa ukaguzi huo pia utafanyika jijini Dar es Salaam.   

Hali ya Ukusanyaji wa Mikopo iliyoiva hadi 2017/2018
Akizungumza kuhusu hali ya ukusanyaji wa mikopo iliyoiva hadi kufikia Desemba 31, 2018, Mkurugenzi Mtendaji huyo amesema kiasi cha TZS 85 bilioni kilikuwa kimekusanywa huku lengo la makusanyo kwa mwaka mzima wa fedha utakaomalizika Juni 30, 2018 ni TZS 130 bilioni.

“Katika kazi hii ya ukusanyaji, kwa miezi hii sita tumewabaini wanufaika wapya zaidi ya 26,000 na wameanza kulipa na kufanya jumla ya wanufaika wanaolipa hadi sasa kuwa zaidi ya 121,000,”amesema Bw. Badru na kuwashukuru waajiri wote wanaotimiza wajibu wao.

Kuhusu changamoto inayokutana nazo katika kazi ya ukusanyaji wa mikopo, Bw. Badru amesema baadhi ya waajiri kutowasilisha kwa Bodi ya Mikopo orodha za waajiriwa ambao ni wahitimu wa taasisi za elimu ya juu kama sheria inavyotaka. Aidha, changamoto nyingine ni kutowasilisha makato ya wanufaika kwa Bodi kwa wakati.

Hali ya Utoaji Mikopo kwa Mwaka 2017/2018
Kuhusu utoaji mikopo kwa wanafunzi wahitaji, Mkurugenzi Mtendaji huyo amesema katika mwaka huu wa masomo, jumla ya wanafunzi 122,623 wamepata mikopo yenye thamani ya TZS 422.45 bilioni. Kati yao, wanafunzi 33,244 ni wa mwaka wa kwanza waliopata mikopo yenye thamani ya TZS 110.37 bilioni na wengine 89,379 ni wanaoendelea na masomo ambao wamepata mikopo yenye thamani ya TZS 312.16 bilioni.

Katika mwaka wa masomo uliopita (2016/2017), jumla ya wanafunzi 112,409 walipangiwa mikopo yenye thamani ya TZS 409.61 bilioni. Kati ya hao, wanafunzi 28,383 walikuwa wa mwaka wa kwanza na wengine 86,688 walikuwa wanaendelea na masomo.



Bodi ya Mikopo ilianzishwa kwa sheria mwaka 2004 na kuanza kazi rasmi Julai 2005. Majukumu makuu ya Bodi ya Mikopo ni kutoa mikopo kwa watanzania wahitaji wenye sifa na kukusanya mikopo iliyoiva ili iweze kukopeshwa kwa wahitaji.

No comments:

Post a Comment

Post Bottom Ad