HABARI MPYA

Home Top Ad

Post Top Ad

Saturday, January 13, 2018

CUBA YAKUBALI KUSOMESHA MADAKTARI KUTOKA ZANZIBAR

Serikali ya Jamuhuri ya Cuba imetiliana Saini Mkataba na Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar kwa Usomeshwaji wa Madaktari Wazalendo 15 wa Zanzibar Nchini Cuba katika Fani ya Shahada ya Uzamili ya Udaktari.


Madaktari hao 15 ambao Wanane wa Mwanzo wataanza Mafunzo yao Mwezi ujao wakifuatiwa na wengine 7 wa awamu ya Pili ni Miongoni mwa Wanafunzi waliomaliza masomo yao kupitia mpango wa masomo ulioasisiwa kati ya Serikali ya Cuba na Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar.

Saini ya Mkataba huo kwa Serikali ya Cuba imewekwa na Balozi wa Nchi hiyo Nchini Tanzania Profesa Lucas Domingo Hernades na kwa upande wa Zanzibar Saini ikatiwa na Naibu Katibu Mkuu Wizara ya Afya Zanzibar Bibi Halima Maulid Salum.

Hafla hiyo fupi ya Kihistoria imeshuhudiwa na Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar Balozi Seif Ali Iddi aliyejumuika pamoja na baadhi ya Mawaziri wa Wizara husika, Watendaji wa Wizara hizo na kufanyika Ofisini kwake Vuga Mjini Zanzibar.

Akizungumza katika hafla hiyo Balozi wa Jamuhuri ya Cuba Nchini Tanzania Profesa Lucas Domingo Hernades alisema Cuba bado inaendelea kutafakari maeneo mapya zaidi inayoweza kushirikiana na Zanzibar katika kuendelea kupiga hatua kubwa zaidi za Kiuchumi na Maendeleo.

Balozi Lucas alisema suala la kuwafanya Wananchi wa Visiwa vya Unguja na Pemba wanakuwa katika ustawi ulio bora zaidi wa afya na kipato limepewa kipaumbele na Serikali ya Cuba kuliko jambo jengine lolote la ushirikiano wa pande hizo mbili.

Balozi wa Cuba Nchini Tanzania alielezea faraja yake kutokana na ukarimu anaoushuhudia wa Watu wa Zanzibar kwa wageni jambo ambalo limempa nguvu na ari zaidi ya kuona jinsi gani anaweza kuitumia fani yake ya Diplomasia katika kudumisha udugu wa pande hizo mbili.

Naye Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar Balozi Seif Ali Iddi alisema mkataba huo wa Usomeshwaji wa Madaktari Wazalendo wa Zanzibar Nchini Cuba umejenga historia mpya ya ushirikiano kati ya Zanzibar na Cuba katika Sekta ya Afya kuelekea mfumo wa kisasa wa Sayansi na Teknolojia Ulimwenguni.

Balozi Seif aliishukuru na kuipongeza Jamuhuri ya Cuba kupitia Balozi wake Nchini Tanzania kwa ukarimu wake wa kupungua kima cha malipo kwa Wanafunzi hao wa Fani ya Udaktari katika ngazi ya Shahada ya Uzamili ya Udaktari.

Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar alimuhakikishia Balozi Lucas Domingo kwamba Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar na ile ya Jamuhuri ya Muungano wa Tanmzania zitaendelea kuupa ushirikiana ubalozi huo ili uendelee kutekeleza vyema majukumu yake ya Kidiplomasia.

Mapema Waziri wa Afya Zanzibar Mheshimiwa Mahmoud Thabit Kombo alisema uhusiano wa Sekta ya Afya kati ya Zanzibar na Cuba umeanza kupata baraka zaidi kufuatia Ziara ya Rais wa Zanzibar Dr. Ali Mohamed Shein wakati akiwa Makamu wa Rais wa Jamuhuri ya Muungano wa Zanzibar aliyoifanya Nchini Cuba Mnamo Mwaka 2008.

Mh. Mahmoud alisema baraka hizo zimewezesha kuanzishwa kwa Chuo cha Madaktari Zanzibar ambacho tayari kimeshazalisha Madaktari Wazalendo 50 waliosomeshwa chini ya Wahadhiri na Wataalamu kutoka Cuba kupitia mpango wa masomo ulioasisiwa kati ya Zanzibar na Cuba.

Waziri Mahmoud alifahamisha kwamba mafunzo hayo yamekuwa yakiendelea kwa makundi mengine ya Udaktari kila Mwaka ambapo mfumo uliopo hivi sasa kwa mafunzo hayo umejumuishwa na Chuo Kikuu cha Taifa cha Zanzibar {SUZA}.

Alisema ushirikiano wa Kidiplomasia kati ya Jamuhuri ya Cuba na Zanzibar umeasisiwa Mnamo Mwaka 1964, Cuba ikiwa ni miongoni mwa Mataifa Matano ya Kwanza yaliyoitambua Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar mara baada ya Mapinduzi Matukufu ya Zanzibar ya Mwaka 1964.

Jamuhuri ya Cuba kupitia Balozi wake Nchini Tanzania katika Mkataba huo uliowekwa saini imeridhia kupungua kima cha malipo kwa kila Mwanafunzi katika Kundi hilo la Madaktari 15 Wazalendo wa Zanzibar katika ngazi ya Shahada ya Uzamili ya Udaktari.

Othman Khamis Ame
Ofisi ya Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar

Balozi wa Cuba Nchini Tanzania Profesa Lucas Domingo Kushoto na Naibu Katibu Mkuu Wizara ya Afya ya Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar Bibi Halima Maulid Salum wakisaini Mkataba wa Usomeshwaji wa Madaktari Wazalendo 15 wa Zanzibar Nchini Cuba katika Fani ya Shahada ya Uzamili ya Udaktari.Nyuma yao ni Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar Balozi Seif Ali Iddi na aliye simama mbele yao ni msaidizi wa Balozi wa Cuba Meylin Suarez.
Profesa Lucas Domingo Kushoto na Naibu Katibu Mkuu Wizara ya Afya ya Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar Bibi Halima Maulid Salum wakibadilishana nyaraka za Mikataba mara baada ya kusaini.
Balozi Lucas Domingo akizungumza kabla ya utiaji saini kwenye Ofisi ya Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar iliyopo Vuga Mjini Zanzibar. Wa kwanza kushoto ni Makamu wa Pili wa Zanzibar Balozi Seif Ali Iddi na Waziri wa Afya Zanzibar Mheshimwa Mahmoud Thabit Kombo.
Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar Balozi Seif kati kati waliokaa vitini akiwa katika picha ya pamoja na Uongozi wa Wizara ya Afya Zanzibar na ule wa Ubalozi wa Cuba Nchini Tanzania. Kulia ya Balozi Seif ni Balozi wa Cuba Prifesa Lucas Domingo na Waziri wa Nchi Ofisi ya Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar Mh. Moha’d Aboud Moha’d, Kushoto ya Balozi Seif ni Waziri wa Afya Mh. Mahmoud Thabit Kombo na Msidizi wa Balozi Cuba Nchini Tanzania Bibi Meylin Suarez.
Balozi Lucas Domingo Kushoto akibadilishana mawazo na Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar Balozi Seif mara baada ya utiaji saini mkataba wa usomeshwaji wa Madaktari wa Zanzibar Nchini Cuba.
Balozi Seif kati kati akiagana na Msaidi wa Balozi wa Cuba Nchini Tanzania Bibi Meylin Suarez wakati Balozi Wake kushoto yake akifurahia itendo hicho.
Balozi Lucas Domingo Kushoto akibadilishana mawazo na Waziri wa Nchi Ofisi ya Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar Mheshimiwa Moh’d Aboud Moh’d.
Nyuma na Mheshimiwa Moh’d Aboud ni Katibu Mkuu Wizara ya Nchi Ofisi ya Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar Dr. Idriss Muslim Hijja.

Waziri wa Afya Mh. Mahmoud Thabit Kombo Kushoto akiwa katika Picha ya Pamoja na Balozi wa Cuba Nchini Tanzania Profesa Lucas Domingo Kulia na Msaidizi wake Bibi Meylin Suarez pamoja na Mtoto wake. Picha na – OMPR – ZNZ.

No comments:

Post a Comment

Post Bottom Ad