HABARI MPYA

Home Top AdPost Top Ad

Saturday, 27 January 2018

BALOZI SEIF AHIMIZA WANANCHI KUJITOKEZA KWA WINGI KUCHANGIA DAMU

Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar Balozi Seif Ali Iddi alisema wakati umefika kwa kila Mwananchi kujiwekea utaratibu wa kujitokeza kuchangia Damu ili kuhakikisha muda wote Hospitali Nchini zinakuwa na Damu ya kutosha kwa lengo la kuwahudumia wagonjwa pale yanapojitokeza mahitaji.

Alisema jamii inapaswa kuelewa kwamba hakuna zawadi nzuri na yenye thamani kubwa kwa Binaadamu kuliko kumchangia Damu mwenzake na kumuwezesha kuokoa maisha yake pale inapojitokeza haja hiyo.

Balozi Seif Ali Iddi alisema hayo kwenye Tamasha la uchangiaji Damu salama lililoandaliwa na Jumuiya ya kuwaendeleza Wanawake na Vijana na kufanyika katika Viwanja vya Mnara wa Kumbukumbu ya Mapinduzi Kisonge Michenzani Mjini Zanzibar.

Alisema hadi sasa mwitikio wa Wananchi kujitokeza kuchangia Damu haujawa wa kuridhisha hali ambayo hufikia wakati ikawa ni hatari kubwa katika Benki za Damu kutokana na baadhi ya Wananchi kutojitokeza kabisa kuchangia Damu salama.

Balozi Seif ambae aliyapokea Maandamano ya Wananchi waliyoyafanya kuhamasisha jamii kupenda Utamaduni wa kuchangia Damu alisema wapo Watu wenye tabia ya kutoa visingizio tofauti katika kuchangia Damu kwa kujifanya hawana muda wa kufanya hivyo kutokana na kutingwa na mambo mengi ya Kimaisha.

Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar alieleza pia kwamba wamo miongoni mwa Wananchi wenye tabia ya kukisita kujitokeza kuchangia Damu kutokana na hofu mbali mbali ikiwemo kutojiamini juu ya afya zao.

Balozi Seif aliwanasihi Wananchi wote wenye fikra hizo kuona kwamba hatua ya kuchangia Damu ni fursa nyengine ya kipekee katika kuelewa afya yake Mtu licha ya kumsaidia Mwananchi mwenzake mwenye mahitaji ya huduma hiyo muhimu.

Alifahamisha kwamba jambo la kuchangia Damu ni la kila mwana Jamii Hivyo inapasa kila Mwananchi Akaelewa kwamba mahitaji ya Damu yanaweza kumkuta Mtu ye yote na wakati wowote kutokana mitihani inayowazunguuka na kuwakumba.

“ Tufanye hivyo kwa kuelewa mahitaji ya Damu huweza kumkuta kila mmoja wetu. Kama si wewe basi jua kwamba Mtoto wako, ndugu yako au hata jirani yako anaweza kuhitaji msaada wa Damu”. Alisema Balozi Seif.

Alisema Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar kupitia Wizara ya Afya na kwa kushirikiana na wadau wa Maendeleo imeanzisha juhudi za makusudi katika kuanzisha Benki ya Damu ili kuhakikisha Damu ya akiba inakuwepo ya kutosha muda wote.

Balozi Seif alisema jukumu la kuwa na Damu ya kutosha katika Benki ya Damu ni la kila Mtu kwa vile tayari limeshaelezwa ndani ya Vitabu vya Dini likifafanua na kuweka wazi kwamba Mtu anayesaidia kuokoa maisha ya mwenzake ni sawa na kusaidia wanaadamu wote.

Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar aliipongeza Jumuiya ya Maendeleo ya Wanawake na Vijana {Bright Initiative Women Organization - BIWO} kwa uamuzi wake wa kuandaa Tamasha hilo licha ya majukumu mengine iliyojipangia ikiwemo kusaidia vita dhidi ya Udhalilishaji, dawa za kulevya, mimba za utotoni pamoja na changamoto nyengine zinazowakumba Vijana.

Alisema Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar itaendelea kuunga mkono jitihada zote zinazochukuliwa na Jumuiya za Kiraia katika kukomesha matumizi ya dawa za kulevya, matendo ya udhalilishaji wa Wanawake na Watoto,likiwemo suala la watoto wadogo kubebeshwa mzigo wa ujauzito.

Balozi Seif alieleza kuwa Jamii inaendelea kushuhudia athari kubwa zinazowakumbwa Vijana wanaotumia Dawa za kulevya, mbali ya athari hizo kuwakumba Vijana lakini pia Jamii nzima imekuwa ikiathirika na matendo hayo mabaya.

Alisema Serikali kwa upande wake imekuwa ikikosa nguvu kazi ya Vijana ambao wanahitajika katika ujenzi wa Taifa, kutokana na udhaifu wanaoupata wa kimwili na kiakili baada ya kujiingiza katika mtego wa matumizi ya dawa hizo.

“ Hatutaki kuona Taifa letu ambalo asilimia kubwa ni Vijana wanakuwa katika hali ya mazezeta wanaoshindwa kuwajibika ipasavyo ”. Alisema Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar.

Hata hivyo Balozi Seif aliwahakikishia Wananchi wote kwamba Serikali Kuu itaendeleza mapambano dhidi ya maovu yote na kuzidi kutoa ushirikiano na Jumuiya za Kiraia katika kupiga vita matendo hayo maovu.

Mapema Mwakilishi wa Mpango wa Damu salama Zanzibar Bwana Abdulla Magarawa alisema zaidi ya chupa 70 hupaswa kutumiwa kila siku katika Hospitali mbali mbali Nchini ili kukidhi mahitaji halisi wagonjwa.

Magarawa alisema Hospitali ya Mnazi Mmoja pekee hutumia chupa 40 ambapo akina mama wanaojifungua hutumia zaidi ya asilimia 75% jambo ambalo uchangiaji bado unahitajika kufanywa na kila Mwananchi.

Alisema katika kuunga mkono jitihada za Serikali za kuhamasisha uchangiaji wa Damu Wizara ya Afya imeshaanzisha utaratibu wa utoaji damu kwa baadhi ya Hospitali na vituo vya Afya Nchini ili kwenda sambamba na Kampeni hiyo ya changia damu salama.

Mwakilishi huyo wa Benki ya Damu salama Zanzibar alielezea faraja yake kutokana na jitihada za Wananchi mbali mbali walioanza kujitokeza kuchangia Damu ambapo kipindi cha saa Moja na Nusu tayari imeshakusanywa Damu Chupa 40 lengo likiwa kupata chupa 1,000.

Akitoa Taarifa ya Jumuiya ya Maendeleo ya Wanawake na Vijana {BIWO} Kaimu Katibu wa Jumuiya hiyo Bibi Raya Hamad alisema Jumuiya hiyo iliyoasisiwa Mwaka 2017 imelenga kuyasaidia makundi hayo mawili katika masuala ya stadi za Kimaisha.

Raya alisema Taasisi hiyo ya Kiraia imeamua kwa makusudi kutekeleza agizo la Rais wa Zanzibar la uchangiaji Damu salama kwa kushirikiana na Ofisi ya Mkoa Mjini Magharibi kupitia Kampeni ya Mimi na wewe chini ya Mpango waDamu salama Zanzibar.
Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar Balozi Seif Al Iddi akiyapokea Matembezi ya Wananchi mbali mbali waliojitokeza katika Kampeni ya kuhamasisha kuchangia Damu salama hapo Viwanja vya Mnara wa Kumbu kumbu ya Mapinduzi Michenzani Mjini Zanzibar.
Balozi Seif akifarajika kuona Kundi kubwa la Wananchi waliojitokeza kwa wingi kuchangia Damu salama katika zoezi maalum lililofanyika katika Viwanja vya Mnara wa Kumbukumbu ya Mapinduzi Michenzani.
Bibi Doto Mohd Hassan { Maarufu Doto Mjanja} alihamasika kuamua kuchangia Damu kufuatia Kampeni Maalum iliyokuwa ikitolewa ndani ya Juma hili.
Bibi Hawa Ibrahim Dau hakua nyuma katika kujitokeza kuchangia Damu akielezea furaha yake akina Mama wanapatia huduma hiyo hasa wakati wa Kujifungua Hospitalini.

Mwandishi Muandamizi wa Idara ya Habari Maelezo na Gazeti la Zanzibar Leo Hassan Vuai akiwa Mwanamme wa Kwanza kujitokeza kutoa Damu salama katika Kampeni ya Changia Damu hapo Mnara wa Kumbukumbu ya Mapinduizi Michenzani.
Kikundi cha Utamaduni cha Mkoa kikitoa burdani kwenye Tamasha la Uchangiaji Damu salama hapo Mnara wa Kumbukumbu ya Mapinduizi Michenzani.
 Balozi Seif akiwapongeza Vijana wa Kizazi Kipya mara baada ya kutoa burdani kwenye Tamasha la Uchangiaji Damu salama hapo Mnara wa Kumbukumbu ya Mapinduizi Michenzani.

Vijana wadogo wa Mchezo wa Karati wakifanya vitu vyao kwenye Tamasha la Uchangiaji Damu salama lililoandaliwa na Jumuiya ya Kuwaendeleza Wanawake na Vijana { BIWO }.
Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar Balozi Seif Ali Iddi akizungumza na kuzindua Tamasha la Uchangiaji Damu salama Michenzani Mjini Zanzibar.

Kulia ya Balozi Seif ni Mkuu wa Mkoa Mjini Magharibi Mheshimiwa Ayoub Mohamed Mahmoud.
Mwakilishi wa Mpango wa Damu Salama Zanzibar Bwana Abdullah Magarawa akitoa taarifa ya hali ya upatikanaji wa Damu salama katika Hospitali za Zanzibar. Picha na – OMPR – ZNZ.                                                         

No comments:

Post a Comment

Post Bottom Ad