HABARI MPYA

Home Top Ad

Post Top Ad

Thursday, December 21, 2017

WAZIRI KALEMANI AAGIZA WOTE WALIOLIPIA UMEME 2017 WAUNGANISHIWE KABLA YA MWISHO WA MWAKA

Na Veronica Simba 
Serikali imeliagiza Shirika la Umeme Tanzania (Tanesco) kuhakikisha wateja wote walioomba na kulipia huduma hiyo mwaka 2017 wanaunganishiwa kabla ya Desemba 30 mwaka huu.
Waziri wa Nishati, Dkt. Medard Kalemani alitoa agizo hilo kwa nyakati tofauti hivi karibuni, akiwa katika ziara ya kazi kukagua utekelezaji wa miradi ya umeme mkoani Singida na Dodoma.
“Agizo hili ni kwa nchi nzima. Hakikisheni wateja waliowasilisha maombi yao na kulipia ndani ya mwaka huu wa 2017 wawe wameunganishiwa umeme siyo zaidi ya Desemba 30 mwaka huu.”
Aidha, Dkt Kalemani aliwaagiza watendaji wa shirika hilo kutoa elimu kwa umma, hasa wananchi walioko vijijini kuhusu umuhimu wa kutumia umeme ili kuwahamasisha kuunganisha nishati hiyo katika makazi yao.
Akifafanua, Waziri alisema kuwa takwimu zinaonesha kuwa baadhi ya wananchi hawajaunganisha umeme katika makazi yao japokuwa tayari Serikali imekwishawafikishia nishati hiyo katika maeneo yao.
“Inawezekana baadhi ya wananchi hawajatambua umuhimu wa kutumia umeme, hivyo ni vema wapatiwe elimu husika. Tuwatembelee mahali waliko, hususan vijijini na tuwapatie elimu hiyo,” alisisitiza.
Akizungumzia faida za umeme, Waziri Kalemani alisema umeme ni kichocheo kikubwa cha maendeleo kwani shughuli nyingi za kiuchumi zinahitaji nishati hiyo.
Aliongeza kuwa, ili dhamira ya Serikali ya Awamu ya Tano ya Uchumi wa Viwanda ifanikiwe, ni lazima kuwepo na umeme wa kutosha na wa uhakika. “Ndiyo maana tumedhamiria kufikisha umeme hadi vijjijini kwa kasi kubwa, hivyo wananchi tafadhali tumieni umeme ili kukuza pato lenu na uchumi wa nchi kwa ujumla.”
Waziri aliwapongeza viongozi wa Serikali wakiwemo Wakuu wa Mikoa, Wakuu wa Wilaya, Wabunge na Watendaji wa Halmashauri na Vijiji, kwa jitihada zao za kufuatilia utekelezaji wa ahadi za serikali kwa wananchi ikiwemo upelekaji wa umeme vijijini.
Aliwataka wananchi kutoa ushirikiano kwa Serikali kwa kutunza miundombinu ya umeme katika maeneo yao ili isihujumiwe na hivyo kuwakosesha huduma hiyo muhimu na pia kuleta hasara kwa serikali.
Ziara hiyo ya Waziri Kalemani ni muendelezo wa ziara mbalimbali ambazo amekuwa akifanya nchi nzima kukagua utekelezaji wa miradi ya umeme na kuzungumza na wananchi wa maeneo husika ikiwa ni pamoja na kupokea kero na changamoto mbalimbali za wananchi kuhusu sekta ya nishati ili zifanyiwe kazi.
Katika ziara hii, Waziri ametembelea Wilaya za Mkalama na Singida  Vijijini mkoani Singida pamoja na Wilaya ya Chamwino mkoani Dodoma. 
 Waziri wa Nishati, Dkt. Medard Kalemani akizungumza na wananchi wa Kijiji cha Ibaga, Wilaya ya Mkalama mkoani Singida, wakati wa ziara yake hivi karibuni kukagua utekelezaji wa miradi ya umeme.
 Mbunge wa Iramba Mashariki, Allan Kiula akizungumza wakati wa ziara ya Waziri wa Nishati, Dkt. Medard Kalemani jimboni kwake hivi karibuni, kukagua utekelezaji wa miradi ya umeme.
 Mbunge wa Mtera, Livingstone Lusinde (kushoto), akizungumza wakati wa ziara ya Waziri wa Nishati, Dkt. Medard Kalemani, jimboni kwake hivi karibuni kukagua utekelezaji wa miradi ya umeme.
 Waziri wa Nishati, Dkt Medard Kalemani, akiwakabidhi baadhi ya wazee kifaa kinachotumika kuunganisha umeme pasipo kutandaza mfumo wa nyaya, kijulikanacho kama Umeme Tayari (UMETA) alipokuwa katika ziara ya kazi Mikoa ya Singida na Dodoma hivi karibuni.
 Afisa Uhusiano wa Shirika la Umeme Tanzania (Tanesco), Innocent Lupenza, akiandika majina ya baadhi ya wazee waliopatiwa zawadi ya kifaa kijulikanacho kama Umeme Tayari (UMETA) na Waziri wa Nishati, Dkt Medard Kalemani (hayupo pichani), alipokuwa katika ziara ya kazi Mikoa ya Singida na Dodoma hivi karibuni.
  Baadhi ya wataalam wa Wizara ya Nishati na Shirika la Umeme Tanzania (Tanesco), wakimsikiliza Waziri wa Nishati, Dkt. Medard Kalemani (hayupo pichani) wakati wa ziara yake katika Kijiji cha Muungano, Wilaya ya Chamwino hivi karibuni, kukagua utekelezaji wa miradi ya umeme.



 Sehemu ya Umati wa wananchi wa vijiji mbalimbali vya Mikoa ya Singida na Dodoma, wakimsikiliza Waziri wa Nishati, Dkt. Medard Kalemani (hayupo pichani) alipokuwa akizungumza nao wakati wa ziara yake hivi karibuni kukagua utekelezaji wa miradi ya umeme.
 Waziri wa Nishati, Dkt. Medard Kalemani (wa pili - kushoto) na Mbunge wa Mtera, Livingstone Lusinde (kushoto) wakimsikiliza Msimamizi wa Mradi wa Ujenzi wa Kiwanda cha Ngozi kilichopo kijiji cha Idifu, Wilaya ya Chamwino, Dkt. Francis Njau (wa tatu – kulia), kuhusu mahitaji ya umeme kwa kiwanda hicho.
Waziri wa Nishati, Dkt. Medard Kalemani, akiwasalimu wananchi wa Kijiji cha Idifu, Wilaya ya Chamwino alipokuwa katika ziara ya kazi kukagua utekelezaji wa miradi ya umeme.

No comments:

Post a Comment

Post Bottom Ad