HABARI MPYA

Home Top Ad

Post Top Ad

Tuesday, December 5, 2017

WANAFUNZI 2,679 WAPATA MIKOPO ELIMU YA JUU KUPITIA RUFAA

Bodi ya Mikopo ya Wanafunzi wa Elimu ya Juu (HESLB) leo (Disemba 5, 2017) imetangaza orodha yenye wanafunzi 2,679 ambao wamepata mikopo ya elimu ya juu yenye thamani ya TZS 9.6 bilioni kufuatia kukamilika kwa uchambuzi wa rufaa zilizowasilishwa na wanafunzi hao.

Kati ya wanafunzi hao, 1,847 ni wa mwaka wa kwanza ambao mikopo yao ina thamani ya TZS 6.84 bilioni na wengine 832 ni wale wanaoendelea na masomo lakini hawakuwa na mikopo katika miaka iliyopita. Wanafunzi hao wanaoendelea na masomo wamepata mikopo yenye thamani ya TZS 2.76 bilioni.
Orodha kamili ya wanafunzi waliofanikiwa kupata mikopo kupitia dirisha la rufaa pamoja na fedha za wanafunzi hao zimetumwa katika vyuo walipo wanafunzi hao hivi sasa.
Hatua hii inafanya jumla ya wanafunzi 33,200 wa mwaka wa kwanza kuwa wamepangiwa mikopo yenye thamani ya zaidi ya TZS 108 bilioni kwa mwaka wa masomo 2017/2018 hadi sasa. Bajeti ya jumla kwa wanafunzi wote kwa mwaka 2017/2018 ni TZS 427.54 bilioni.
Dirisha la rufaa lilifunguliwa kwa siku saba kuanzia tarehe 13 Novemba, 2017 hadi tarehe 19 Novemba, 2017 ili kuwapa fursa waombaji wote ambao hawakuwa wameridhika na upangaji wa mikopo na kuwasilisha rufaa kupitia vyuo walivyopata udahili.
Wanafunzi waliohamishiwa mikopo yao
Wakati huohuo, Bodi ya Mikopo ya Wanafunzi wa Elimu ya Juu imeanza kuhamisha mikopo iliyokuwa imeelekezwa katika vyuo tofauti na waliko kwa sasa. Mikopo ya wanafunzi590 wa mwaka wa kwanza yenye thamani ya TZS 1.78 bilioni ambayo awali ilikuwa imepelekwa katika vyuo tofauti na walipo wanafunzi imehamishwa.
Wanafunzi hao waliohamishiwa mikopo yao ni wale ambao walipangiwa mikopo na kupelekewa fedha zao katika vyuo ambavyo walipata udahili awali, ila baadaye wakaamua kujiunga na vyuo vingine ambavyo nako walipata udahili.
Orodha kamili ya wanafunzi hao pamoja na fedha za wanafunzi hao zimetumwa katika vyuo walipo hivi sasa.
Bodi ya Mikopo inaendelea kupokea orodha za wanafunzi waliosajiliwa katika vyuo mbalimbali na wale wenye mikopo, fedha zao zitahamishiwa katika vyuo walipo katika awamu zijazo.
Mikopo kwa Wahadhiri wa Vyuo Vikuu
Aidha, jumla ya wanafunzi 45 wa shahada za uzamili na uzamivu ambao ni wanataaluma na waajiriwa wa vyuo mbalimbali nchini wamepata mikopo yenye thamani ya TZS 441.4 milioni katika mwaka wa masomo 2017/2018.
Mikopo hii hutolewa na Bodi ya Mikopo kwa wanataaluma hao ili kuvijengea vyuo uwezo wa kitaaluma chini ya makubaliano kati ya Bodi ya Mikopo na vyuo hivyo.
Imetolewa na:

Abdul-Razaq Badru
MKURUGENZI MTENDAJI
BODI YA MIKOPO YA WANAFUNZI WA ELIMU YA JUU
Jumanne, Disemba 5, 2017

No comments:

Post a Comment

Post Bottom Ad