HABARI MPYA

Home Top Ad

Post Top Ad

Sunday, December 17, 2017

WAKAGUZI WA MIGODI KUPUNGUZA AJALI MIGODINI

Wakaguzi wa Migodi Nchini wameagizwa kutembelea mara kwa mara kwenye migodi hususan ya wachimbaji wadogo kwa ajili ya kukagua hali ya usalama na kuwasaidia Wachimbaji kuepusha ajali wakati wa utekelezaji wa shughuli zao.

Agizo hilo limetolewa Desemba 14, 2017 Mkoani Tabora na Naibu Waziri wa Madini, Stanslaus Nyongo alipotembelea kwenye Mgodi wa Dhahabu wa Nsungwa Gold Mine uliopo katika Kata ya Silambo Wilaya ya Kaliua ili kujionea shughuli zinazofanywa mgodini hapo na kuzungumza na wachimbaji.

Baadhi ya Wachimbaji walimueleza Naibu Waziri Nyongo kuwa wamekuwa wakifanya shughuli zao katika mazingira magumu bila kuwa na elimu ya namna bora ya uchimbaji wa madini.

Nyongo alisema ni jukumu la Maafisa Madini wakiwemo Wakaguzi wa Migodi (Mining Inspectors) kuhakikisha wachimbaji hususan wadogo wanapatiwa elimu ya mara kwa mara kuhusu afya, uchimbaji salama na uhifadhi wa mazingira ili kuepusha magonjwa na ajali zinazosababishwa na uelewa finyu wa uchimbaji bora.

“Wachimbaji wadogo wanapaswa kutembelewa na kuelimishwa mara kwa mara na hili ni jukumu lenu, msisubiri hadi kutokee madhara ndio mfike kutoa elimu,” alisema.

Aidha, Nyongo aliagiza wamiliki wa machimbo kuhakikisha wanawapatia vitendea kazi wachimbaji kwenye maeneo yao ili kuwalinda na madhara yanayoweza kujitokeza wakati wa utekelezaji wa shughuli zao.

Alisema suala la kuwapatia vitendea kazi wachimbaji litasaidia kuepukana na ajali na wakati huohuo kuchangia kuongezeka kwa mapato yatokanayo na shughuli hiyo ya uchimbaji madini.

“Inabidi muelewe, mnapowapatia vifaa hawa wachimbaji wenu mtaepukana na ajali kwahiyo muda mwingi mtatumia kwenye kuzalisha na hivyo uzalishaji utaongezeka sambamba na mapato yenu,” alifafanua Naibu Waziri Nyongo.

Vilevile Nyongo alisisitiza umuhimu wa wachimbaji hao kujiunga katika vikundi ili kuwa na urahisi wa kusaidiwa kuwa na uchimbaji wenye tija kwao na taifa kwa ujumla.

"Mkijiunga kwenye vikundi itakua ni rahisi kuwafikia kwa pamoja na kuwapatia misaada mbalimbali yenye tija kwenye shughuli zenu," alisema.

Aliongeza kwamba dhamira ya Serikali ni kuhakikisha  Wachimbaji Wadogo wa Madini wanafanikiwa kufikia kwenye uchimbaji wa Kati na baadaye kuwa Wachimbaji Wakubwa.

 Naibu Waziri wa Madini, Stanslaus Nyongo akizungumza kwenye mkutano na Wananchi na Wachimbaji Wadogo kutoka Kata ya Silambo Wilayani Kaliua (hawapo pichani).
 Naibu Waziri wa Madini, Stanslaus Nyongo (wa sita kushoto waliosimama mbele) akiwa katika picha ya pamoja na viongozi wa Wilaya ya Kaliua, Maafisa kutoka Ofisi ya Madini, Tabora na viongozi wa Mgodi wa Dhahabu wa Nsungwa Gold Mine uliopo katika Kata ya Silambo Wilaya ya Kaliua.
 Naibu Waziri wa Madini, Stanslaus Nyongo (katikati) akielekea kwenye machimbo ya dhahabu yaliyopo katika Kata ya Silambo Wilayani Kaliua.
 Naibu Waziri wa Madini, Stanslaus Nyongo (wa tatu kutoka kulia) akitazama moja ya shimo la dhahabu lililoko katika Mgodi wa Nsungwa Gold Mine uliopo katika Kata ya Silambo Wilayani Kaliua.
 Naibu Waziri wa Madini, Stanslaus Nyongo (mbele) akielekea kwenye machimbo ya dhahabu yaliyopo katika Kata ya Silambo Wilayani Kaliua.
Naibu Waziri wa Madini, Stanslaus Nyongo (mbele) akiongoza ujumbe wake kukagua shughuli za uchimbaji wa dhahabu kwenye mgodi wa dhahabu wa Nsungwa Gold Mine uliopo katika Kata ya Silambo Wilayani Kaliua.

No comments:

Post a Comment

Post Bottom Ad