HABARI MPYA

Home Top AdPost Top Ad

Saturday, 2 December 2017

SAVE THE CHILDREN YATOA MSAADA WA GARI,PIKIPIKI KUENDELEZA MAPAMBANO DHIDI YA UKATILI WA WATOTO SHINYANGA


Shirika la Kimataifa la Save The Children limetoa msaada wa gari aina ya Toyota Landcruiser katika Halmashauri ya Mji Kahama mkoa wa Shinyanga kwa ajili ya kusaidia ufuatiliaji wa matukio ya ukatili na unyanyasaji wa watoto. Mbali na kukabidhi gari hilo, Save The Children pia imekabidhi pikipiki mbili aina ya Boxer, Kompyuta mpakato moja (Laptop) na Ipad moja kwa shirika la KIWOHEDE linalotekeleza mradi wa kupambana na mila na desturi kandamizi kwa watoto katika halmashauri ya Ushetu wilayani Kahama. 


Hafla fupi ya makabidhiano hayo imefanyika leo Ijumaa,Desemba Mosi,2017 katika viwanja vya Halmashauri ya Kahama Mji wilayani Kahama,mkoani Shinyanga. 

Akizungumza wakati wa kukabidhi,gari,pikipiki,laptop na Ipad, Meneja wa Shirika la Save The Children mkoa wa Shinyanga,Benety Malima alisema vifaa hivyo vitasaidia katika utendaji kazi kupambana na ukatili dhidi ya watoto. 
“Leo ni siku ya Ukimwi duniani na sisi tumeona tushiriki katika siku hii ili kuonesha kwamba ukatili ni njia mojawapo ya maambukizi ya Virusi vya Ukimwi, Mradi wetu umeisha lakini mapambano dhidi ya ukatili kwa watoto yanaendelea, kwa hiyo tunakabidhi gari hili ili mapambano yaendelee”,alisema Malima. 
“Vifaa hivi likiwemo gari hili vitakwenda kufanya kazi za mapambano dhidi ya ukatili wa watoto,tunaomba likafanye kazi kama ilivyokusudiwa ili kuhakikisha kuwa vitendo vya ukatili dhidi ya watoto vinaisha mkoani Shinyanga”,aliongeza Malima. 
Aidha alisema tangu mwaka 2014 walikuwa wanatekeleza mradi wa Ukatili dhidi ya watotokatika halmashauri ya Mji Kahama,Manispaa ya Shinyanga na Shinyanga Vijijini na baada ya mradi kuisha mwaka huu wametoa gari hilo kwa halmashauri ya Kahama Mji kwani imekuwa mstari wa mbele katika mapambano ya ukatili dhidi ya watoto. 
“Tunawapongeza sana halmashauri ya Kahama Mji kwa kuwa mfano mzuri katika vita dhidi ya ukatili wa kijinsia na watoto,wameonesha hatua za ziada,waliamua kuubeba mradi huu na kuufanya wao,tunaamini wataendeleza mapambano”,alisema Malima. 
Hata hivyo,Kaimu Mkurugenzi wa halmashauri ya Kahama Mji,Robert Kwela aliuhakikishia uongozi wa shirika hilo kuwa watalitunza na kulitumia gari hilo kwa malengo yaliyokusudiwa. 
“Mradi wa wenzetu Save the Chidren kuisha muda wake, wamekabidhi vifaa hivi ili shughuli za mapambano ya ukatili dhidi ya watoto ziendelee”,alisema. 
“Baada ya mradi kuisha,ili shughuli zilizokuwa zinatekelezwa ziweze kuendelea,utaratibu huwa ni lazima mashirika husika yaendelee kuona namna ya kujenga uwezo kwenye taasisi ambazo walikuwa wanafanya nazo kazi ili shughuli zilizokuwa zimeanzishwa ziweze kuendelezwa”,alifafanua Kwela. 
Kwa upande wake,Mwenyekiti wa halmashauri ya Kahama Mji,Abel Shija alilishukuru shirika hilo kwa ushirikiano ambao limekuwa likiwapa na kuongeza kuwa suala la ukatili dhidi ya watoto linapaswa kufanywa kwa vitendo kama vile Save the Children walivyoonesha kwa kutoa vifaa hivyo vya kutendea kazi. 
Naye Mratibu wa Mradi wa kupambana na mila na desturi kandamizi kwa watoto Shirika la KIWOHEDE, Lulu Makwale alilishukuru shirika la Save the Children kwa kuwapatia msaada wa pikipiki mbili,laptop na Ipad vifaa ambavyo vitasaidia katika utekelezaji wa mradi huo katika Halmashauri ya Ushetu.
Makabidhiano hayo pia yalishuhudiwa na Katibu tawala mkoa wa Shinyanga,Albert Msovela alilishukuru shirika hilo kwa msaada wa gari na kuongeza kuwa litasaidia katika kupunguza changamoto ya usafiri katika halmashauri hiyo.
Meneja wa Shirika la Save The Children mkoa wa Shinyanga,Benety Malima akizungumza wakati akikabidhi gari katika halmashauri ya Kahama Mji na pikipiki,laptop na Ipad kwa shirika la KIWOHEDE leo katika viwanja vya Kahama Mji,wilayani Kahama.Wa kwanza kushoto ni Mwenyekiti wa halmashauri ya Kahama Mji,Abel Shija. Kulia ni Mratibu wa ulinzi wa mtoto,haki za watoto na utawala shirika la Save The Children,Alex Enock akifuatiwa na Kaimu Mkurugenzi wa halmashauri ya Kahama Mji,Robert Kwela.
Gari na pikipiki zilizotolewa na shirika la Save The Chilren vikiwa nje ya ofisi za halmashauri ya Kahama Mji.
Meneja wa Shirika la Save The Children mkoa wa Shinyanga, Benety Malima (kulia) akimkabidhi funguo za gari Mwenyekiti wa halmashauri ya Kahama Mji,Abel Shija. 
Katikati ni Mwenyekiti wa halmashauri ya Kahama Mji,Abel Shija akionesha funguo za gari lililotolewa na shirika la Save the Children kwa ajili ya kuendeleza mapambano dhidi ya ukatili wa watoto.

No comments:

Post a Comment

Post Bottom Ad