HABARI MPYA

Home Top Ad

Post Top Ad

Thursday, December 14, 2017

MSHAURI WA ELIMU BEATRICE :WALIMU WENYE UWEZO WANATAKIWA KUFUNDISHA WANAFUNZI WA DARASA LA AWALI

Na Said Mwishehe
MSHAURI wa elimu nchini kutoka Shirika la Maendeleo la Canada, Beatrice Omari amesema walimu wenye uwezo mkubwa kufundisha na walio na hekima, busara na uvumilivu ndio wenye kustahili kufindisha wanafunzi wa elimu ya awali,darasa la kwanza na pili.

 Akizungumza Dar es Saalam leo baada ya kutolewa matokeo ya utafiti wa Kiufunza awamu ya pili wa motisha kwa walimu uliofanyika katika kipindi cha mwaka 2015/2016 katika shule120 nchini.

 Amesema kwa maoni yake na uzoefu alionao kwenye elimu ,ni vema walimu wenye uwezo mkubwa wa kufundisha ndio wawe wanafundishi wanafunzi wa elimu ya awali,darasa la kwanza,pili na tatu kwani ndio ujenzi wa msingi bora wa elimu.

 Ametoa majibu hayo baada ya kuulizwa kwanini miaka ya zamani waliokuwa wanafundisha darasa la kwanza na pili walikuwa wenye umri mkubwa ambapo alisisitiza ilitokana na uzoefu wao wa kufundisha na kuwavumikia wanafunzi ambao ndio wameanza kujengwa kielimu.

 "Elimu ya awali, darasa la kwanza na pili inahitaji walimu wenye uwezo mkubwa wa kufundisha maana ndipo ambapo mwanafunzi anaandaliwa kielimu,ndio eneo ambalo mwaamnafunzi anafundishwa kuandika maumbo ya herufi.

 " Wanapoandaliwa na walimu wazuri mwanzoni,walimu wa madarasa ya mbele jukumu lao inakuwa ni kuwajaza maarifa ya kielimu.Wasipoandaliwa vema matokeo take ndio wanapatikana wanafunzi wanaohitimu darasa la saba lakini hawajui kusoma na kuandika,"amesema.

 Kuhusu motisha amesema Serikali inafanya jitihada kubwa kuboresha maslahi ya walimu nchini lakini no vema kukawa na mfumo rasmi ambao utasaidia kujenga mazingira bora ya walimu.

 Pia badala ya motishi,jamii inatakiwa kutambua thamani ya mwalimu ambaye ndio anayepika wataalamu wa fani mbalimbali. Amesema zamani nyumba nzuri kijijini ilikuwa ni ya mwalimu na walikuwa kimbilio la wananchi kwani walitambua thamani yao lakini sasa jamii imeshindwa kutambua umuhimu wa mwalimu.

 Awali Mkurugenzi Mtendaji waTaasisi ya Twaweza Aidan Eyakuze amesema Serikali inapoteza inapoteza sh.  bilioni 793 kila  mwaka kwa kulipa mishahara walimu wasiofundisha au kutofika shule kwa shule msingi nchini.

 Eyakuze amesema si watoto tu hawajifunzi lakini hata kodi zetu zinalipia huduma ambayo haipatikani na utafi  huo umedhihirisha kuwa kuwalipa walimu fedha baada ya matokeo ya kujifunza kunaweza kuboresha matokeo ya kujifunza.

 "Kwa mujibu wa utafiti huo mwaka 2015 asilimia 31 ya walimu hawakuwepo shuleni kabisa ambapo asilimia 34 walimu hao walikuwepo lakini hakuwepo darasani akifanya shughuli zake zingine na asilimia 35 ilionesha wapo darasani.

 "Kwa mwaka 2016 takwimu zilishuka ambapo asilimia 27 ya walimu hawakuwepo shuleni kabisa, asilimia 32 yupo shuleni lakini hayupo darasani na asilimia 41 wapo darasani, "amesema.

 Amesema utafiti huo umeonesha matokeo mazuri kwa kumpa mwalimu motisha kunampa ari mwalimu kufundisha mwanafunzi na kufaulu zaidi. 

 "Kasi ya mtoto kujifunza inaongezeka katika kipindi kifupi unavyomuongezea mwalimu motisha, "amesema.

Pia amefafanua asilimia 91 ya walimu katika utafiti huo wameupenda mpango huo na asilimia 63 ya walimu waliafiki serikali iweke mfumo rasmi wa motisha kwa walimu kutokana na matokeo mazuri. Utafiti huo umefanywa na taasisi ya Twaweza kwa kushirikiana na Tume ya Sayansi na teknolojia (COSTECH)  pamoja na Shirika la Innovations for Poverty Action (IPA).

Ambapo takribani sh 266,315 zilitumika kulipa walimu 788 motisha kati ya 900 huku wastani wa sh milioni 3.6 kikiwa ni kiwango kikubwa kwa mwalimu kupata. Wadau waliokuwepo kwenye matokeo ya utafiti huo wameipongeza Serikali kwa juhudi zinazofanywa katika kuboresha sekta ya elimu nchini.

Mshauri  wa elimu nchini kutoka Shirika la Maendeleo la Canada, Beatrice Omari akizungumza na waandishi wa habari juu ya mfumo wa elimu katika mkutano wa Twaweza leo jijini Dar es Salaam.

No comments:

Post a Comment

Post Bottom Ad