HABARI MPYA

Home Top Ad

Post Top Ad

Saturday, December 9, 2017

MSAMAHA WA RAIS KWA WAFUNGWA KATIKA KUADHIMISHA MIAKA 56 YA UHURU WA TANZANIA BARA, TAREHE 9 DISEMBA, 2017

Katika kuadhimisha Miaka 56 ya Uhuru wa Tanzania Bara tarehe      9 Disemba, 2017 Mheshimiwa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kwa kutumia madaraka aliyopewa chini ya Ibara ya 45(1)(d) ya Katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania ametoa msamaha kwa wafungwa wafuatao:-

(i)           Wafungwa wote wapunguziwe moja ya sita (1/6) ya vifungo vyao zaidi ya punguzo la kawaida la moja ya tatu (1/3) linalotolewa chini ya Kifungu 49(1) cha Sheria ya Magereza Sura ya 58, isipokuwa wafungwa walioorodheshwa katika Ibara ya 2(i – xxi).

(ii)         Wafungwa wagonjwa wenye magonjwa kama UKIMWI, Kifua kikuu (TB) na Saratani (Cancer) ambao wako kwenye “terminal stage”. Wafungwa hawa wathibitishwe na Jopo la Waganga chini ya Uenyekiti wa Mganga Mkuu wa Mkoa/Mganga Mkuu wa Wilaya.

(iii)       Wafungwa wazee wenye umri wa miaka sabini (70) au zaidi.  Umri huo uthibitishwe na Jopo la Waganga chini ya Uenyekiti wa Mganga Mkuu wa Mkoa/Mganga Mkuu wa Wilaya.

(iv)        Wafungwa wa kike walioingia na mimba gerezani, pamoja na wale walioingia na watoto wanaonyonya na wasionyonya.

(v)          Wafungwa wenye ulemavu wa mwili na akili (Physical disability and mental disability). Ulemavu huo uthibitishwe na Jopo la Waganga chini ya Uenyekiti wa Mganga Mkuu wa Mkoa/Mganga Mkuu wa Wilaya.

2.      Aidha, Msamaha wa Mheshimiwa Rais hautawahusu wafungwa wafuatao:-

(i)                Wafungwa waliohukumiwa adhabu ya kunyongwa au kwa makosa ya kujaribu kuua (attempt to murder).

(ii)              Wafungwa waliohukumiwa adhabu ya kunyongwa na adhabu hiyo kubadilishwa kuwa kifungo cha maisha au kifungo gerezani.

(iii)            Wafungwa waliohukumiwa kifungo cha maisha gerezani.

(iv)             Wafungwa wanaotumikia kifungo kwa makosa ya kujihusisha na usafirishaji na matumizi ya madawa ya kulevya kama vile cocaine, heroin, bhangi n.k.

(v)               Wafungwa wanaotumikia kifungo kwa makosa ya kujihusisha na uombaji na upokeaji au utoaji rushwa.

(vi)             Wafungwa wanaotumikia kifungo kwa makosa ya unyang’anyi na unyang’anyi wa kutumia silaha au kujaribu kutenda makosa hayo (robbery with violence, armed robbery and attempted robbery).

(vii)           Wafungwa wanaotumikia kifungo kwa makosa ya kupatikana na silaha, risasi au milipuko isivyo halali (fire arms, ammunitions and explosives).

(viii)         Wafungwa wanaotumikia kifungo kwa makosa ya shambulio la aibu, kunajisi, kubaka na kulawiti, ukatili kwa watoto au kujaribu kutenda makosa hayo.

(ix)            Wafungwa waliopatikana na hatia na kuhukumiwa kifungo kwa kosa la kuwapa mimba wanafunzi wa Shule za Msingi na Shule za Sekondari na ambao walitenda kosa hilo wakiwa na umri wa miaka kumi na nane (18) na kuendelea.

(x)              Wafungwa wanaotumikia kifungo kwa makosa ya wizi wa magari na pikipiki, uharibifu wa miundombinu au kujaribu kutenda makosa hayo.

(xi)            Wafungwa wanaotumikia kifungo chini ya Sheria ya Bodi ya Parole (Act. No. 25/1994) na Sheria ya Huduma kwa Jamii (Act. No. 6/2002).

(xii)          Wafungwa waliopatikana na hatia na kuhukumiwa kifungo kwa makosa ya kutumia vibaya madaraka yao na kuhujumu uchumi.

(xiii)        Wafungwa waliowahi kupunguziwa kifungo na Msamaha wa Mhe. Rais na bado wangali wanaendelea kutumikia sehemu ya kifungo kilichobaki.

(xiv)         Wafungwa waliopatikana na hatia na kuhukumiwa kwa kosa la kuzuia watoto kupata masomo.

(xv)           Wafungwa waliopatikana na hatia na kuhukumiwa kwa kosa la utekaji wa watoto, kupoka na kufanya biashara ya binadamu (Human Trafficking).

(xvi)         Wafungwa waliopatikana na hatia na kuhukumiwa kwa kosa la kukutwa na viungo vya binadamu.

(xvii)       Wafungwa wanaotumikia vifungo kwa makosa ya kujihusisha kwa namna yoyote ile na nyara za Serikali na ujangili (poachers).

(xviii)     Wafungwa wanaotumikia vifungo kwa makosa ya wizi/ubadhirifu wa fedha za Serikali.

(xix)         Wafungwa wanaotumikia vifungo kwa makosa ya kutoroka au kujaribu kutoroka chini ya ulinzi halali.

(xx)           Wafungwa walioingia gerezani baada ya tarehe 30/10/2017.

(xxi)         Wafungwa waliowahi kufungwa gerezani.

3.      Wafungwa 8,157 watafaidika na msamaha huu ambapo 1,828 wataachiliwa huru tarehe 9 Disemba, 2017 na 6,329 watabaki gerezani kumalizia sehemu ya kifungo kilichobaki baada ya kupewa msamaha huu. Ni mategemeo ya Serikali kwamba watarejea tena katika jamii kushirikiana na wenzao katika ujenzi wa Taifa na kwamba watajiepusha kutenda makosa ili wasirejee tena gerezani.
Aidha Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt. John Pombe Magufuli kwa mujibu wa  Ibara ya  45(1) (d) ya  Katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania inampa  Mamlaka  Rais wa Jamhuri ya Muungano    wa Tanzania  kufuta adhabu yote au sehemu ya adhabu yoyote aliyopewa mtu yeyote kwa ajili ya kosa lolote au kufuta adhabu yote. 
Kwa kutumia Mamlaka aliyo nayo amewasamehe wafungwa  wengine 63  kati yao wafungwa 61 ni wale waliokuwa wamehukumiwa kunyongwa, waliokuwa na  umri mkubwa  na waliokaa gerezani muda mrefu. Na pia amewasamehe wafungwa wengine wawili waliokuwa wakitumikia kifungo cha maisha ambao ni  Nguza Viking(BABU SEA) na Johnson Nguza. Hivyo kwa ujumla amewasamehe wafungwa 8220.


imetolewa na

Meja Jenerali Projest Rwegasira (Mstaafu)
KATIBU MKUU
WIZARA YA MAMBO YA NDANI YA NCHI
09/12/2017

No comments:

Post a Comment

Post Bottom Ad