HABARI MPYA

Home Top Ad

Post Top Ad

Wednesday, December 27, 2017

MAKATIBU WAKUU WAJADILI UTEKELEZAJI MRADI WA UMEME WA STIEGLER’S GORGE

Na Veronica Simba 
Makatibu Wakuu wa Wizara mbalimbali, hivi karibuni walifanya kikao kujadili hatua iliyofikiwa katika utekelezaji wa Mradi wa kufua umeme kutoka katika maporomoko ya maji ya Mto Rufiji katika eneo la Stiegler’s Gorge.
Kikao hicho kilichoongozwa na Katibu Mkuu wa Wizara ya Nishati, Dkt. Hamisi Mwinyimvua, kilifanyika Makao Makuu ya Wizara mjini Dodoma.
Aidha, kikao hicho pia kilijadili majukumu ya kila Wizara husika katika kufanikisha utekelezaji wa Mradi huo.
Akifungua kikao hicho, Dkt. Mwinyimvua alieleza kuwa mahitaji ya umeme nchini kwa sasa ni makubwa kutokana na kutekeleza sera ya uchumi wa viwanda hali inayosababisha huduma ya umeme wa uhakika kuhitajika zaidi ya muda mwingine wowote.
“Serikali ya Awamu ya Tano inaelekeza nchi kuingia kwenye uchumi wa kati ifikapo Mwaka 2025. Ili kufikia malengo hayo, hatua za makusudi za kuongeza uzalishaji wa umeme kwa ajili ya viwanda zinahitajika.”
Kamishna wa Nishati na Masuala ya Petroli, Mhandisi Innocent Luoga, akielezea umuhimu wa Mradi huo kwa Taifa alisema kuwa umeme wa uhakika unahitajika ili pamoja na mambo mengine kukidhi mahitaji ya mkakati wa kusambaza umeme vijijini ambao unaendelea nchini kote.
Awali, akiwasilisha taarifa fupi kuhusu Mradi husika katika kikao hicho, Msimamizi wake, Mhandisi Leonard Masanja alieleza kuwa, Desemba 19 mwaka huu, Wizara ya Nishati ilitangaza zabuni ya kumpata Mkandarasi wa Ujenzi wa Mradi huo ambao utekelezaji wake unakadiriwa kuanza mwishoni mwa mwezi Februari 2018.
Alisema kuwa, mwishoni mwa mwezi Juni mwaka huu, Rais John Magufuli aliamua kuanza utekelezaji wa ujenzi wa Mradi huo ambao ulibuniwa na Baba wa Taifa Mwalimu Julius Nyerere miaka ya 1970.
Mhandisi Masanja aliongeza kuwa, timu ya wataalam kutoka Wizara ya Nishati, Shirika la Umeme Tanzania (Tanesco) na Wakala wa Barabara Tanzania (Tanroads), iliundwa ili kufanya maandalizi ya Mradi na baadaye kusimamia ujenzi mara baada ya Mkandarasi kupatikana. “Timu hiyo iliungana na timu ya wataalam kutoka Ethiopia katika utekelezaji wa jukumu hilo.”
Makatibu Wakuu walioshiriki au kuwakilishwa katika kikao hicho ni kutoka Ofisi ya Makamu wa Rais, Ofisi ya Waziri Mkuu, Wizara ya Fedha na Mipango, Wizara ya Ulinzi na Jeshi la Kujenga Taifa pamoja na Wizara ya Mambo ya Ndani ya Nchi.
Wengine ni kutoka Wizara ya Maji na Umwagiliaji, Wizara ya Kilimo, Wizara ya Mifugo na Uvuvi, Wizara ya Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano pamoja na Wizara ya Maliasili na Utalii.
 Katibu Mkuu wa Wizara ya Nishati, Dkt. Hamisi Mwinyimvua akiongoza kikao cha Makatibu Wakuu wa Wizara mbalimbali (hawapo pichani) kujadili Mradi wa Umeme wa Stiegler’s Gorge, hivi karibuni mjini Dodoma.
 Msimamizi wa Mradi wa Umeme wa Stiegler’s Gorge, Mhandisi Leonard Masanja, akiwasilisha taarifa fupi kuhusu Mradi huo, wakati wa kikao cha Makatibu Wakuu wa Wizara mbalimbali (hawapo pichani), kilichofanyika hivi karibuni mjini Dodoma.
 Ramani ya Mradi wa kufua umeme kutoka katika maporomoko ya maji ya Mto Rufiji katika eneo la Stiegler’s Gorge, utakavyoonekana baada ya kukamilika.
 Wajumbe wa kikao cha Makatibu Wakuu wa Wizara mbalimbali, wakijadili utekelezaji wa Mradi wa Umeme wa Stiegler’s Gorge, hivi karibuni mjini Dodoma.

No comments:

Post a Comment

Post Bottom Ad