HABARI MPYA

Home Top Ad

Post Top Ad

Friday, 22 December 2017

BALOZI SEIF ATAKA UWEKEZAJI KWENYE UCHAPISHAJI WA VITABU VYA KISWAHILI

 Mwenyekiti wa Baraza la Kiswahili Zanzibar (BAKIZA) Dr. Mohamed Seif  Khatib  aliyevaa shati rangi Nyekundu akimkaribisha Makamu wa pili wa Rais Zanzibar, Balozi Seif Ali Iddi kufunga Kongamano ya kwanza la Kimataifa la Kiswahili. Kati kati yao ni Naibu Waziri wa Elimu na Mafunzo ya Amali Zanzibar Mh. Mmanga Mjengo Mjawiri.
Makamu wa pili wa Rais Zanzibar, Balozi Seif Ali Iddi (kushoto) akiongozwa na Viongozi wa Baraza la Kiswahili kuingia katika Ukumbi wa zamani wa Baraza la Wawakilishi Kikwajuni Mjini Zanzibar kulifunga Kongamano la kwanza la Kimataifa la Kiswahili.
 Baadhi ya Wataalamu na wadau wa Kiswahili walioshiriki Kongamano ya kwanza la Kimataifa la Kiswahili lililofanyika  Siku Mbili Visiwani Zanzibar.
 Makamu wa pili wa Rais Zanzibar, Balozi Seif Ali Iddi akitoa vyeti kwa Mmoja wa Washiriki wa Kongamano la kwanza la Kimataifa la Kiswahili lililofanyika Zanzibar kwa Siku mbili.
Makamu wa pili wa Rais Zanzibar, Balozi Seif Ali Iddi kushoto akiwa pamoja na Mwenyekiti wa Bakiza Dr. Mohamed Seif wakiangalia baadhi ya vitabu vya Kiswahili vilivyotungwa na Magwiji wa Lugha ya Kiswahili na kusomeshwa katika skuli na vyuo mbali mbali ndani na nje ya Nchi.
Makamu wa pili wa Rais Zanzibar, Balozi Seif Ali Iddi na Dr. Khatib wakifurahia moja ya Kitabu  mashuhuri cha Mtungaji Gwiji Zanzibar Bwana Mohamed Said  (Maarufu Bwana Msa).
Picha na – OMPR – ZNZ.

Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar Balozi Seif Ali Iddi alisema wakati umefika kwa Wafanyabiashara wakubwa Nchini kuwekeza katika uchapishaji wa Vitabu vya Kiswahili pamoja na kujenga Maduka makubwa ya kuuzia kazi za Kiswahili kwa vile bidhaa zinazotokana na lugha hiyo zinauzika.

Alisema Mwanataaluma au mswahili anayehitaji vitabu vya Waandishi Mahiri wa Lugha hiyo wa Zanzibar kama Profesa Said Ahmed Mohamed, Shafi Adam Shafi, Bwana Msa na wasanii wengine kama Mohamed Seif Khatibu kamwe kwa wakati huu anashindwa kuvipata.

Balozi Seif Ali Iddi alisema hayo wakati alipokuwa akilifunga Kongamano la Kimataifa la Siku mbili la Lugha ya Kiswahili lililokuwa likifanyika katika Ukumbi wa zamani wa Baraza la Wawakilishi Zanzibar uliopo Mtaa wa Kikwajuni Mjini Zanzibar.

Alisema ni faraja iliyoje kwa sasa kuona kiasi gani Lugha ya Kiswahili inavyoendelea kupata heshima ya kutambuliwa na kukubaliwa Kimataifa hasa kutokana na upatikanaji wa mwitiko mkubwa wa kuwa na Wataalamu waliobobea katika nyanja mbali mbali.

Balozi Seif aliwataka Wafanyabiashara, Wataalamu pamoja na watumiaji wa Lugha ya Kiswahili ndani na nje ya Nchi kushirikana kwa pamoja katika kuhakikisha Lugha hiyo inatumika ipasavyo na hasa ikitambulika wazi kwamba hakuna mtu anayeelewa kila kitu.

“ Hakuna Mtaalamu anayejuwa kila kitu. Utamkuta Mtaalamu wa Fasihi Sarufi inampiga chenga au Mtaalamu wa muundo wa L ugha Sarufi inamuendesha kindumbwe ndumbwe ”. Alisema Balozi Seif.

Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar aliwapongeza waandaaji wa Kongamano hilo la Kimataifa la Kiswahili ambalo limewaweka pamoja Wataalamu wa Kiswahili kutoka Tanzania Bara, Ulaya Marekani baadhi ya Nchini za Bara la Afrika na wenyeji Zanzibar.

Alisema ni kawaida katika mijadala kama hiyo ya Kitaaluma washiriki huchangia kwa kuhoji,kuboresha au kutokubaliana na baadhi ya vipengele vya Hoja mambo ambayo yanapaswa kuigwa na kuzingatiwa na wadau wengine kwani huzidi kukipa uhai zaidi Kiswahili Kitaaluma.

Alieleza kwamba Kongamano hilo la Kiswahili limetoa fursa ya mkusanyiko wa Wataalamu wa Taaluma ya nyanja mbali mbali, kukutana na kubadilishana uzoefu, ujuzi na changamoto wanazokumbana nazo wakiwa kwenye harakati za kukiendeleza Kiswahili.

Balozi Seif alifahamisha kwamba mkusanyiko huo sio tu utaimarisha na kukuza Lugha ya Kiswahili, bali pia utajenga wigo mpana zaidi kwa wanataalamu wa Lugha hiyo Dunia nzima kusaidiana katika kukieneza Kiswahili.

Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar aliwasisitiza wana kongamano hao wa Lugha ya Kiswahili kuwa hivi sasa ni wakati muwafaka wa kufikiria uandaaji wa Maonyesho ya Kimataifa ya Vitabu vya Kiswahili hasa katika Ukanda wa Afrika Mashariki.

Alisema maonyesho hayo ambayo ingependeza yakafanyika kila baada ya Miaka miwili au zaidi yatasaidia kuongeza kasi ya uchapishaji na pengine usomaji wa kazi mbali mbali zinazotokana na Lugha ya Kiswahili.

Mapema Mwenyekiti wa Baraza la Kiswahili Zanzibar { BAKIZA} Dr. Mohamed Seif Khatib ameipongeza na kuishukuru Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar kwa kuthamini Lugha ya Kiswahili inayopelekea kutumika katika Taasisi zake za Umma na Jamii.

Dr. Khatib alisema kitendo hicho kinaendelea kuleta faraja kwa Wana Baraza la Kiswahili Zanzibar na kusisitiza kwamba lazima Lugha hiyo iimarishwe ili iweze kurahisisha Maisha ya Mswahili.

Alifahamisha kwamba Mswahili tokea anazaliwa, anakua na kusoma, anaingia katika harakati za Kimaisha, anafariki kwa kumaliza muda wake wa kuishi anaombewa Dua kwa Lugha ya Kiswahili.

Akimkaribisha Mgeni Rasmi kulifunga Kongamano hilo la kwanza la Kimataifa la Kiswahili Waziri wa Habari, Utamaduni, Utalii na Michezo Mheshimiwa Rashid Ali Juma aliupongeza Uongozi wa Baraza la Kiswahili Zanzibar kwa juhudi kubwa zilizopelekea kufanyika kwa Kongamano hilo Visiwani Zanzibar.

Mh. Rashid alisema Wizara ya Habari, Utamaduni, Utalii na Mic hezo itakuwa chachu ya kusimamia yale yote yaliyokusanywa katika Kongamano hilo ili yasaidie kunufaisha Kizazi cha sasa na kijacho.

Waziri wa Habari alisema wakati Zanzibar ikiendelea kuimarisha miundombinu ya Sekta ya Utalii Kiswahili ni moja ya kivutio kinachoshawishi wageni wengi kupendelea kutembelea Zanzibar kujifunza Utamaduni wa Visiwa hivi kupitia lugha ya Kiswahili.
Alisema Mataifa mengi Duniani hivi sasa yameshaelewa umuhimu na thamani ya Lugha ya Kiswahili kwa kufundisha Wananchi wao. Hivyo kitendo hicho ni vyema kikatiliwa mkazo katika kuona walimu wa kutosha wa kusomesha lugha hiyo hasa kwa wageni wanapatikana katika dhana nzima wa kuilinda lugha hiyo isipotoshwe.

No comments:

Post a comment

Post Bottom Ad