HABARI MPYA

Home Top Ad

Post Top Ad

Friday, December 8, 2017

Aliyedaiwa kuuibia DCB bank aachiwa huru

Na Karama Kenyunko, Blogu ya Jamii.

Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu imemuachia huru mfanyabiashara Manfred Sangawe aliyekuwa akikabiliwa na kesi ya wizi wa fedha zaidi ya Shilingi milioni 130 za benki ya DCB.

Hakimu Mkazi Mkuu, Huruma Shaidi amemuachia huru mshtakiwa huyo, baada ya Wakili wa Serikali, Mwanaamina Kombakono kuomba aachiwe chini ya kifungu cha 91(1)  cha sheria ya Makosa ya Jinai,(CPA) kwa kuwa Mkurugenzi wa Mashtaka (DPP) hana nia ya kuendeleza mashtaka dhidi yake.

Baada ya kutolewa kwa maelezo hayo, mahakama iliridhia ombi hilo na kumuachia huru Sangawe.

Mbali na Sangawe,  wenzake sita akiwamo John Sarakikya, Hidergard Mahrurus na wafanyakazi wa benki hiyo, Suzan Kaboko na Belinda Chaula bado wanaendelea kukabiliana na kesi hiyo yenye mashtaka 14 yakiwamo ya kula njama, kughushi na wizi na ipo katika hatua ya usikilizwaji wa ushahidi wa mashahidi wa upande wa mashtaka.

Katika shtaka la kula njama, washtakiwa hao wote wanadaiwa tarehe tofauti kati ya Septemba mosi na Novemba 16, 2015 Dar es Salaam, walikula njama na watu wengine kuidanganya benki hiyo kuhusu Shilingi milioni 313.

Pia, washtakiwa hao wanakabiliwa na mashtaka ya kughushi barua na fomu za kuhamisha fedha za kiwango tofauti wanadaiwa kuyatenda katika benki hiyo tawi la Arnautoglou.

Washtakiwa hao wanadaiwa kuiibia benki hiyo viwango tofauti vya fedha ambavyo vinafikia zaidi ya Sh 139 milioni.

No comments:

Post a Comment

Post Bottom Ad