HABARI MPYA

Home Top Ad

Post Top Ad

Wednesday, November 1, 2017

WILAYANI YA CHATO YATAKIWA KUSIMAMIA FEDHA ZA MIRADI YA MAENDELEO

Utekelezaji wa ujenzi wa mradi wa uwanja wa ndege Chato ukiendelea.

Mhandisi Robert Gabriel Lughumbi Mkuu wa Mkoa wa Geita amewataka Viongozi wa Serikali Wilayani Chato kusimamia na kufuatilia kwa karibu utekelezaji wa miradi mbalimbali ya maendeleo Wilayani humo ili thamani ya fedha zinazotolewa ionekane.

Akizungumza baada ya kuwasili wilayani Chato kwa mara ya kwanza tangu kuteuliwa kwake kuwa Mkuu wa Mkoa amesema kuwa umefika wakati watendaji kuacha tabia ya kukaa Ofisini bali waende maeneo mbalimbali ya Wilaya ambapo kunatekelezwa miradi ili kusimamia kwa karibu miradi inayoendelea.

"Wananchi wanatakiwa kusimamiwa ata kama fedha ni za kwao ili kuweka miradi katika ubora unaotakiwa"Alisisitiza Lughumbi.

Aidha, alimuagiza Mkurugenzi wa Halmashauri ya Chato kuhakikisha wananchi wanakuwa katika vikundi ili vishiriki katika ujenzi na utekelezaji wa miradi mbalimbali ya maendeleo katika vijiji kwa kuchangia michango midogo midogo kama vile kutafuta mawe, kokoto, mchanga. Kazi kubwa ya Halmashauri ni kuhakikisha wahandisi wanasaidia kupeleka michoro na kusimamia ujenzi wa miradi ya Zahanati na madarasa katika vijiji husika.

Katika hatua nyingine Mkuu wa Mkoa amemuagiza Mkuu wa Wilaya ya Chato kufuatilia ujenzi wa Bweni la wanafunzi shule ya Sekondari Jikomboe ambalo limegharimu kiasi cha Shilingi milioni 75 ili kujiridhisha kama fedha hizo zimetumika kama ilivyokusudiwa na kuona kama thamani yake inaonekana.

Akiwa Wilayani Chato Mheshimiwa Robert Gabriel ametembelea shule ya Msingi Chato na kukagua ujenzi wa vyumba vya madarasa sita na vyoo, ujenzi wa Zahanati ya kijiji Mganza, ujenzi wa Bweni shule ya Sekondari Zakia Meghj pamoja na Ujenzi wa Soko la dagaa Kasenda na kuagiza takukuru kufika katika miradi hiyo ili kufuatilia matumizi ya fedha katika miradi ya Zahanati, Bweni na madarasa.

Vilevile Mkuu wa Mkoa ametembelea ujenzi wa uwanja wa ndege wa Chato na kupongeza jitihada za utekelezaji wa mradi huo zinazoendelea kwa kufikia asilimia 63. Awali Meneja wa Tanroads Mkoa wa Geita Mhandisi Haruna Senkuku alimweleza Mkuu wa Mkoa kuwa uwanja huo una Run way ya Kilometa 3 ambapo hadi kukamilika mradi utagharimu kiasi cha shilingi Bilioni 39.


Mhandisi Robert Gabriel Lughumbi Mkuu wa Mkoa wa Geita akizungumza na Viongozi mbalimbali wa Mkoa na Wilaya ya Chato baada ya kuwasili Wilayani Chato.Wakwanza kulia ni Mbunge wa Chato pia ni waziri wa Nishati Mheshimi Dkt Medard Kalemani. Meneja wa Tanroads Mkoa wa Geita Mhandisi Haruna Senkuku akifafanua jambo kwa Mkuu wa Mkoa wa Geita Mhandisi Robert Gabriel Lughumbi wakati wa ukaguzi wa ujenzi wa Uwanja wa ndege Chato alipotembelea na kujionea ujenzi katika moja kati ya ziara yake ya kikazi Wilayani Humo.
Mhandisi Robert Gabriel Mkuu wa Mkoa wa Geita akiongoza viongozi katika ukaguzi wa ujenzi wa uwanja wa ndege Chato. Mhandisi Robert Gabriel Mkuu wa Mkoa wa Geita akitoa maelekezo wakati akikagua maendeleo ya ujenzi wa uwanja wa ndege Chato.

(PICHA NA MAGESA JUMAPILI AFISA HABARI MKOA WA GEITA)

No comments:

Post a Comment

Post Bottom Ad