HABARI MPYA

Home Top Ad

Post Top Ad

Thursday, November 2, 2017

WATANZANIA WAISHIO CHINA WATAKIWA KUCHANGIA JUHUDI ZA KUKUZA UCHUMI WA TAIFA LA TANZANIA

 Balozi wa Tanzania nchini China Mhe. Mbelwa Kairuki akihutubia katika mkutano wa Shirikisho la Jumuiya ya Watanzania wanaosoma katika  Taifa la China(TASAFIC) uliofanyika mjini Wuhan, jimbo la Hubei hivi karibuni. 
Katibu Mkuu wa Shirikisho la Watanzania wanaosoma nchini China (TASAFIC) Bw. Remidius Emmanuel akizungumza katika mkutano wa Jumuiya hiyo uliofanyika mjini Wuhan, jimbo la Hubei hivi karibuni.

 Afisa Mwandamizi wa Ubalozi wa Tanzania nchini China (Mwambata wa Elimu) Bw. Lusekelo Gwassa Akifafanua jambo wakati wa Mkutano Mkuu wa TASAFIC kwa Mwaka 2017.
 Baadhi ya Watanzania wanaosoma nchini China waliohudhuria Mkutano Mkuu wa Shirikisho la Jumuiya ya Watanzania wanaosoma katika  Taifa la China(TASAFIC) uliofanyika mjini Wuhan, jimbo la Hubei hivi karibuni. 

Baadhi ya Watanzania waliohudhuria  Mkutano Mkuu wakiwa katika Picha ya pamoja na Balozi Mbelwa Kairuki

Na Happiness Shayo- China
Balozi wa Tanzania  nchini China  Mhe Mbelwa Kairuki amewataka Watanzania wanaosoma katika Taifa hilo  kutumia fursa hiyo kuunga mkono juhudi za Tanzania kuelekea Uchumi wa kati ifikapo  mwaka 2025.
Akizungumza katika Mkutano Mkuu wa shirikisho la Jumuiya za Watanzania wanaosoma katika  Taifa la China(TASAFIC) uliofanyika hivi karibuni katika mji wa Wuhan, Jimbo la Hubei.

Balozi Kairuki alisema kuwa yapo maeneo kadhaa ambayo Watanzania hao wanaweza  kutoa michango yao katika kuunga mkono juhudi za Serikali ya Awamu ya Tano kwenye ujenzi wa Viwanda  ili sekta hiyo isaidie na kuleta tija katika ukuaji wa Uchumi. 

Akizungumzia kuhusu sekta ya Utalii, Balozi Kairuki  aliitaja China kama soko jipya wanalopatikana watalii na kwamba kwa mwaka 2016 ni Wachina Millioni 120 waliokwenda nje ya nchi kutalii sawa na idadi ya watu wote wa  nchi za Tanzania,Kenya,Uganda,Burundi  na Rwanda,  idadi inayoonekana ni kubwa sana,ambapo kwa mwaka huo huo ni watalii 30,000 walipokelewa Tanzania kutoka China.

“Zipo hatua kadhaa ambazo sasa zimechukuliwa na Ubalozi wa Tanzania nchini China, hivi sasa tunazungumza  na kampuni kubwa inayomiliki mitandao ya kijamii hapa ya  China ya TENCENT ili tuweze kutumia mtandao wao wa QQ kurusha vivutio vyetu vya utalii hapa China mubashara, lakini pia mwezi huu tulikuwa na Mazungumzo na Serikali ya China kuwajulisha nia ya shirika letu la ndege la Air Tanzania kuanza safari za moja kwa moja kutoka Dar es Salaam hadi Guangzhou. Matarajio yetu ni kuona kwamba ifikapo Mwezi Septemba mwakani lengo hilo linatimia. Vilevile tumeanza kuzungumza na Mamlaka za China kuangalia uwezekano wa mashirika ya ndege ya China kuifanya Tanzania kuwa kitovu (HUB) ya safari zao Barani Afrika. Maana yake nini? Ndege kadhaa za China zinazokwenda Afrika zitakuwa zitasimamna (stopover) pale Dar es salaam au KIA au Mbeya (Songwe) kwa ajili ya kujaza mafuta na kupata huduma nyinginezo. Alisema Balozi Kairuki.

Kwa upande wa Sekta ya Elimu Balozi Kairuki  amewataka Watanzania wanaosoma katika taifa hili kuendelea kutafuta fursa za masomo hapa China kwa faida ya watanzania wengine na kwamba China ina vyuo takribani 2000 hivyo jambo hili sio jukumu la Ubalozi pekee, hususani maeneo yenye upungufu katika taifa letu, huku akitoa kipaumbele kwenye  kozi za Kilimo na Uhandisi ambazo alizitaja kama nguzo muhimu katika Uchumi wa viwanda.

“Kilimo ni uti wa mgongo wa taifa letu. Kilimo kimeajiri zaidi ya asilimia 70 ya Watanzania wote ambao wengi wao wapo vijijiji. tunahitaji kilimo kuzalisha malighafi za viwandani na hatuwezi kutimiza malengo ya kujenga uchumi wa viwanda bila kufanya maboresho makubwa ya sekta ya kilimo.Lakini pia tunaamini kabisa Mtanzania anayekuja kusoma uhandisi hapa China mbali na elimu ya darasani, atapata pia exposure kubwa ya kazi za uhandisi zinazofanyika hapa China na tayari tumeanza kuzungumza na makampuni ya ujenzi ya hapa China kuyaomba yatoe fursa kwa wanafunzi watanzania kufanya elective programs ili mshiriki kwenye miradi mikubwa ya ujenzi.

Aidha , Balozi Kairuki aliwataka Watanzania hao kutumia fursahizo kuvutia wawekezaji . “Tunahitaji uwekezaji wa mitaji, teknolojia na ujuzi katika kuanzisha na kuendesha viwanda nchini na  kazi yetu kubwa ni kuendelea kuvutia uwekezaji wa viwanda kutoka China sambamba na kutafuta teknolojia rahisi na nafuu zinazoweza kupelekwa nyumbani kuwezesha watanzania kufanya shughuli za uzalishaji. Hivi sasa uwekezaji nchini kutoka China unakadiriwa kufikia dola za kimarekani Bilioni 3.7. Lengo letu ni kufikia Dola za Kimarekani Bilioni 5 ifikapo mwaka 2020. Wanafunzi wanaosoma China ni muhimu kuwatumia pia Wahadhiri katika vyuo vyao, ambao wengi wao wanayo mahusiano na wa kichina ambao wana mitaji na wangependa kuwekeza barani Afrika. Alisema Kairuki.

Akihitimisha hotuba yake Balozi kairuki  aliwataka Watanzania hao  kuheshimu tamaduni na sheria za taifa la China,Kila mmoja kutambua kusudi la uwepo wake hapa nchini kuepuka maisha ya kifahari, Kuchukua tahadhari  juu ya Madawa ya Kulevya, kuepuka migomo  kwa kuzingatia taratibu na sheria za vyuo vyao,kutunza na kulinda Afya zao na kwa wanafunzi wa shahada za uzamili na Uzamivu aliwataka  kufanya Tafiti zenye tija kwa Taifa la Tanzania.Ingawa pia alitumia nafasi hiyo kuwatambua Watanzania kadhaa wanaosoma katika Taifa hilo kutambua michango wao mkubwa walioutoa kwa manufaa ya Tanzania kupitia sekta ya Kilimo na Uhandisi. 

Kwa upande wake Katibu Mkuu wa Shirikisho hilo Bw. Remidius Emmanuel alisema Mkutano huo  ulilenga kuwakutanisha Watanzania wote wanaosoma katika taifa la China  kwa lengo la kujadili masuala mbalimbali juu ya Elimu na changamoto mbalimbali wanazokutana nazo lakini pia kutengeneza sauti ya pamoja na kuona namna bora zaidi ya kutumia fursa hiyo ya uwepo wao katika taifa hilo kwa manufaa ya  Tanzania.

“Tunamshukuru sana Balozi wetu Mhe. Mbelwa Kairuki wakati wote amekuwa karibu na sisi lakini kutumia muda mwingi kuzifanya taaluma zetu katika matumizi mapana yanayolenga kuendana na sera za nchi yetu hususani kipindi hiki ambacho taifa letu liko kwenye kasi ya kuelekea uchumi wa kati.Kwa hiyo Madaktari,Wataalam kilimo ,Wahandisi,Wachumi  na wataalam wengine wote  sasa wanaelekeza taaluma zao  kwa manufaa ya taifa letu” Alisema Remidius.

Mapema akisoma Taarifa ya Mkutano huo Mwenyekiti wa Shirikisho hilo Bw,Hussein Mtoro alisema  mbali na kuwaunganisha Watanzania kwa Umoja wao , Shirikisho hilo linalo jukumu la kuhakikisha Watanzania wote wanaosoma katika taifa la China  wanatoa mawazo,fikra zao ,kwa kutumia taaluma na uzoefu wao  kwa manufaa ya Taifa la Tanzania.

"Shirikisho limeweza kuweka mazingira mazuri kwa Watanzania wanaowasili China kwa mara ya kwanza kila mwaka, tunaendelea kutatua changamoto kwa baadhi ya mawakala wasio waaminifu ambao wamekuwa wakiwatelekeza na kuwalaghai wanafunzi wapowaleta katika taifa hili,  lakini tunajivunia kuwa na  wataalamu mbalimbali ambao kutoa michango wa moja kwa moja kwa taifa letu, Mfano  wataalam kutoka fani za  Kilimo na uhandisi".Alisema Bw. Hussein

Mkutano huo Ulihudhuriwa na Watanzania wanaosoma katika  Taifa la China  na baadhi ya watumishi kutoka Ubalozi wa Tanzania nchini China. 

No comments:

Post a Comment

Post Bottom Ad