HABARI MPYA

Home Top Ad

Post Top Ad

Monday, November 20, 2017

Wabunge wawapongeza NSSF, PPF na magereza mradi wa kiwanda cha sukari cha mkoani Morogoro

KAMATI ya Bunge ya Katiba na Sheria imepongeza namna mifuko ya hifadhi ya jamii ya NSSF na PPF inavyotekeleza mradi wa pamoja wa ujenzi wa kiwanda cha sukari unaofahamika kama Mkulazi huku ikitoa wito kwa wadau hao kuhakikisha wanakamilisha mradi huo kwa wakati ili kulinusuru taifa na uhaba wa bidhaa hiyo.

Mwisho mwa wiki kamati hiyo ilitembelea mradi huo unaotekelezwa katika gereza la Mbigiri, lililopo Dakawa mkoani Morogoro kupitia kampuni Hodhi ya Mkulazi Holding inayoshirikiana na Jeshi la Magereza nchini.

"Baada ya kusikiliza mpango mikakati na kisha kutembelea shamba husika kiukweli kamati yetu imeridhishwa sana na jinsi wadau hawa wanavyotekeleza mradi huu. Ni wazi kuwa walifanya utafiti wa kutosha kabla na matunda yake kiukweli yameanza kuonekana kikubwa tu tunachowaomba wamalize mradi huu kwa wakati .'' alisisitiza  Mwenyekiti wa kamati hiyo Bw Mohamedi Mchengelwa.

Aidha, wajumbe wa kamati hiyo walionyesha kuridhiswa zaidi na namna mradi huo unavyohusisha wananchi walio jirani na maeneo ya mradi ambao mbali na kupata ajira za moja kwa moja pia wamepatiwa fursa ya kulima miwa ili kukiuzia kiwanda hicho, hatua waliyosema kuwa itapunguza tatizo la ajira na kuongeza kipato cha wananchi.

"Kingine kikubwa zaidi kwa wadau hawa ni kuhakikisha kuwa mradi huu hauishii kwenye kuzalisha sukari tu bali pia bidhaa zitokanazo na mabaki ya malighafi za miwa ikiwemo ethanol, vyakula vya mifugo pamoja na uzalishaji wa nishati umeme,'' alisema mjumbe Selemani Zedi huku akiungwa mkono na wenzie akiwemo Mbunge wa Wawi Ali Salehe.

Akijibu baadhi ya hoja za wabunge hao ambao pia walitaka kufahamu uwezekano wa mifuko hiyo kuwekeza kwenye sekta ya uvuvi hapa nchini  Waziri wa Kazi, Ajira, Sera, Bunge, Vijana na wenye ulemavu, Jenista Mhagama  alisema uwezekano huo upo ikiwa mamlaka zinazosimamia mifuko hiyo zikiwemo bodi pamoja na Mamlaka ya usimamizi na udhibiti wa sekta ya hifadhi ya jamii (SSRA) zitaridhia miradi hiyo kwa kuangalia vigezo muhimu.

"Ili kuwekeza kwenye miradi mikubwa kama hii inahitaji ruhusa za mamlaka mbalimbali zinazosimamia mifuko hiyo kwa kuwa mamlaka hizo pia zinahitaji kujiridhisha pasipo kuacha chembe ya shaka kuwa utekelezaji wa miradi hii haihatarishi fedha za wanachama japo habari njema ni kwamba kati ya miradi 27 inayotarajiwa kutekelezwa na mifuko hii tayari miradi 15 imepatiwa ruhusa ya utekelezwaji na mamlaka hizi,'' alisema.

Mwenyekiti wa Bodi ya Kampuni ya Mkulazi ambae pia ni Mkurugenzi Mkuu wa NSSF, Prof Godius Kahyarara pamoja na Mkurugenzi Mkuu wa Mfuko wa Pensheni wa PPF, Bw.William Erio, waliihakikishia kamati hiyo, serikali, wananchama na wadau wote wa mifuko hiyo kuwa hadi kufikia mwishoni mwa mwaka ujao mradi huo utakuwa tayari umeanza kuzalisha sukari pamoja na baadhi ya bidhaa ambatanishi kulingana na wito wa wabunge hao.

"Mradi huu mliotembelea leo unaolenga kuzalisha tani 50 za sukari kwa mwaka na ni sehemu tu ya mradi mkubwa unaotekelezwa na mifuko yetu miwili yaani NSSF na PPF ukiwepo mwingine mkubwa zaidi katika eneo la Ngerengere, Wilaya ya Morogoro Vijijini unaofahamika kama Mkulazi I ambao unaolenga kuzalisha tani 200,000 za sukari kwa mwaka,'' alisema Prof Kahyarara.

"Zaidi tuwahakikishie tu waheshimiwa wabunge kuwa hoja zenu tumezipokea na tutasimamia kuhakikisha kwamba mradi huu unakamilika kwa wakati na zaidi si tu kwamba tutalisha soko la ndani bali pia soko la nje hususani mataifa jirani ya Burundi na Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo,'' aliongeza Bw Erio.

Naye Mwakilishi wa jeshi la Magereza, Mkuu wa Magereza Mkoa wa Morogoro (RPO), Kamishna Msaidizi wa Magereza (ACP)Mzee Nyamka mbali na kuishukuru mifuko hiyo pia alitoa wito kwa mifuko mingine ya hifadhi ya jamii pamoja na  wadau wengine kujitokeza ili kushirikiana na Jeshi hilo katika utekelezaji wa miradi mingine huku akibainisha kuwa jeshi hilo lina eneo kubwa la ardhi pamoja na nguvu kazi ya kutosha.

Mkuu wa Mkoa wa Morogoro Dk Stephen Kebwe alisema mkoa wake umekuwa ukiupa kipaumbele kikubwa mradi huo kuwa utekelezaji wake pamoja na mambo mengine unalenga kuongeza ajira kwa wananchi wa mkoa huo na kupunguza kabisa kasi ya mfumuko wa bei ya sukari kwa kuongeza uzalishaji wa bidhaa hiyo muhimu. 
 Mwenyekiti wa Kamati ya Bunge ya Katiba na Sheria Bw Mohamedi Mchengelwa akizungumza na waandishi wa habari mara baada ya kukagua shamba kubwa la miwa lililopo katika gereza la Mbigiri lililopo Dakawa mkoani Morogoro ambalo ni sehemu ya mradi wa ujenzi wa kiwanda cha sukari kinachojengwa kwa ubia kati ya mifuko ya Hifadhi ya Jamii ya NSSF, PPF na jeshi la Magereza nchini.
 Waziri wa Kazi, Ajira, Sera, Bunge, Vijana na wenye ulemavu, Jenista Mhagama  (wa tatu kulia) akiwaongoza baadhi ya wajumbe wa kamati ya Bunge ya Katiba na Sheria  kukagua shamba hilo.
 Waziri wa Kazi, Ajira, Sera, Bunge, Vijana na wenye ulemavu, Jenista Mhagama  (katikati) akiwaongoza baadhi ya wajumbe wa kamati ya Bunge inayohusika na Katiba na Sheria chini ya mwenyekiti wake Bw Mohamedi Mchengelwa (wa pili kulia)  kukagua shamba hilo. Kulia ni Mkuu wa Mkoa wa Morogoro Dk Stephen Kebwe .
 Waziri wa Kazi, Ajira, Sera, Bunge, Vijana na wenye ulemavu, Jenista Mhagama  akizungumza na waandishi wa habari mara baada ya kukagua shamba hilo.
 Mwenyekiti wa Bodi ya Kampuni ya Mkulazi ambae pia ni Mkurugenzi Mkuu wa NSSF, Prof Godius Kahyarara akizungumza na waandishi wa habari mara baada ya kukagua shamba hilo. Kwa mujibu wa Prof. Kahyarara hadi kufikia mwishoni mwa mwaka ujao mradi huo utakuwa tayari umeanza kuzalisha sukari pamoja na baadhi ya bidhaa ambatanishi ikiwemo uzalishaji wa umeme.
 Mkurugenzi Mkuu wa Mfuko wa Pensheni wa PPF, Bw.William Erio, akizungumza na waandishi wa habari mara baada ya kukagua shamba hilo. Erio aliihakikishia kamati hiyo kuwa mradi huo unakamilika kwa wakati na utalisha pia soko la nje hususani mataifa jirani ya Burundi na Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo.
 Mwakilishi wa jeshi la Magereza, Mkuu wa Magereza Mkoa wa Morogoro (RPO), Kamishna Msaidizi wa Magereza (ACP)Mzee Nyamka akizungumza kwenye ziara hiyo.
 Wadau wote wakiwa kwenye picha ya pamoja.
 Pamoja na mambo mengine huo tayari umeanza kutoa ajira kwa wananchi wanaoishi jirani na eneo la mradi kama walivyokutwa siku ya ziara.
Waziri wa Kazi, Ajira, Sera, Bunge, Vijana na wenye ulemavu, Jenista Mhagama (Kushoto) akiagana na Mwenyekiti wa Bodi ya Kampuni ya Mkulazi ambae pia ni Mkurugenzi Mkuu wa NSSF, Prof Godius Kahyarara mara baada ya kumaliza ziara hiyo. Anaeshuhudia ni Mkurugenzi Mkuu wa Mfuko wa Pensheni wa PPF, Bw.William Erio (Katikati).

No comments:

Post a Comment

Post Bottom Ad