HABARI MPYA

Home Top Ad

Post Top Ad

Wednesday, November 1, 2017

VYAMA VYA SIASA VYATAKIWA KUTII MAADILI YA UCHAGUZI

Mkurugenzi wa Uchaguzi wa Tume ya Taifa ya Uchaguzi (NEC), Kailima Ramadhan akizungumza jana kuhusu uchaguzi mdogo wa madiwani unaofanyika katika kata 43. (Picha ya NEC).

TUME ya Taifa ya Uchaguzi (NEC) imesema kuwa katika uchaguzi mdogo wa madiwani utakaofanyika Novemba 26, 2017 katika kata 43 utagharimu kiasi cha Sh bilioni 2.5.

Mkurugenzi wa Uchaguzi wa NEC Kailima Ramadhani, alisema msingi wa bajeti ya uchaguzi unategemea idadi ya vituo vya kupigia kura na idadi ya wapiga kura walioandikishwa katika kata husika. Amesema idadi ya Wapiga Kura ndio inatoa bajeti ya mahitaji ya vifaa vya kuendeshea uchaguzi kama karatasi za kura pamoja na idadi ya  vituo ambavyo vinakuwa na watumishi wasiopungua wanne. Kailima alitoa mfano kwamba Kata yenye vituo 41 ina bajeti kubwa kuliko Kata yenye vituo vikubwa.

Alisema katika kituo cha kupigia kura kina watendaji wanne ambao ni Msimamizi na Msimamizi Msaidizi, karani mwongozaji na mlinzi wa kituo “lakini pia kuna watu wa ziada kama Wasimamizi Wasaidizi wako ngazi ya kata na jimbo ambao wanahusika kusimamia zoezi la Uchaguzi katika maeneo husika.

Alifafanua kuwa gharama nyingine za uchaguzi ziko kwenye usafirishaji wa vifaa kutoka Tume kwenda kwenye Halmashauri husika na kutoka Halmashauri kwenda kwenye kata ambako uchaguzi unafanyika.  Gharama hizo pia zanahusu utoaji wa Elimu ya Mpiga Kura kupitia machapisho mbalimbali ya Elimu ya Mpiga Kura, Maelekezo mbalimbali kwa Watendaji wa Uchaguzi n.k.

Elimu hiyo pia hutolewa kupitia Vyombo vya Habari pamoja na machapisho mbalimbali yatakayotumika kwa ajili ya kutoa elimu ya mpiga kura.

“Kwenye uchaguzi huu mdogo bajeti yetu ni Sh bilioni 2.5. Sio kwamba kila kata itatumia gharama sawa za fedha hizi, bali kuna kata itatumia milioni 20 kutokana na idadi ya vituo vya kupigia kura kuwa vichache na kata yenye vituo vingi kwenye uchaguzi huu itatumia Sh milioni 150,” alisema Kailima.

Tume pia imeviasa Vyama vya Siasa vinavyohusika kwenye uchaguzi mdogo wa madiwani kutekeleza maadili ya uchaguzi ya 2015 waliyokubaliana kuyafuata na ameonya kuwa chama au mgombea atakayekika maadili hayo atachukuliwa hatua kama ilivyoanishwa kwenye maadili hayo ya uchaguzi.

Mkurugenzi huyo amesema Vyama vya Siasa vinatakiwa kuhakikisha vinawaelemisha wafuasi,Wapenzi na Wananchama wao juu ya kutekeleza maadili hayo katika kipindi chote cha kampeni. Alisisitiza kuwa iwapo wafuasi wa vyama vya siasa watakikua maadili hayo, chama husika pamoja na mgombea wake watachukuliwa hatua za kinidhamu.

Alitaja baadhi ya vitendo vya kuvunja maadili ya uchaguzi ni kuchana mabango ya wagombea, kutoa lugha chafu wakati wa mikutano ya kampeni pamoja na kupitisha muda wa kufanya mikutano ya kampeni.

Alisisitiza kamati za maadili za kata na jimbo kuchukua hatua kali kwa chama au mgombea ambaye atakikuka maadili hayo. Alisema kamati hizo zinatakiwa kuchukua hatua ndani ya saa 48 mara chama au mgombea anapovunja maadili.

Alizitaja baadhi ya adhabu zitazowakabili wagombea au chama ambacho kitavunja maadili ya uchaguzi kuwa ni kuomba radhi wananchi hadharani, kutotumia vyombo vya habari kwa muda fulani wakati wa kampeni, onyo la maandishi, kusimamishwa kufanya kampeni, mgombea kutangaza mbele ya vyombo vya habari kuwa yeye ni bingwa wa kukikuka maadili ya uchaguzi au kutozwa faini Sh 100,000,

“Ni hatari kwa chama cha siasa kukiuka maadili, hivyo navisihi vyama vya siasa kuheshimu na kuzingatia maadili hayo,” alisema Kailima.  “Pia niwaombe vyama vya siasa vizingatie maadili kwenye mikutano yao, viende kuwaambia wananchi watawafanyia nini katika kata zao na sio vinginevyo,”alisema Kailima.

Kailima pia alisema chama cha siasa ambacho kinataka kufanya mabadiliko ya ratiba ya mikutano ya kampeni, lazima kimfahamishe msimamizi wa uchaguzi wa kata na ombi hilo lazima lijadiliwe na vyama vyote vinavyoshiriki kwenye uchaguzi.

Kuhusu vitambulisho mbadala vitakavyotumika wakati kupigia kura kwa wale ambao wamepoteza kadi ya mpiga kura ambavyo ni vitambulisho vya taifa, leseni ya udereva na hati ya kusafirisha; Kailima amesema vitambulisho hivyo vitatumika tu kwa watu ambao wameandikishwa katika Daftari la Kudumu la Wapiga Kura katika  kituo husika mwaka 2015, lakini pia bado wana sifa za kupiga kura.

“Masharti ya kutumia vitambulisho hivyo mbadala ni ya kisheria chini ya Sheria ya Uchaguzi wa Serikali za Mitaa kifungu 62 (a). Masharti yake ni lazima mtu awe bado na sifa ya kuwa mpiga kura, mfano mtu akishahukumiwa na kufungwa kwa kosa la kukwepa kodi, au amechukua uraia wa nchi nyingine au amewekwa kizuizini kwa mujibu wa sheria na katiba, mtu wa namna hiyo haruhusiwi kupiga kura hata kama ana kadi ya mpiga kura au vitambulisho hivyo vingine vitatu,”amefafanua Kailima.

Akizungumza Mikutano ya Kampeni Kailima alitoa wito kwa vyama vya siasa kutambua kwamba Tume ya Taifa ya uchaguzi imeruhusu mikutano ya kampeni na sio mikutano ya vyama vya siasa. Amesema mtu anayeruhusiwa kwenye mikutano ya kampeni ni mgombea mwenyewe, chama chake au mtu yeyote ambaye anaona anaweza kumfanyia kampeni ndani ya katiba iliyopitishwa.

No comments:

Post a Comment

Post Bottom Ad