HABARI MPYA

Home Top Ad

Post Top Ad

Thursday, November 9, 2017

SERIKALI IMEZINDUA NDEGE MAALUMU ITAKAYOFANYA DORIA KATIKA ENEO LA BAHARI KUU KUDHIBITI UVUVI HARAMU

 Naibu Waziri wa Wizara ya Mifugo na Uvuvi,Abdallah Ulega akizungumza na waandishi wa habari (hawapo pichani) juu ya operesheni ya kutumia ndege maalumu itakayofanya doria katika eneo la bahari kuu kudhibiti uvuvi haramu, leo jijini Dar es Salaam. Kulia  ni Waziri wa Kilimo, Maliasili, Mifugo na Uvuvi Zanzibar, Mhe. Hamad Rashid Mohamed.


Serikali imezindua mkakati unaolenga kutokomeza uvuvi haramu  kwa kuanzisha operesheni ya kutumia ndege maalumu itakayofanya doria katika eneo la bahari kuu.

Akizungumza wakati wa kuzindua safari ya ndege ya kutoka nchini Mauritius iliyotua hapa nchini kwa mara ya kwanza kwa ajili ya kufanya doria ya majini, Naibu Waziri wa Wizara ya Mifugo na Uvuvi Abdallah Ulega alisema lengo ni kudhibiti uvuvi haramu katika eneo la bahari kuu.

Alisema Serikali ya awamu ya tano imejipambanua juu ya ulinzi wa rasilimali ya nchi ikiwamo ya uhakika ya majini, licha ya kukumbwa na dhoruba kubwa.

Alieleza kutoka na hilo ndiyo maana wameunganisha nguvu kwa pamoja kati yao na Ukanda wa nchi za Kusini Magharibi mwa Bahari ya Hindi kudhibiti uvuvi haramu kwa njia zote.

“Tunaruhusu ndege ya doria leo, ili kuongezea nguvu njia za kudhibiti wavuvi haramu, tulianza kwa njia ya bahari na sasa ni kwa njia ya anga.

“Changamoto ya uvuvi haramu ni kubwa, mtu anapiga bomu kwenye matumbawe anafanya uharibifu ambao kuyatengeneza tena yanachukua zaidi ya miaka 100, huku yeye akiharibu kwa dakika tano, ” alisema Ulega.

Ulega alisema uharibifu huo ndiyo unachangia kuwatia umasikini wavuvi wengi kwa sababu siyo rahisi kupata samaki karibuni na kulazimika kwenda mbali ambako siyo rahisi kufika bila kuwa na vyombo maalumu.

Kwa upande wa Waziri wa Kilimo, Maliasili, Mifugo na Uvuvi wa Serikali ya Mapinduzi Zanzibar Hamad Rashid alisema atashauriana na marais wa pande zote mbili kuangalia namna ya kurudisha Shirika la Uvuvi Tanzania (Tafico) na Shirika la Uvuvi Zanzibar (Zafico).

Alisema mashirika hayo yakifanya kazi kwa kushirikiana wananchi watapata fursa ya kufurahia matunda yatokanayo na utajiri uliomo baharini.

“Katika mwendelezo wa kupambana na uvuvi haramu na kulinda bahari ya Hindi Serikali ya Mapinduzi Zanzibar ilifanya mazungumzo ya kuingia ubia na Serikali ya China na tayari kuna meli 10 zinafanya doria.

“Serikali pia imeagiza boti 500 watakazopewa wavuvi ili wazitumie kuvua kisasa, pia inasimamia ujenzi wa soko la samaki la kisasa na namna bora ya kuhifadhi samaki awe katika hali yake ile ile hadi anamfikia mlaji, ” alisema Rashid.

Alisema uvuvi haramu siyo tu janga kwa kuondoa rasilimali za bahari, pia ukiachwa uendelee unaweza kuwa chanzo cha biashara nyingine haramu ikiwamo usafirishaji wa watu, biashara ya dawa za kulevya na utakatishaji fedha.

Nae Katibu mkuu Uvuvi Dk Yohana Budeba alisema ndege hiyo itafanya doria ya anga kwa siku nne.

Kwa upande wa Kaimu Mkurugenzi Mkuu wa Mamlaka ya kusimamia uvuvi wa bahari kuu Hosea Mbilinyi alisema ndege hiyo licha ya kuzunguka angani ikifanya doria, ina uwezo wa kupiga picha na kueleza kinachoendelea.

Alisema doria hiyo ni ya kikanda ambayo inahusisha nchi nane zikiwamo Tanzania Kenya, Msumbiji, Ushelisheli, Reunion, Comoro, Mauritius na Madagascar.


  Naibu Waziri wa Wizara ya Mifugo na Uvuvi,Abdallah Ulega akishuka kwenye ndege maalumu itakayofanya doria katika eneo la bahari kuu kudhibiti uvuvi haramu mara baada ya kuigangua ndani.
 Waziri wa Kilimo, Maliasili, Mifugo na Uvuvi Zanzibar, Mhe. Hamad Rashid Mohamed na Naibu Waziri wa Wizara ya Mifugo na Uvuvi,Abdallah Ulega pamoja na viongozi mbalimbali wakiangalia ndege maalumu ya doria katika eneo la bahari kuu kudhibiti uvuvi haramu.
 Waziri wa Kilimo, Maliasili, Mifugo na Uvuvi Zanzibar, Mhe. Hamad Rashid Mohamed naNaibu Waziri wa Wizara ya Mifugo na Uvuvi,Abdallah Ulega na viongozi mbalimbali wakiwa katika picha ya pamoja


  Naibu Waziri wa Wizara ya Mifugo na Uvuvi,Abdallah Ulega na Waziri wa Kilimo, Maliasili, Mifugo na Uvuvi Zanzibar, Mhe. Hamad Rashid Mohamed akitoa zawadi kwa marubani wa ndege hiyo. Picha zote na Emmanuel Massaka,Globu yajamii.

No comments:

Post a Comment

Post Bottom Ad