HABARI MPYA

Home Top Ad

Post Top Ad

Friday, November 10, 2017

RAIS MAGUFULI ATENGUA UTEUZI WA MKURUGENZI MTENDAJI WA HALMASHAURI YA WILAYA YA TUNDURU

Rais John Magufuli ametengua uteuzi wa Mkurugenzi Mtendaji wa Halmashauri ya Wilaya ya Tunduru, Abdallah Mussa kwa kushindwa kumudu majukumu yake.
Kuenguliwa kwa Mussa kunafanya idadi ya wakurugenzi watendaji wa halmashauri za wilaya walioondolewa madarakani kufikia watatu ndani ya siku tatu.
Taarifa iliyotolewa kwa vyombo vya habari na mkuu wa kitengo cha mawasiliano serikalini katika ofisi ya Tamisemi, Rebecca Kwandu imemkariri Katibu Mkuu Ofisi ya Rais Tamisemi, Mussa Iyombe akisema jana mjini Dodoma kwamba kutokana na hatua hiyo, uteuzi wa mkurugenzi mwingine kujaza nafasi hiyo utafanyika baadaye.
Jumatatu wiki hii, Rais Magufuli alitengua uteuzi wa mkurugenzi wa Halmashauri ya Manispaa ya Bukoba, Erasto Mfugale na wa Halmashauri ya Bukoba, Mwamtumu Dau baada ya kushindwa kutaja kiasi cha fedha za Mfuko wa Barabara walizopokea walipoulizwa na Rais Magufuli wakati wa uzinduzi wa Uwanja wa Ndege wa Bukoba.
Taarifa ya Tamisemi haijaeleza kosa la Mussa zaidi ya kusema ameshindwa kumudu majukumu yake, lakini mkuu wa Wilaya ya Tunduru, Juma Homera alisema hivi karibuni kuwa ataiandikia ofisi ya Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali (CAG) kufanya ukaguzi wa miradi ya maendeleo, akisema kuna ufisadi.
Homera alisema amebaini kuwepo kwa ubadhirifu mkubwa wa mabilioni ya fedha za miradi ya Serikali na kusababisha kutofanya kazi, akitoa mfano uchakachuaji wa zaidi ya Sh3 bilioni za ujenzi wa miradi ya umwagiliaji.

Chanzo: Mwananchi

No comments:

Post a Comment

Post Bottom Ad