HABARI MPYA

Home Top AdPost Top Ad

Wednesday, 15 November 2017

JESHI ZIMBABWE LAWATIA NDANI MAWAZIRI WATATU

Mawaziri kadhaa katika serikali ya Rais Robert Mugabe wamekamatwa baada ya Jeshi la Ulinzi kuonyesha uwezo wake na kushikilia majengo yakiwemo ya shirika la utangazaji (ZBC).
Milipuko mikubwa ilisikika na ikafuatiwa na ya bunduki katika maeneo yanayokaliwa na watu maarufu ya Borrowdale usiku kucha hali iliyozidisha hofu kwamba jeshi lilikuwa kazini.
Shirika la TimesLIVE limeripoti kwamba waliokamatwa ni watu maarufu kutoka kundi la G40 ndani ya chama cha Zanu PF lililokuwa likiongozwa na memsapu wa Rais Mugabe, Grace Mugabe.
Baadhi ya watu waliokamatwa ni Waziri wa Elimu Jonathan Moyo‚ Serikali za Mitaa Saviour Kasukuwere na Waziri wa Fedha Ignatius Chombo.
Jeshi limesema katika taarifa yake iliyosomwa na msemaji wake moja kwa moja kupitia ZBC kwamba Rais Mugabe yuko “salama na mwenye afya njema”. Taarifa hii imekuja baada ya askari wakiwa na silaha jana Jumanne kwenda katikati ya mji wakiwa kwenye magari ya kijeshi.
Shirika la Utangazaji la Zimbabwe ambalo majengo yake yako eneo la Pocket Hills jijini Harare lilitekwa saa 10:00 alfajiri.
Msemaji wa jeshi, Meja Jenerali Sibusiso Moyo alitangaza kwamba jeshi lilikuwa linadhibiti kwa lengo la kuhakikisha linawashughulikia “wahalifu” wanaomzunguka Mugabe.
“Sisi tunawalenga wahalifu wanaomzunguka yeye (Mugabe) wanaofanya uhalifu ambao unawasababishia watu mateso katika Nyanja za kijamii na kiuchumi hapa nchini na kisha tutawafikisha kwenye vyombo vya sheria‚” alisema Moyo.

Chanzo: Mwananchi
Picha na Daily Mail

No comments:

Post a Comment

Post Bottom Ad