HABARI MPYA

Home Top Ad

Post Top Ad

Friday, November 17, 2017

BENKI YA KILIMO YAASWA KUWEZESHA MIRADI YA MAENDELEO SIMIYU

 Mkurugenzi wa Biashara na Mikopo wa TADB, Bw. Augustino Matutu Chacha (aliyesimama) akizungumza wakati walipofanya ziara ya kujionea miradi ya kilimo mkoani Simiyu.
 Mwenyekiti wa Bodi ya Wakurugenzi wa Benki ya Kilimo, Bibi Rosebud Kurwijila (kulia) akizungumza na Mkuu wa Mkoa wa Simiyu (hayupo pichani) kuhusu nafasi ya TADB katika kuwasaidia wakulima nchini.
 Mkuu wa Mkoa wa Simiyu, Bw. Anthony Mtaka akizungumza na ugeni kutoka Benki ya Kilimo (hawapo pichani) katika kikao kilichofanyika Mjini Bariadi kati ya uongozi wa Mkoa huo, wataalam wa kilimo, mifugo na ushirika na Bodi ya Wakurugenzi wa Benki ya Kilimo.
 Mjumbe wa Bodi ya Wakurugenzi ya TADB, Bw. Dome Malosha (kulia) akizungumza katika Kikao na Mkuu wa Mkoa wa Simiyu.
Mmoja wa wajumbe wa Bodi ya Wakurugenzi wa Benki ya Kilimo nchini, Bw. Joseph Mutashubilwa (wapili kulia) akichangia hoja wakati wa walipomtembelea Mkuu wa Mkoa wa Simiyu, Bw. Anthony Mtaka (hayupo pichani).

Na Mwandishi wetu, Simiyu 
Mkuu wa Mkoa wa Simiyu, Bw. Anthony Mtaka  ameiomba Benki ya Maendeleo ya Kilimo Tanzania (TADB) kuuwezesha mkoa wa Simiyu katika kufanya mapinduzi ya Kilimo kupitia miradi ya kimkakati inayotekelezwa mkoani humo.
Bw. Mtaka amesema mkoa wa Simiyu umejipanga kutumia fursa za mikopo nafuu inayotolewa na TADB ili kuunga mkono juhudi za serikali za kuhakikisha wakulima wanalima kisasa ili kuleta mapinduzi ya kilimo nchini.
Bw. Mtaka aliongeza kuwa Mkoa wa Simiyu uko tayari kufanya kazi na Benki ya Kilimo kupitia vikundi vya uzalishaji, Halmashauri na Miradi mbalimbali inayotekelezwa mkoani humo, ikiwa ni pamoja na miradi ya mfano ya umwagiliaji ya Mwamanyili Wilayani Busega  ulio katika hatua ya upembuzi yakinifu na Mwasubuya wilayani Bariadi ambao uko katika hatua ya ujenzi wa miundombinu ya umwagiliaji.
“Tungehitaji kuwa Mkoa ambao kupitia Benki ya Maendeleo ya Kilimo tungetengeneza namna ambayo ingewasaidia wakulima na ikasaidia mikoa mingine kuja kuona maendeleo ya kilimo  ambayo ni matokeo ya Serikali kuwekeza katika Benki ya Kilimo” amesema Mtaka.
"Sisi kama Mkoa tumejipanga, tumetoa Elimu ya utayari na
namna ya utekelezaji wa shughuli zote kwa wataalam wetu pamoja na wananchi na isitoshe tayari tumeshafanya utafiti na kuandaa mwongozo wa uwekezaji ndani ya mkoa, hivyo tunawakaribisha kuwekeza,” aliongeza.
Aidha, Bw.Mtaka ameongeza kuwa Mkoa wa Simiyu unatekeleza Sera ya Uchumi wa Viwanda chini ya Kauli Mbiu ya “Wilaya Moja Bidhaa Moja Kiwanda Kimoja” ambapo hadi sasa kuna kiwanda cha chaki na maziwa na miradi mingine minne ya viwanda iko katika upembuzi yakinifu.
“Hivyo Benki ya Kilimo inaweza kuwekeza katika miradi hii kwa kuwawezesha wakulima na wafugaji kuzalisha malighafi ya Viwanda hivyo au kuwa mdau katika viwanda hivyo,” aliomba.
Kwa upande, Mwenyekiti wa Bodi ya Wakurugenzi wa Benki hiyo, Bibi Rosebud Kurwijila alisema kuwa Benki ya Kilimo imejizatiti katika kuchangia kwa kiasi kikubwa katika  kuleta Mapinduzi yenye tija katika Sekta ya Kilimo kwa wakulima wa Tanzania ili kusaidia upatikanaji wa fedha na sera nzuri zitakazosaidia maendeleo ya kilimo nchini.

Bibi Kurwijila alisema kuwa katika kutekeleza mkakati wa kuwafikia wakulima wengi zaidi nchini TADB imejipanga kutoa huduma kupitia kongani mpya nane (8) ili kuongeza tija kwa wakulima nchini.

Alizitaja Kongani hizo kuwa ni pamoja na Kanda ya Kati, Kanda ya Ziwa, Kanda ya Kaskazini na Kanda ya Mashariki. Nyingine ni Kanda ya Magharibi, Kanda ya Nyanda za Juu Kusini, Kanda ya Kusini na Zanzibar.

“Kongani ni njia ya kimkakati ya kijiografia yenye kujikita katika shughuli za kilimo zinazohusiana, wasambazaji, na taasisi zinazohusishwa katika kujenga usawa wa moja kwa moja miongoni mwa wadau, hivyo ili kukidhi mahitaji ya wakulima nchini, benki ya kilimo itawafikia kupitia njia hii,” alisema.

Naye Mkurugenzi wa Biashara na Mikopo wa TADB Augustino Matutu Chacha  amesema wamefurahishwa na utayari wa Mkoa wa Simiyu juu ya kuwawezesha wakulima na Benki hiyo iko tayari kutoa mikopo pia kwa wakulima wa zao la pamba ambao wanazalisha zaidi ya asilimia 60 ya pamba yote nchini ili izalishwe kwa wingi zaidi na katika ubora wa hali ya juu.
Bw. Chacha amesema wataalam wa kilimo wa Mkoa wa Simiyu kwa kushirikiana na wataalam wa benki ya Maendeleo ya kilimo Tanzania (TADB) watakutana ili kuona namna watakavyofanya kazi kwa pamoja ili mikopo itakayotolewa iweze kuwa wa manufaa kwa wakulima na nchi kwa ujumla.
Aidha amewaeleza Wakurugenzi wa Halmashauri zote kuwa, Halmashauri zinaweza kupatiwa mikopo ili ziweze kuendesha miradi ya kilimo itakayoweza kuwa  vyanzo vipya vya mapato kwa Halmashauri zao.

No comments:

Post a Comment

Post Bottom Ad