HABARI MPYA

Home Top Ad

Post Top Ad

Tuesday, November 7, 2017

AZIMIO LA “BALFOUR” SIO MNASABA WA KUSHEREHEKEA

Imeandikwa na Rais wa Taifa la Palestina, Mheshimiwa Mahmuud Abbas
Waingereza wengi hawamjui “Sir.Arthur James Balfour”ambae aliwahi kuwa Waziri Mkuu mwanzoni mwa karne ya ishirini, lakini jina lake ni maarufu sana kwa Wapalestina wapatao milioni kumi na mbili. Katika kumbukumbu ya azimio la Balfour,serikali ya Uingereza inalazimika kutumia fursa hiyo ili kurekebisha makosa ya kihistoria iliyoyafanya dhidi ya wananchi wetu wa Palestina.

Mnamo Novemba 2,1917 akiwa ofisini kwake mjini London,“Sir.Arthur James Balfour”alisaini barua akiliahidi shirika la kizayuni, kuanzisha taifa lao ndani ya ardhi ya Palestina. Ameahidi kutoa ardhi hiyo wakati sio yake, huku akifumbia macho haki za kisiasa za Wapalestina walioishi katika ardhi hiyo kwa miaka mingi. Kwa Wapalestina ambao ni raia wangu, matukio yaliyosababishwa na barua hii yamekuwa na uharibifu mkubwa, huku pia yakiacha madhara ya muda mrefu kwa wananchi wetu.

Sera ya Uingereza iliyounga mkono uhamaji wa Wayahudi kwenda Palestina, ikiwa ni mbadala wa kukataa kwao haki ya Kiarabu ya Palestina ya kujipangia mustakabali wao, sera hiyo imeleta mvutano mkali kati ya wahamiaji wa Kiyahudi wa Ulaya na wakazi wa asili wa Kipalestina. Palestina iliyokuwa ajenda ya mwisho ya kumaliza ukoloni, inasumbuka kama tunavyosumbuka wananchi wake kutafuta haki yetu isiyo badilika katika kujipangia mustakabali, jambo ambalo ni janga kubwa mno kushuhudiwa na historia ya sasa.

Mnamo mwaka 1948, wanajeshi wa kizayuni waliwafukuza kwa mabavu kutoka katika miji yao, watu wanaofikia milioni moja wakiwemo wanawake na watoto, huku wakifanya mauaji ya kutisha na kubomoa kabisa vijiji kadhaa. Wakati tulipofukuzwa kwa mabavu kutoka mji wa Safad, umri wangu ulikuwa miaka kumi na tatu, wakati Israel ikisherehekea kuasisi taifa lake, sisi Wapalestina tunakumbuka siku ya giza zaidi katika historia yetu. 

Azimio la “Balfour” kwa hakika sio tukio la kusahaulika, kwani wananchi wangu leo wanaofikia zaidi ya milioni kumi na mbili wamesambaa duniani kote, baadhi yao wakilazimishwa kwa nguvu kuacha miji yao mnamo mwaka 1948, huku zaidi ya Wapalestina milioni sita bado wanaishi uhamishoni hadi leo hii, waliosalia katika miji yao ni milioni (1.75) ila wao wanaishi chini ya mfumo wa kibaguzi uliopangika nchini Israel.

Aidha, Wapalestina zaidi ya milioni (2.9) wanaishi Ukingo wa Magharibi wakiwa chini ya uvamizi wa kijeshi na wa kinyama uliogeuka kuwa ni ukoloni. Miongoni mwao wapo wakazi wa Jerusalem ambao ni wa asili kabisa wapatao laki tatu (300,000), bado wanapambana na sera za kivamizi za Israel zinazowahamisha kwa nguvu kutoka katika mji wao. Huku wapalestina wengine wapatao milioni mbili wapo katika Ukanda wa Gaza, ambayo ni gereza la wazi linaloharibiwa mara kwa mara na vifaa vya jeshi la Israel.

Azimio la “Balfour” kwa hakika sio mnasaba wa kusherehekea, hasa katika wakati ambao bado upande mmoja unadhulumiwa na unapata dhiki kwa sababu ya azimio hilo, kuasisiwa kwa taifa la watu fulani, kumepelekea kufukuzwa kwa watu wengine na kuendelea kukandamizwa, haiwezekani kulinganisha kati ya mvamizi na taifa linalokaliwa kimabavu. Ni lazima kulisawazisha kosa hili ambalo Uingereza inabeba jukumu kubwa na inalazimu sherehe hizo zifanywe katika siku ambayo, wakazi wote wa ardhi hii wakiwa katika uhuru, heshima na usawa. 

Tukio la kusaini azimio la “Balfour”, limeshatokea na halibadiliki lakini ni jambo ambalo yapasa kurekebishwa, jambo hili linahitaji unyenyekevu, ushujaa, kukubali yaliyopita, kukiri makosa na kuchukuwa hatua stahiki za kurekebisha makosa hayo. Nami katika mtiririko huu, ninapongeza ushujaa wa wananchi wa Uingereza wanaoitaka serikali yao kuchukua hatua kama hizi zifuatazo: Wabunge 274 wamepiga kura ya kulitambua taifa la Palestina, wakati maelfu ya wananchi wakiitaka serikali yao kuomba radhi kwa azimio la Balfour, huku makundi kadhaa na asasi za kiraia zikiandamana kuunga mkono haki za taifa letu bila usumbufu wowote.

Pamoja na mateso tuliyokumbana nayo karne iliyopita, bado wananchi wa Palestina wamesimama kidete, kwani sisi ni wananchi tunaojifaharisha kwa urithi wake mwingi, ustaarabu wake mkongwe na kwa kutambua ya kwamba Palestina ndio chimbuko la dini tatu za mbinguni. Ukweli wa mambo, tumezoea kwa miaka mingi kuishi na matukio yaliyotuzunguka, ambayo yamesababishwa na mtiririko wa matukio yaliyoanza mwaka 1917, tukafikia makubaliano machungu kwa ajili ya kufikia amani, kuanzia kukubali kuasisiwa taifa la Palestina kwa asilimia 22% tu ya ardhi ya kihistoria, kulitambua taifa la Israel bila ya sisi kutambuliwa hadi leo hii.

Tukawa na msimamo wa ufumbuzi wa dola mbili kwa muda wa miaka thelathini iliyopita, msimamo ambao utekelezaji wake umekuwa hauwezekani pamoja na muda kupita. Hivyo basi, muda wa kuwa Israel inaendelea kupata kinga na misaada kutoka jamii za kimataifa, badala ya kuichukulia hatua kwa ukiukaji wake unaoendelea dhidi ya misingi ya sheria za kimataifa, jambo hilo halitaihamasisha kuacha uvamizi wake na lazima huu utakuwa ni mtazamo dhaifu.

Inapasa kwa Israel na marafiki zake kutambua vizuri kuwa, ufumbuzi wa kuwepo dola mbili unaweza kwisha kabisa, isipokuwa taifa la Palestina litabaki hapa na kuendelea na juhudi zake ili kurudisha uhuru wake, iwe kupitia ufumbuzi wa dola mbili au mapambano kwa ajili ya kujipatia haki sawa kwa kila mkazi wa Palestina ya kihistoria.

Muda umefika sasa kwa serikali ya Uingereza kuchukua nafasi yake, kwani kuchukua hatua stahiki kunalenga kumaliza uvamizi kwa mujibu wa sheria za kimataifa na maazimio yake, likiwemo azimio la hivi karibuni la Baraza la Usalama namba 2334 na kulitambua taifa la Palestina kwa mujibu wa mipaka ya mwaka 1967, lenye mji mkuu wake Jerusalem ya Mashariki. Kufanya hivyo, kutapeleka mbele upatikanaji wa haki za kisiasa za wananchi wa Palestina, kuondoa dhulma kwa wananchi hao na usawa wa haki zake za kisheria, bila shaka utachangia kupatikana amani iliyo sawa ya uadilifu na ya kudumu katika Mashariki ya Kati kwa Wapalestina, waisrael na mataifa mengine ya eneo husika. 

Mahmoud Abbas, Rais wa taifa la Palestina na Mwenyekiti wa Kamati ya utendaji ya P.L.O

No comments:

Post a Comment

Post Bottom Ad