HABARI MPYA

Home Top Ad

Post Top Ad

Wednesday, October 25, 2017

WAMILIKI VYUO VYA UDEREVA WATAKIWA KUONGEZA MUDA WA MAFUNZO

  Mhandisi John Gunda wa karakana ya Magari katika Chuo Cha Ufundi Arusha (Arusha Technical College) akimuelezea mgeni rasmi Kamanda wa Polisi mkoa wa Arusha Naibu Kamishna (DCP) Charles Mkumbo kupitia "Screen" namna mfumo wa Injini ya gari unavyofanya kazi. (Picha na Rashid Nchimbi wa Jeshi la Polisi Arusha)
 Naibu Mkuu wa Chuo cha Ufundi Arusha (Mwenye koti la bluu) Mhandisi Dr. Erick Mgaya akimuelezea Kamanda wa Polisi mkoa wa Arusha Naibu Kamishna (DCP) Charles Mkumbo namna mashine mbalimbali zinavyofanya kazi katika karakana ya magari iliyopo chuoni hapo. (Picha na Rashid Nchimbi wa Jeshi la Polisi Arusha)
 Kamanda wa Polisi mkoa wa Arusha Naibu Kamishna (DCP) Charles Mkumbo akimkabidhi cheti mmoja wa wahitimu wa mafunzo ya udereva katika chuo cha ufundi Arusha, mwenye koti la bluu ni Naibu Mkuu wa Chuo Mhandisi Dr. Erick Mgaya na kushoto kwake ni Mkuu wa Kikosi cha Usalama Barabarani mkoa wa Arusha Mrakibu wa Polisi Joseph Bukombe. (Picha na Rashid Nchimbi wa Jeshi la Polisi Arusha)

Na Rashid Nchimbi wa Jeshi la Polisi Arusha
Wamiliki wa vyuo vya udereva mkoani Arusha wameombwa kuongeza muda wa mafunzo ya udereva kutoka wiki nne hadi wiki nane ili kuweza kutoa madereva wahitimu wenye viwango vya hali ya juu.

Hayo yameelezwa na Kamanda wa Polisi Mkoa wa Arusha Naibu Kamishna (DCP) Charles Mkumbo alipokuwa akizindua mafunzo ya udereva yanayoendeshwa na Chuo Cha Ufundi Arusha (Arusha Technical College) jijini hapa.

Kamanda Mkumbo alisema endapo vyuo hivyo vitatoa mafunzo hayo kwa muda mrefu bila kuogopa gharama za uendeshaji vitawasaidia wahitimu kupata uzoefu na wakati mwingine kupata fursa za ajira moja kwa moja pindi wamalizapo mafunzo yao.

Kamanda Mkumbo aliwashauri madereva wasiopitia mafunzo wajiunge na vyuo kwani ajira zao zipo hatarini na kuwaeleza wahitimu wapya milango yao ya ajira kwa sasa imefunguliwa kwa kuwa ujuzi wao na vyeti vyao ni sifa mojawapo.

Aidha Kamanda Mkumbo ambaye alikuwa ameambatana na Mkuu wa Kikosi cha Usalama barabarani Mrakibu wa Polisi Joseph Bukombe, amewataka wahitimu hao kuzingatia sheria za usalama barabarani ili kuepusha ajali zilizo ndani ya uwezo wao.

“Hayo yatawezekana endapo mtafuata sheria za udereva kama vile kufanya ukaguzi wa chombo cha usafiri kabla ya kuanza safari, kutoendesha gari mkiwa mmechoka au kulewa pombe na kutotumia simu wakati mnaendesha”. Alifafanua Kamanda Mkumbo.

Mwisho alitoa pongezi kwa Chuo hicho kwa kuanzisha Progamu hiyo ya mafunzo ya udereva kwani anaamini kitakuwa kinatoa madereva wenye uweledi wa hali ya juu kutokana na kuwa na wataalamu waliobobea na hii ni ishara ya kuliunga mkono Jeshi la Polisi katika kupunguza ajali za barabarani kama si kukomesha kabisa.

Akitoa historia ya chuo hicho Naibu Mkuu wa Chuo hicho cha Ufundi Arusha  Mhandisi Dr. Erick Mgaya alisema kwamba awali chuo kilianza udahili mwaka 1978 ambapo kilikuwa kinatoa mafunzo katika progamu tano.

Na kuongeza kwamba, pamoja na chuo hicho kukua na kutoa elimu kwa kiwango cha Shahada ya kwanza lakini pia walisukumwa kuanzisha progamu ya udereva kwa nia ya kutoa fursa kwa wanafunzi wa chuo hicho hasa wa ufundi wa magari kujifunza udereva na kuwa na leseni.

Alisema wanafunzi hao lazima wawe wanafanya majaribio ya uendeshaji wa magari hivyo mafunzo hayo pamoja na leseni watakazopata zitawasaidia kuendesha magari yao ndani na hata nje ya chuo bila kuwa na shaka.

Jumla ya wahitimu 76 baadhi yao wakiwa wafanyakazi na wanafunzi wa chuo hicho pamoja na watu wengine wasio wanafunzi kutoka nje ya chuo hicho walioanza mafunzo hayo toka tarehe 15.08.2017 wametunukiwa vyeti baada ya kuhitimu mafunzo hayo ambayo yalikuwa yanasimamiwa na Mhandisi David Mtunguja pamoja na walimu wengine 14.

No comments:

Post a Comment

Post Bottom Ad