HABARI MPYA

Home Top AdPost Top Ad

Saturday, 14 October 2017

WAHAMIAJI HARAMU 106 WAKAMATWA WILAYANI NGARA

Idara ya uhamiaji katika mkoa wa Kagera imeendesha operesheni maalumu katika wilaya ya Ngara na Biharamulo na kufanikiwa kuwakamata wahamiaji haramu 106 walioingia kinyemela katika wilaya hizo kutoka  katika nchi za Rwanda na Burundi na watanzania wawili wanaokabiliwa na tuhuma ya kuwaingiza baadhi ya wahamiaji haramu hao.
Wahamiaji haramu 62 waliokamatwa walikuwa wakifanya kazi ya vibarua mashambani na 44 walikamatwa kwenye maeneo vizuizi vya ukaguzi wa magari vilivyowekwa barabarani na idara hiyo, baadhi ya wahamiaji waliozungumza mbele ya afisa uhamiaji wa wilaya ya Ngara, Marwa Nyanswi aliyetoa onyo kwa wanaowasafirisha na wanaowaingiza wamesema kuwa wanalazimika kukimbilia hapa nchini kwa lengo kutafuta ajira kwa kuwa katika nchi wanakotoka hali ya maisha ni ngumu. 

Idara hiyo katika kutekeleza operesheni hiyo imeweka kizuizi barabarani katika eneo la Lukole lililoko wilayani Ngara ambacho  maofisa wa idara ya uhamiaji  wanakitumia kuwakagua abiria wanaokuwa ndani ya magari, akizungumza afisa wa idara hiyo  mkaguzi msaidizi Joackim Shija aliyekutwa kwenye kizuizi hicho amesema kimefanikisha zoezi la kuwakamata wahamiaji haramu, naye afisa wa idara ya uhamiaji wa wilaya ya Biharamulo Laulent Mutale amesema operesheni ya kuwasaka wahamiaji haramu itakuwa endelevu na wahamiaji haramu waliokamatwa watarudishwa walikotoka. 

Chanzo: ITV Tanzania

No comments:

Post a Comment

Post Bottom Ad