HABARI MPYA

Home Top AdPost Top Ad

Saturday, 14 October 2017

TAKUKURU Morogoro yawaburuza kortini watendaji wa vijiji kwa tuhuma za rushwa

Taasisi ya kuzuia na kupambana na kuzuia nchini TAKUKURU mkoa wa Morogoro imewafikisha  mahakamani maafisa watendaji watatu wa vijiji, mwenyekiti wa kamati ya vocha pamoja na wafanyakazi watatu wa wakala wa barabara nchini TANROADS kitengo cha mizani wakituhumiwa kujihusisha na vitendo vya kuomba na kupokea rushwa.

Kamanda wa kikosi cha TAKUKURU mkoa wa Morogoro Beutoz Mbwiga amewataja walioburuzwa mahakamani kuwa ni pamoja na afisa mtendaji wa kijiji cha Bonye wilayani Morogoro, Habibu Juma. Mwenyekiti wa kamati ya vocha katika kijiji hicho Costa Thadei pamoja na afisa mtendaji wa kijiji cha Mtombozi katika wilaya ya Morogoro Petronila Kivike wakituhumiwa kwa nyakati tofauti kuwapa wananchi mbegu ya mahindi bila malipo na kuwataka wasaini vocha kwa lengo la kujipatia fedha.

Shtaka jingine ni dhidi ya afisa mtendaji wa kijiji cha Ngong'olo wilaya ya Morogoro Thomas Chibago anayedaiwa kuomba na kupokea rushwa ya shilingi laki moja kutoka kwa mwananchi wa kijiji hicho ili asimchukulie hatua kwa kosa la kuchimba madini kinyume na sheria huku mashtaka mengine yakiwahusisha wafanyakazi watatu wa TANROADS Morogoro kitengo cha mizani, Elizabert Nyanda, Theodora Buchenja na Rosemary Mringo wanaotuhumiwa kuomba rushwa ya laki mbili toka kwa dereva wa basi ili wasimtoze dereva huyo faini baada ya gari yake kuharibika kwenye mizani.
Watuhumiwa wote wamefikishwa katika mahakama ya hakimu mkazi mkoa wa Morogoro  na kesi hizo zitatajwa oktoba 24 mwaka huu.

Chanzo: ITV Tanzania

No comments:

Post a Comment

Post Bottom Ad