HABARI MPYA

Home Top Ad

Post Top Ad

Monday, October 9, 2017

Rukwa wajipanga kuzalisha malighafi nyingi za viwanda kuvutia wawekezaji.

KATIKA kujiandaa na msimu wa kilimo Uongozi wa Mkoa wa Rukwa chini ya Mkuu wa Mkoa Kamishna Mstaafu Zelote Stephen wamezuru Taasisi ya Utafiti Kilimo (ARI) pamoja na Taasisi ya Utafiti wa Mifugo (TALIRI) nyanda za juu kusini - Uyole, Mkoani Mbeya ili kushuhudia shughuli zinazofanywa na taasisi hizo na kuchota utaalamu ili kunufaisha maendeleo ya mkoa. 

Ziara hiyo iliwayobeba Katibu Tawala wa Mkoa, Wakuu wa Wilaya na makatibu tawala wao walioambatana na viongozi wa vikundi vya wakulima,Wakurugenzi, maafisa kilimo na mifugo wa wilaya, pamoja na wenyeviti wa Halmashauri nne za Mkoa huo, na wataalamu wa kilimo na mifugo kutoka katika ofisi ya Mkuu wa Mkoa wa Rukwa.

Katika ziara hiyo ya siku moja mada mbalimbali zilitolewa kuhusu aina ya mazao yanayoweza kustawi katika Mkoa wa Rukwa, wadudu wanaoweza kushambulia mazao hayo na namna ya kuwadhibiti ili kuongeza uzalishaji pamoja na utafiti wa udongo.

Pia viongozi hao waliweza kujifunza umuhimu wa kilimo cha nyasi kwaajili ya mifugo, ufugaji bora kwaajili ya viwanda vya mazao ya mifugo, magonjwa mbalimbali ya mifugo na namna ya kukabiliana nayo

Mh. Zelote alisema kuwa kwa miongo kadhaa Mkoa wa Rukwa umekuwa katika mikoa inayoongoza kwa kilimo lakini haikuwahi kuwa namba moja hivyo ziara hiyo ndio mwanzo wa kuiendea Rukwa mpya yenye kuzalisha mazao yenye kuleta tija kwa wakulima, mkoa na taifa kwa ujumla.

 “Lengo la kufunga safari kutoka Rukwa hadi hapa ni kwa lengo la kuleta mabadiliko ya Kilimo na mifugo, Rukwa kupitia kilimo ndio litakuwa ni chimbuko la viwanda, kama wataalamu walivyosema kuwa kilimo ndio chimbuko la viwanda,tunahitaji kuboresha kilimo katika Mkoa wa Rukwa ili tuwe na viwanda vya uhakika” Amesema.

Amesema kuwa ili kuwakomboa wananchi wa hali ya chini ambalo ndio lengo la Rais Dk. John Pombe Magufuli Hakuna budi kuimarisha kilimo na hatimae kuinuka kutoka katika uchumi wa viwanda vidogo kwenda viwanda vya kati na kutoka katika uchumi mdogo kwenda uchumi wa kati.

Kwa upande wake mratibu wa ziara hiyo Benjamin Kiwozele alimshukuru Mh. Zelote kwa kuona umuhimu wa kuzitumia taasisi hizo kwa malengo yaliyowekwa na serikali.

Kabla ya Kumkaribisha Mh. Zelote, Mkurugenzi wa Taasisi ya utafiti wa Kilimo Tulole Bucheyeki alisema kuwa wataendelea kutoa ushirikiano kwa uongozi wa Mkoa wa Rukwa kwa heshima kubwa walioionyesha kwa kufika kwenye Taasisi hiyo na kuweza kukutana na wataalamu wao kwa nia ya kuboresha uwekezaji na vipato vya wananchi.

 Mkuu wa Mkoa wa Rukwa Kmaishna Mstaafu Zelote Stephen (aliyevaa miwani-kaundasuti) akiwa katika picha ya pamoja na watafiti mbalimbali katika Taaisi ya Utafiti wa Kilimo – uyole, Mbeya pamoja na baadhi ya wataalamu wa Kilimo na Mifugo kutoka Rukwa.
 Mkuu wa Mkoa wa Rukwa Kmaishna Mstaafu Zelote Stephen (aliyevaa miwani-kaundasuti) akipewa maelezo ya kilimo cha maharage na mtafiti hifadhi ya mimea Reinfred Maganga (shati nyeupe) katika moja ya bustani ya mifano yaliyopo kwenye viwanja vya taasisi hiyo.
 Mkuu wa Mkoa wa Rukwa Kmaishna Mstaafu Zelote Stephen (aliyevaa miwani-kaundasuti) pamoja na uongozi wa Mkoa wa Rukwa wakipewa maelezo ya kilimo cha maparachihci na mtafiti hifadhi ya mimea Reinfred Maganga (shati nyeupe- kushoto) katika moja ya vitalu vilivyopo kwenye viwanja vya taasisi hiyo.
Uyole4 - Mkuu wa Mkoa wa Rukwa Kmaishna Mstaafu Zelote Stephen (wa tatu kutoka kulia) akisikiliza uwasilishaji kutoka kwa mtafiti rasilimali za mifugo Dk. Pius Mwambene (wa kwanza kulia) kutoka Taasisi ya Utafiti wa Mifugo (TALIRI)

No comments:

Post a Comment

Post Bottom Ad