HABARI MPYA

Home Top Ad

Post Top Ad

Friday, October 13, 2017

MVIWATA MANYARA WALIA NA MBEGU FEKI KWA WAKULIMA

Tatizo la  mbegu feki nchini bado ni changamoto kubwa kwa wakulima, kwani wakulima wa mkoa wa Manyara wamekuwa wakinunua mbegu ambazo wakizipanda zinakaa ardhini kwa muda mrefu bila mazao kuota hali inayolalamikiwa na wakulima wengi.

Mratibu wa Mtandao wa Vikundi vya Wakulima Tanzania (MVIWATA) mkoani Manyara, Martin Pius aliyasema hayo kwenye mkutano mkuu wa 10 wa mkoa huo uliofanyika kwenye ukumbi wa White Rose mjini Babati.

Alisema pamoja na nia nzuri ya Serikali ya kutaka kukuza kipato cha mkulima kwa kuongeza bei ya chakula  anaiomba serikali upatikanaji wa bembejeo ya urahisi na gharama nafuu kwani kumekuwa na utolewaji wa pembejeo feki na kwa bei ya juu kutoka kwa wakala wanaopewa kazi hizo na serikali.

“Kutokana kubadilika kwa tabia ya nchi mbegu zilizobadilishwa vinasaba siyo njia ya kutatua changamoto hiyo, hivyo wataalamu wa kilimo wanapaswa kutafuta njia nyingine zitakazoleta tija kwa mkulima na siyo zitakazo ongeza changamoto,” alisema Pius.

Alisema mkutano wa mwaka huu umebeba kauli mbiu inayosema ‘uhakika wa mbegu kwa uhakika wa chakula' lakini kauli mbiu hiyo anaeleza bado ni changamoto kwani mbegu zinazosambazwa sio halisi.

Alisema baadhi ya wakulima wa mkoa huo  wamekuwa wakiuziwa mbegu feki za kilimo hali inayowarudisha nyuma katika shughuli za kilimo na pia kuwasababishia njaa.

Mgeni rasmi wa mkutano huo, mkuu wa mkoa wa Manyara,  Dk Joel Bendera aliwataka wakulima kutokata tamaa ya kulima zao la mbaazi kutokana na zao hilo kutokuwa na bei nzuri kwa mwaka huu .

Alisema anajua fika kuporomoka kwa bei ya zao hilo kumewaathiri wakulima wengi kwani ndilo zao kubwa la biashara ambapo mwaka jana walipambania bei ya zao hilo na kufikia kuuzwa sh 1,600 kwa kilo na mwaka huu zao hilo kufikia kuuzwa kwa sh 250 kwa kilo kutokana na wanunuzi wakubwa wa zao hilo ambao wapo India kudai kuwa wametosheka na mbaazi.

"Wakulima wanalima kulingana na soko, kwa bei hii ya mbaazi nani utamshawishi alime mbaazi mwakani, ndio maana tunasisitiza pamoja na kilimo tuwe na viwanda ili tuongeze thamani mazao yetu wenyewe," alisema Dk Bendera.

Alisema baada ya zao la pamba kushuka bei  wakulima walihamia kwenye mbaazi na mbaazi imeshuka bei wakulima watakosa la kufanya ila wasikate tamaa waendelee kulima, kwani kutatengenezwa kiwanda cha kubangulia mbaazi ili ifungashwe kwenye mifuko kisha ikauzwe nje ya nchi siyo lazima India pekee.

Aliwataka maafisa ugani wa halmashauri kuacha kukaa maofisini na badala yake kushirikiana na Mvitawa ili kuboresha teknolojia ya kilimo katika mkoa wa Manyara na kuwafundisha wakulima namna ya kulima kisasa, kuacha nafasi, kutumia mbolea na mbegu bora za kutumia.

"Hatuna maofisa ugani wa kutosha, angalau kila kata wawepo watatu, lakini hata hao waliopo kazi yao si kukaa maofisini watoke nje watu bado wanalima kienyeji  kazi zao zote wamewaachia Mviwata, kupitia halmashauri tutoe wataalamu wa kilimo kishirikiana na Mviwata," alisema Dk Bendera.

No comments:

Post a Comment

Post Bottom Ad