HABARI MPYA

Home Top AdPost Top Ad

Monday, 30 October 2017

KILELE CHA WIKI YA KUTAMBUA HUDUMA YA MCHUNGAJI YAFANA

Na. Sarah Reuben
Kanisa la Waadventista Wasabato Manzese limehitimisha Wiki ya Kutambua Huduma ya Mchungaji Elitabu Kajiru wa Kanisa la Waadventista Wasabato Manzese. 

Akizungumza wakati wa Ibada Kuu Mch. Aston Mmamba amelipongeza kanisa la waadventista wasabato Manzese kufanikisha tukio hilo muhimu linaloleta upendo na umoja kanisani. "Ninawapongeza sana washiriki wa mtaa wa Manzese kwa kuthamini kazi ya utume inayofanywa na mchungaji wenu Elitabu Kajiru", alisema.

Mch. Mmamba amewataka washiriki wa kanisa kuwasikiliza viongozi wao kwani wanajukumu kubwa la kuwalea kiroho. Alifafanua kuwa mchungaji mara nyingi hana muda maalum wa kutenda kazi kwa sababu muda wowote anapohitajika kutoa huduma kwa washiriki wake analazimika kufanya hivyo. Aidha, Mch. Mmamba aliwakumbusha kisa cha Musa alivyowaongoza wana wa Israeli kutoka utumwani Misri kwenda Kaanani ambapo kutokana na majaribu mengi, wanawaisraeli walisababisha Musa asifike Kanaan na kufia njiani.

Mch. Mmamba pia alimpongeza Mch. Elitabu Kajiru kwa kukubali kuacha kazi serikalini na kuamua kujiunga na kazi hii ya uchungaji anayoitumikia hadi sasa. Alifafanua kuwa, "Sio kitu rahisi kuacha ajira yenye mshahara mzuri na kuja kwenye uchungaji, inahitaji nguvu ya uweza wa roho mtakatifu kuweza kufanya maamuzi ya namna hii, alisisitiza Mch. Mmamba.

Naye Mch. Elitabu Kajiru na Mke wake waliwashukuru washiriki wa kanisa la Wasabato Manzese na Tandale kwa kutambua huduma yake na kuendelea kumtia moyo katika kazi hii ya utume.

Kilele cha Wiki ya Kutambua Huduma ya Mchungaji Elitabu Kajiru wa Kanisa la Waadventista Manzese kilihitimishwa na Mch. Aston Mmamba aliyeambatana na mkewe kwa hafla fupi ya waumini wote kushiriki chakula cha mchana pamoja na kuwepo kwa kwaya ya Angaza, Mbiu, Vijana, Dorcas na vikundi mbalimbali vya uimbaji. Wiki hii ilianza tarehe 21 Oktoba, 2017 na kuhitimishwa tarehe 28 Oktoba, 2017 hapa jijini Dar es Salaam.
 Mchungaji Elitabu Kajiru(wa kwanza kushoto) akiongozana na mkewe wakikaribishwa rasmi kanisani kwa program maalum ya kutambua huduma ya mchungaji wa Kanisa la Waadventista Wasabato Manzese.
 Mchungaji Aston Mmamba akitoa neno wakati wa ibada maalum ya kutambua huduma ya mchungaji wa kanisa la Waadventista Wasabato Manzese.

Kwaya ya Angaza ya Kanisa la Waadventista Wasabato Manzese ikimtukuza Mungu kwa Wimbo wakati wa hafla ya kutambua huduma ya Mchungaji Kajiru

No comments:

Post a Comment

Post Bottom Ad