HABARI MPYA

Home Top Ad

Post Top Ad

Wednesday, October 18, 2017

KIA YAFANYIWA UKARABATI MKUBWA

 Mafundi wakiendelea na ukarabati katika jengo la abiria la Kiwanja cha Ndege wa Kimataifa cha Kilimanjaro (KIA). Ukarabati huo unatarajiwa kukamilika Desemba 2017.
 Naibu Waziri wa Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano (Sekta ya Ujenzi), Mhe. Elius Kwandikwa (wa tatu kulia), akitoa maelekezo kwa wasimamizi wa mradi wa ukarabati wa Kiwanja cha Ndege cha Kimataifa cha Kilimanjaro (KIA), wakati alipofanya ukaguzi wa ukarabati huo.
 Meneja mradi wa ukarabati Kiwanja cha Ndege cha Kimataifa cha Kilimanjaro (KIA), Mhandisi Mathew Ndossi, akimuonesha Naibu Waziri wa Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano (Sekta ya Ujenzi), Mhe. Elius Kwandikwa (Mb), (Kushoto), upanuzi wa maegesho ya ndege yanayofanyika kiwanjani hapo.
Na Mwandishi Wetu.
KIWANJA cha ndege cha Kimataifa cha Kilimanjaro (KIA) kinafanyiwa ukarabati mkubwa unaohusisha miundombinu mbalimbali, ambapo unaotarajiwa kukamilika Desemba 2017.
Maeneo yanayofanyiwa ukarabati ni pamoja na jengo la kupumzikia abiria, upanuzi wa maegesho ya ndege  na mifumo ya maji  taka.

Akizungumza baada ya kukagua maendeleo ya ukarabati huo, Naibu Waziri wa Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano, Mhe. Elius Kwandikwa amesema ameridhika na hatua iliyofikia, ikiwa ni zaidi ya asilimia 90.
 
"Nimeridhishwa na ukarabati unaoendelea katika kiwanja hiki na nafikiri mmejionea wenyewe kazi inaendelea vizuri, hivyo naamini kutokana na hali hii kazi itakamilika hivi karibuni, amesema Naibu Waziri Kwandikwa.
 
Aidha, Mhe Naibu Waziri amefafanua kuwa ukarabati huo ambao pia umehusisha maboresho ya mfumo wa maji taka unalenga kuleta tija kwa mkoa huo na Taifa kwa ujumla kutokana na kuwepo ongezeko la abiria, huduma za kijamii na kibiashara.

Amesisitiza kuwa Serikali itaendelea kukarabati na kujenga viwanja vya ndege nchini ili kurahisisha huduma za usafiri wa anga kwa wananchi wake lengo likiwa ni kuchochea fursa za kiuchumi ambazo zitasaidia kulipeleka Taifa katika uchumi wa kati.

Naye Meneja Miradi wa KIA, Mhandisi Mathew Ndossi,  amesema kuwa maegesho yatakapokamilika yatakuwa na uwezo wa kuegesha jumla ya ndege kubwa 11 kwa wakati mmoja badala ya 6 zinazoegeshwa sasa.
Ameongeza kuwa abiria wanatarajiwa kuongezeka kutoka 800,000 kwa mwaka hadi kufikia 1.2 milioni mara baada ya kukamilika kwa ukarabati huo.

Hivi karibuni KIA imeandaa mbio za marathoni zitakazofanyika Novemba 19 kwa kushirikisha raia mbalimbali wa nadani na nje ya nchi, ili kuvutia zaidi watalii na watumiaji wa usafiri wa anga kwa ujumla.
 
Kia pamoja na Kiwanja cha ndege cha Kimataifa cha Julius Nyerere (JNIA) ni milango ya kuingia nchini kwa usafiri wa anga kwa watalii wanaotoka nchi mbalimbali duniani, kuja kutembelea mbuga za wanyama na  vivutio vinavyopatikana kwenye mikoa mbalimbali ya Tanzania Bara na Zanzibar.

Wakati huo huo, Naibu Waziri Kwandikwa amekagua barabara ya Sakina - Tengeru (km 14.1) na barabara ya mchepuko ya Arusha (Arusha Bypass km 42.4) ambapo amesema kuwa kukamilika kwa barabara ya Sakina - Tengeru  ni mkombozi mkubwa kwa wananchi wa mkoa wa Arusha na wageni wanaoingia katika mkoa huo kwani kumepelekea  kupungua kwa  ajali na msongamano wa magari  katika eneo hilo.

Ametoa wito kwa wananchi kuzitunza barabara  na kutunza mazingira yanayozunguka barabara hizo ili ziweze kudumu kwa muda mrefu kwa vizazi vya sasa na vijavyo.

Naye, Meneja wa Wakala wa Barabara (TANROADS), mkoa wa Arusha Mhandisi, Johny Kalupale,  amemhakikishia Naibu Waziri huyo kufanya kazi kwa ubora na kwa weledi ili kutimiza malengo ya Serikali ya kuwajengea wananchi miundombinu bora na ya kisasa.

Awamu ya pili ya mradi huo sehemu ya barabara ya mchepuo ya Arusha (Arusha Bypass), inayofadhiliwa na Benki ya Maendeleo ya Afrika (AfDB), inatarajiwa kukamilika mwakani na kugharimu kiasi cha shilingi bilioni 67.
Naibu Waziri Kwandikwa amemaliza ziara ya kikazi katika mkoa wa Kilimanjaro na Arusha ambapo amekagua miradi mbalimbali inayotekelezwa na Wizara yake.

No comments:

Post a Comment

Post Bottom Ad