HABARI MPYA

Home Top AdPost Top Ad

Monday, 2 October 2017

KATIBU MKUU DKT. MERU ASTAAFU RASMI UTUMISHI WA UMMA

Aliyekuwa Katibu Mkuu Wizara ya Viwanda, Biashara na Uwekezaji anayeshughulikia maendeleo ya viwanda Dkt. Adelhelm Meru.

Na Mwandishi Wetu, Dar
KATIBU Mkuu Wizara ya Viwanda, Biashara na Uwekezaji anayeshughulikia maendeleo ya viwanda Dkt. Adelhelm Meru, amestaafu rasmi utumishi wa umma baada ya kutimiza umri wa miaka 60.
Dkt. Meru ambaye ni mtaalamu aliyebobea katika masuala ya viwanda na uwekezaji, aliteuliwa kushika nafasi hiyo na Rais Dkt. John Magufuli, Disemba 2015 na amehudumu katika nafasi hiyo hadi alipostaafu Jumatano wiki iliyopita.

Akizungumza katika hafla ya kumuaga Dkt. Meru, Waziri wa Viwanda, Biashara na Uwekezaji, Bw. Charles Mwijage licha ya kumpongeza kwa kumaliza salama utumishi wa umma, alimsifu kwa umahiri wake wa kutekeleza sera ya maendeleo ya viwanda.

“Sote tunafahamu Serikali ya Awamu ya Tano inaamini katika viwanda, wewe ulikuwa mstari wa mbele katika kubuni mbinu na mikakati ya kuharakisha ujenzi wa viwanda nchini,” alisema Bw. Mwijage.
Alisema Dkt. Meru alitumia uzoefu wake wa kufanya kazi Mamlaka ya Ukanda Maalumu wa Uwekezaji (EPZA), kuvutia kampuni mbalimbali ya ndani na nje ya nchi kujenga viwanda vya uzalishaji wa bidhaa.

Kwa upande wake, Dkt. Meru aliishukuru wizara kwa ushirikiano aliopewa na kuwaomba wafanyakazi wenzake kumpa ushirikiano wa juu Rais Dkt. Magufuli katika dhamira ya kuijenga Tanzania mpya yenye uchumi wa viwanda.

“Tumuunge mkono Rais Magufuli hasa katika ukamilishaji wa miradi mikubwa ya maendeleo ambayo ina matokeo makubwa kwa uchumi wa taifa hususan mradi wa Eneo Maalum la Viwanda la Bagamoyo (SEZ) na miradi ya Mchuchuma na Liganga.

Alichukua nafasi hiyo pia kumshukuru Rais Magufuli kwa kumwamini katika nafasi hiyo muhimu na kuushirikiano mkubwa alioupata wakati akiwa Katibu Mkuu Wizara ya Viwanda.
“Kwa kipindi chote tulichikuwa pamoja kuna mengi tuliyakamilisha na pale tulipokosana naamini tulikosana kwa ajili ya kazi, hivyo naamini tumesameheana kwa sababu mimi si malaika na hakuna mkamilifu zaidi ya Mungu aliyetuumba,” alisema Dkt. Meru.

Kabla ya kuwa Katibu Mkuu Viwanda, Dkt. Meru aliwahi kufanya kazi katika viwanda vya NECO na Kilimanjaro Machine Tools vilivyokuwa chini ya Shirika la Maendeleo la Taifa (NDC); aliwahi kuwa Mkurugenzi Mkuu Mamlaka ya Elimu na Mafunzo ya Ufundi Stadi (VETA).

Vilevile alikuwa mwanzilishi na Mkurugenzi Mkuu wa kwanza Mamlaka ya Ukanda Maalumu wa Uwekezaji (EPZA) pia aliteuliwa na Rais wa Serikali ya Awamu ya Nne, Jakaya Kikwete kuwa Katibu Mkuu wa Wizara ya Maliasili na Utalii. Dkt. Meru amewahi pia kuwa Mshauri Viwanda katika Kampuni ya Car & General (Kenya) Ltd, iliyoko Nairobi nchini Kenya.

No comments:

Post a Comment

Post Bottom Ad