HABARI MPYA

Home Top AdPost Top Ad

Monday, 2 October 2017

Jengeni utamaduni wa kuwapenda na kuwaheshimu wagonjwa, -Makinda.

Baadhi ya vifaa tiba na dawa zilizotumika katika zoezi hilo vikikabidhiwa kwa mkuu wa mkoa wa Lindi Bwana Godfrey Zambi.
 Madaktari Bingwa wakiendelea kumpa huduma mmoja wa wangonjwa wa macho katika hospitali ya Sokoine Lindi.
 Daktari Bingwa wa watoto Martha Mkonyi akimuhudumia mmoja wa watoto waliokuja kupata huduma.

MWENYEKITI wa Bodi  ya Wakurugenzi wa Mfuko  wa Taifa wa Bima ya Afya (NHIF) Spika Mstaafu  Anne Makinda amewahimiza watoa huduma katika vituo vya matibabu kujenga utamaduni wa kuwapenda na kuwaheshimu wagonjwa ili kuwapa faraja na huduma bora wanapokwenda kupata matibabu katika vituo vyao.

Akizunguza wakati wa uzinduzi wa huduma za madaktari bingwa katika mikoa ya Mtwara na Lindi, Mama Makinda amesema wagonjwa wengi hususan wanawake wajawazito wanaogopa kwenda kupata huduma za mazitbabu katika vituo hivyo kutokana na mapokezi mabaya wanayopata hivyo wanaamua kwenda kwa wakunga wa jadi au kujifungulia majumbani ambako hakuna mazingira salama.

Amesisitiza kuwa wahudumu wa vituo vya matibabu wanawajibika kuwa na lugha nzuri na huruma kwa wagonjwa kwani kazi wanayofanya inaweza kuwa na mafanikio au madhara makubwa kwa afya za watu wanapwahudumia.


Naye Mkurugenzi Mkuu wa Mfuko wa Taifa wa Bima ya Afya Bwana Bernald Konga amesema Mfuko huo umepania kufikisha huduma bora kwa kila mtanzania hivyo hatua ya kupeleka madaktari bingwa katika mikoa yenye mahitaji makubwa ya huduma hiyo ni hatua mojawapo ya kusogeza huduma karibu na watanzania wengi.

Amesema kuanzia mwaka 2013 hadi sasa Mfuko umeshapeleka madaktari bingwa katika mikoa 17 ambapo mikoa minne imepata huduma hizo mara mbili. Mikoa hiyo ni pamoja na Kigoma, Rukwa, Lindi na Mtwara. 

Ameongeza kuwa katika kipindi cha miaka minne cha utekelezaji wa mpango huo katika mikoa ya pembezoni zaidi ya wananchi Elfu Kumi na Tisa wamehudumiwa na madaktari bingwa ambapo zaidi ya Mia saba wamefanyiwa upasuaji wa kibingwa.

Wananchi waliopata huduma hiyo wamepongeza huduma walizopatiwa na madaktari bingwa hao na kueleza kuwa uwepo wao katika mikoa ya Lindi na Mtwara kwa muda wa siku sita tangu 25 hadi 30 Septemba, 2017 umewasaidia kupunguza gharama za matibabu hayo kwani wangelazimika kusafiri hadi Dar es Salaam ili kupata huduma hizo.

Wananchi hao wamepongeza juhudi na huduma zilizotolewa na madaktari hao na  kuomba Mfuko uweke utaratibu wa kutoa huduma hizo mara kwa mara ili kuwapunguzia usumbufu wa kufuata huduma hizo mahali pengine.

Pamoja na kugharamia upelekaji wa madaktari bingwa hao, NHIF pia imepeleka vifaa tiba na dawa zilizotumika katika zoezi hilo zenye thamani ya zaidi ya Shilingi Milioni 10.

Madaktari bingwa 18 kutoka Hospitali ya Rufaa ya Taifa ya Muhimbili na MOI wa magonjwa ya wanawake, watoto, mfumo wa mkojo, moyo, magonjwa ya ndani, magojwa ya masikio, pua na koo, na mabingwa wa dawa za usingizi na magojwa mahututi, walishiriki katika zoezi hilo la kutoa huduma katika hospitali za mikoa ya Ligula mkoani Mtwara na Sokoine mkoani Lindi. 

Katika zoezi hilo la siku sita wagonjwa 800 walipata huduma na 42 walifanyiwa upasuaji katika hospitali ya Ligula mkoani Mtwara, wakati katika hospitali ya Sokoine wagonjwa 676 walipatiwa huduma na  62 walifanyiwa upasuaji.

No comments:

Post a Comment

Post Bottom Ad