HABARI MPYA

Home Top Ad

Post Top Ad

Tuesday, September 12, 2017

ZANZIBAR KUIMARISHA KANUNI ZA KUKATAZA MATUMIZI YA TUMBAKU KATIKA KULINDA AFYA ZA WANANCHI

 Mwakilishi wa Shirika la Afya Duniani (WHO) Zanzibar Dkt Ghirmay Andemichael akitoa maelezo ya Shirika hilo kwenye warsha ya siku tatu ya kuimarisha kanuni za kupambana na matumizi ya tumbaku inayofanyika Hoteli ya Golden Tulip Malindi Mjini Zanzibar.
 Mkurugenzi Mkuu wa Wizara ya Afya Dkt. Jamala Adam Taib akifungua warsha ya kuimarisha kanuni za mapambano ya matumizi ya bidhaa zinazotokana na tumbaku katika Hoteli ya Golden Tulip Malindi Mjini Zanzibar.
 Dkt. William Maina kutoka WHOAFRO akitoa maelezo ya Azimio la WHO na sheria za kimataifa dhidi ya mapambano ya matumizi ya bidhaa zinazotokana na tumbaku katika warsha ya kuimarisha kanuni za mapambano hayo katika Hoteli ya Golden Tulip Malindi.
 Baadhi ya washiriki wa warsha ya kumiarisha mikakati ya kanuni za kupiga vita matumizi ya tumbaku inayofanyika Hoteli ya GoldenTulip Malindi Mjini Zanzibar.
Picha ya pamoja ya mgeni rasmi na washiriki wa warsha ya kuimarisha mikakati ya kupiga vita matumizi ya tumbaku inayofanyika Hoteli ya Goden Tulip Malindi Mjini Zanzibar.
Picha na Makame Mshenga.

Na Ramadhani Ali - Maelezo
Wizara ya Afya Zanzibar inaendelea kuimarisha kanuni za kupunguza matumizi ya tumbaku baada ya kuundwa sheria ya Afya ya Jamii ya mwaka 2012 na kuridhia Azimio la Shirika la Afya ulimwenguni (WHO) kupiga vita bidhaa zinazotokana na tumbaku katika kunusuru afya za wananchi.
Mkurugenzi Mkuu wa Wizara ya Afya Dkt. Jamala Adam Taib amesema Wizara hiyo tayari imeweka kanuni ya kukataza kuvuta sigara kwenye mikusanyiko ya watu katika kuwanusuru waathirika wa moshi wa sigara bila ya kuwa wavutaji.
Dkt. Jamala ameeleza hayo alipokuwa akifungua warsha ya siku tatu ya kuimarisha kanuni za kupambana na matumizi ya tumbaku katika Hoteli ya Golden Tulip iliyopo Malindi iliyowashirikisha wadau kutoka taasisi mbali mbali za Serikali.
Mkurugenzi Mkuu alisema uvutaji wa sigara umeonekana kuwa chanzo kikubwa cha ongezeko la maradhi yasiyoambukiza ikiwemo saratani, sukari maradhi ya mapafu na maradhi ya ini.
Alisema pamoja na kwamba Zanzibar haizalishi tumbaku na haina viwanda vinavyohusika na bidhaa za tumbaku bado wananchi wamekuwa waathirika wa moshi wa sigara.
Alieleza kuwa tafiti zilizofanyika zinaonyesha kuwa asilimia kubwa ya watu wanaofariki kutokana na maradhi hayo yanatokana na kuvuta sigara ambapo asilimia 15 ya vifo hivyo vinawafika watu wanaovutishwa moshi na wavutaji wa sigara bila ya wao kushiriki kuvuta.
Katika kufanikisha lengo  hilo Dkt. Jamala alizishauri taasisi za Serikali, Jumuiya za kiraia na jamii kwa jumla kuunga mkono kanuni inayokataza sigara kuvutwa kwenye mikusanyiko ya watu  na nyengine zinazoundwa ili kulinda afya zao.
Mwakilishi wa WHO Zanzibar Dkt. Ghirmay Andemichael alisema Zaidi ya watu milioni saba wanapoteza maisha kila mwaka duniani kutokana na matumizi ya bidhaa zinazotokana na tumbaku ambapo asilimia 80 ya vifo vinatokea katika mataifa yanayoendelea.
Aliongeza kuwa katika Bara la Afrika kiasi ya watu 146,000 wenye umri kuanzia miaka 30 wanakufa kila mwaka kutokana na maradhi yanayotokana na matumizi ya tumbaku.
Amekumbusha kuwa iwapo hatua madhubuti hazitachukuliwa za kuandaa mikakati ya kupunguza matumizi ya bidhaa za tumbaku nusu ya watumiaji wa bidhaa hizo watafariki kwani tumbaku ni hatari kwa kila mtu na inatabia ya kuuwa kimya kimya.
Aliishauri Serikali, jamii na washirika wa maendeleo kufanya juhudi  za ziada kuhakikisha kanuni zinazokaataza  matumizi ya tumbaku Zanzibar zinaimarishwa na zinatekelezwa kikamilifu.
Aliahidi kuwa WHO itandelea kutoa kila msaada katika kuimarisha kanuni hizo ili kuiwezesha Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar kufikia lengo la maendeleo endelevu la kupunguza vifo vinavyotokana na maradhi yasiyoambukiza kwa asilimia 3.4 ifikapo mwaka 2030.
Akizungumzia Azimio la WHO na mikakati ya kimataifa katika mapambano ya matumizi ya tumbaku, Dkt. William Maina alisema nchi zinapaswa kuongeza kodi ya bidhaa za tumbaku kwa lengo la kuzipandisha bei ili baadhi ya watu washindwe kuzitumia.
Alizitaja njia nyengine  kuwa ni kupunguza matangazo ya bidhaa hizo katika vyombo vya habari, kuweka ilani ya madhara ya tumbaku katika paketi za sigara na nchi jirani kushirikiana pamoja katika mapambano ya matumizi ya tumbaku.

No comments:

Post a Comment

Post Bottom Ad