HABARI MPYA

Home Top Ad

Post Top Ad

Monday, September 11, 2017

WIZARA YA AFYA YAPOKEA BIL. 227.76 KUSAIDIA SEKTA YA AFYA NCHINI.

Katibu Mkuu wa Wizara ya Afya Dkt. Mpoki Ulisubisya

NA WAMJW-DAR ES SALAAM
WIZARA ya Afya, Maendeleo ya Jamii,Jinsia ,Wazee na Watoto imepokea shilingi Bilioni 227.76 kutoka kwenye mfuko wa pamoja (Health Basket Fund) kwa ajili ya kufadhili shughuli mbalimbali za sekta ya afya nchini.

Akizungumza na Waandishi wa habari leo jijini Dar es salaam wakati wa kupokea fedha hizo , Katibu Mkuu wa Wizara ya Afya Dkt. Mpoki Ulisubisya amesema kuwa fedha hizo zitaelekezwa katika uboreshaji wa huduma za afya nchini.
“Fedha hizi zitasaidia pia kutoa huduma za chanjo kwani ni afua muhimu kwa wananchi hususan katika kupunguza vifo vya mama wajawazito na watoto wenye umri chini ya miaka mitano nchini” alisema Dkt. Ulisubisya.
Aidha Dkt. Ulisubisya amesema kuwa kwa mara ya kwanza wameamua kupeleka fedha hizo moja kwa moja kwenye vituo vya kutolea huduma za afya ili kuepuka changamoto za vituo hivyo kukosa dawa muhimu mara kwa mara.
Mbali na hayo Dkt. Ulisubisya  alisema kuwa asilimia 90 ya fedha hizo zinaenda moja kwa moja kwenye vituo vinavyotolea huduma za afya vya ngazi ya Halmashauri na asilimia 10 inatumika kwa ajili ya shughuli mbalimbali za usimamizi wa kisera katika sekta ya afya nchini.
Aidha Dkt. Ulisubisya amesema kuwa fedha hizo pia zitasaidia katika kuimarisha  miundombinu katika vituo vya afya na zahanati ili viweze kutoa huduma za upasuaji wa dharura kwa ajili ya  akina mama wajawazito wanaokabiliwa na uzazi pingamizi.
Kwa upande wake Balozi wa Denmark nchini Tanzania Bw. Einar Jensen kwea niaba ya wadau wa mfuko huo amesema kuwa mbali na Fedha hizo kushughulikia maswala ya afya nchini hapa pia zitakuwa na shughuli mbalimbali za maendeleo .
“Mbali na kushughulikia masuala ya afya pia napendekeza fedha hizi zihusike katika kuhudumia wakimbizi wanaongia Tanzania hasa katika maeneo ya Kigoma na Kibondo” alisema Bw. Jensen.

No comments:

Post a Comment

Post Bottom Ad