HABARI MPYA

Home Top Ad

Post Top Ad

Sunday, September 3, 2017

Wanafunzi wa Tusiime wasaidia wasiojiweza

WANAFUNZI wa shule ya Msingi ya Tusiime ya Tabata jijini Dar es Salaam, wametoa msaada wa vyakula na vitu mbalimbali kwa watu wasiojiweza wanaolelewa katika kituo cha Mama Teresa cha Mburahati, Dar es Salaam.

 Msaada huo ambao umetokana na michango ya wanafunzi wa shule hiyo ni pamoja na unga, mchele, mafuta ya kupikia na vinywaji vya aina mbalimbali.

Akizungumza punde tu baada ya kukabidhi msaada huo, mmoja wa wanafunzi wa Tusiime, Agnes Heke  amesema walianza kuchangishana wenyewe kwa wenyewe muda mrefu lengo ikiwa ni kusaidia watu wanaolelewa kwenye kituo hicho.

Alisema dhamira ya kusaidia wenzao wa kituo hicho inatokana na mafundisho ya upendo wanayofundishwa wakiwa shuleni Tusiime.

“Tumekuwa tukifundishwa kuwajali wenye shida na kwa kweli tulianza kuchangishana muda na leo hii tumeona hiki tulichopata tuwape wenzetu, huu ni mwanzo maana kadri tutakavyokuwa tunapata tutarudi kuwasaidia,” alisema Agnes.

Akizungumza mara baada ya makabidhiano hayo, Mkuu wa Taaluma wa shule hiyo, Maxon Wilson amesema  msaada uliotolewa na wanafunzi hao ni sehemu tu na wameahidi kuendelea na moyo huo wa upendo kwa wenzao.

Alisema msaada uliotolewa na wanafunzi hao unadhihirisha kuwa mafunzo ya maadili na kuwapenda wenzao wanayoyafundisha yamewaingia vema na wanayazingatia kwa dhati.

Mmoja wa wazee wanaolelewa na kituo hicho, Elizabeth Daudi, aliishukuru shule ya Tusiime kwa namna ambavyo imewafundisha wanafunzi wake kuwa na upendo kiasi cha kuamua kuchanga kwa ajili yao

“Msaada huu ni ishara kwanza mafunzo ya upendo mnayoyapata shuleni yamefanyakazi, hatukutarajia kupata msaada kama huu tunawashukuru na Mungu awazidishie,” alisema kwa niaba ya wenzake.

Alishukuru msaada huo wa wanafunzi wa Tusiime kwani umekuja wakati muafaka kwani huwa wanaishiwa na vyakula mara kwa mara.

“hatuna maneno ya kutosha kuelezea furaha yetu , tunaomba watu wengine waige mfano wa Tusiime, waone watu  wanaolelewa hapa ni wajamii nzima,” alisema.
Wanafunzi wa Shule ya Msingi  Tusiime, ya Tabata Dar es Salaam, Agnes Heke na Ibrahim Shaban wakikabidhi vyakula mbalimbali kwa Bi. Elizabethi Daudi asiyeona ambaye ni mmoja wa watu wasiojiweza wanaolelewa kwenye kituo cha Mama Teresa Mburahati jijini Dar es Salaam.Msaada huo umetokana na michango ya wanafunzi wenyewe.

 Wanafunzi wa Shule ya Msingi ya  Tusiime ya Tabata wakiwa wamebeba vyakula mbalimbali na sabuni kwa ajili ya kutoa msaada kwenye kituo cha watu wasiojiweza wanaolelewa kwenye kituo cha Mama Teresa Mburahati jijini Dar es Salaam. Msaada huo umetokana na michango ya wanafunzi wenyewe.    

No comments:

Post a Comment

Post Bottom Ad