HABARI MPYA

Home Top Ad

Post Top Ad

Sunday, September 17, 2017

SHIRIKA LA EMPOWER SOCIETY TRANSFORMM LIVES LATOA ELIMU JUU YA MADHARA YA UKEKETAJI SINGIDA

Makamu Mwenyekiti wa Bodi ya ESTL, Bi Rose Mjema akiwasilisha mada kwa washiriki wa mafunzo ya kupinga vitendo vya ukeketaji huku akitoa tahadhari juu ya madhara yatokanayo na vitendo hivyo vya ukeketaji.(Picha zote Na Jumbe Ismailly).

Shirika lisilokuwa la kiserikali la Empower Society Transform Lives (ESTL) la Mkoani Singida limesema kwamba ukeketaji wa wanawake na watoto ni tatizo kubwa Afrika,Tanzania ikiwa ni miongoni mwa nchi 28 zinazotajwa kuendeleza mila hiyo mbaya.

Hayo yalisemwa na Mtendaji Mkuu wa Shirika hilo Mkoani Singida, Joshua Ntandu kwenye risala aliyosoma wakati wa uzinduzi wa mradi wa kutokomeza ukeketaji katika vijiji 14 vilivyopo katika kata za Itaja,Mgori,Ntonge na Ughandi,uliofadhiliwa na The Foundation For Civil Society na kufanyika kwenye ukumbi wa mikutano wa Halmashauri ya wilaya ya Singida.

Aidha Ntandu alifafanua kwamba inakadiriwa kuwa Tanzania ina zaidi ya wanawake milioni 7.9 waliogundulika kuwa wamekeketwa huku Mkoa wa Singida ukishika nafasi tano za juu za mikoa inayoongoza kwa ukeketaji hapa nchini.

Alisema tafiti zinaonyesha pia kwamba vitendo hivyo vinaendelea kuongezeka katika Mkoa wa Singida na sababu kubwa zinazotajwa ni pamoja na imani kwamba ukeketaji ni sehemu ya makuzi ya mtoto wa kike na kwamba humzuia mtoto wa kike asiingie katika mahusiano ya mapenzi kabla ya kuolewa.
Hata hivyo Ntandu alisisitiza kuwa jamii pia huamini kwamba ukeketaji ni tiba ya ugonjwa unaojulikana kama lawalawa kwa watoto wa kike (Vaginal or Urinary Tract Infection (UTI).

“Kadhalika kuna mbinu mpya ambayo imeshamiri ya ukeketaji wa watoto wachanga mara tu wanapozaliwa na kabla ya kufikia umri wa mwaka mmoja,na hii hufanywa ili kuepuka kuchukuliwa hatua za kisheria na vyombo vya dola”alisisitiza Mtendaji mkuu huyo wa ESTL.

Akizindua mradi huo kwa niaba ya Katibu Tawala wa Mkoa wa Singida,Afisa Ustawi wa jamii wa Mkoa wa Singida,Shukurani Mbago,pamoja na kusikitishwa na mbinu mpya iliyoshamiri ya ukeketaji wa watoto wachanga,alizitaja baadhi ya sababu za kuongezeka kwa vitendo hivyo kuwa ni imani kuwa ukeketaji ni sehemu ya makuzi ya mtoto wa kike na kwamba kumzuia mtoto wa kike asiingie katika mahusiano ya mapenzi kabla ya ndoa.

“Jamii pia huamini kuwa ukeketaji ni tiba ya ugonjwa ujulikanao kwa jina la lawalawa kwa watoto wa kike mara tu wanapozaliwa na kabla ya kufikia umri wa mwaka mmoja.”alifafanua Katibu tawala huyo wa Mkoa.

Kwa upande wake Makamu Mwenyekiti wa Bodi ya ESTL Mkoa wa Singida,Rose Mjema aliweka bayana kwamba mpaka sasa wameshaunda kamati za kutokomeza ukeketaji katika ngazi za vijiji na kata kutokana na watu waliopo katika ngazi hizo kuonyesha utayari wa kufanyakazi na wao.

Kwa mujibu wa Mjema wajumbe waliopo katika kamati hizo ni ni vijana tu kwa ngazi ya kata na vijiji,viongozi wa jadi,wakunga wa tiba asilia na wakunga wa jadi kwa kuwaandalia vikundi vya kupiga vita masuala ya ukeketaji kwenye maeneo yao.

Naye Mwenyekiti wa Halmashauri ya wilaya ya Singida,Elia Digha akizungumza na washiriki wa semina hiyo alishauri kwamba ili kukabiliana na vitendo hivyo kuanzia ngazi za serikali za vijiji pamoja na Halmashauri waanze kuandaa sheria ndogo itakayosimamia udhibiti wa ukeketaji katika Halmashauri ya wilaya hiyo.
Baadhi ya Mangariba na wakunga wa jadi kutoka katika Tarafa ya Mgori, wilayani Singida ambao wameamua kuachana na shughuli za kukeketa baada ya kupatiwa elimu na Shirika lisilokuwa la kiserikali la ESTL la Mkoani Singida,wakitoa ushuhuda kwenye uzinduzi wa mradi wa kutokomeza ukeketaji kwa wanawake katika Mkoa wa Singida uliofanyika kwenye ukumbi wa mikutano wa Halmashauri ya wilaya ya Singida.

No comments:

Post a Comment

Post Bottom Ad