HABARI MPYA

Home Top Ad

Post Top Ad

Monday, September 11, 2017

SERIKALI YAINGIZA TANI 55,000 ZA MBOLEA ILI KUDHIBITI MFUMUKO WA BEI


 Kaimu Mkurugenzi Mamlaka ya Udhibiti wa Ubora wa Mbolea Tanzania(TFRA) Bw. Lazaro Kitandu (katikati) akisisitiza jambo kwa waandishi wa habari wakati zoezi la upakuaji wa mbolea ya kupandia ukiendelea katika bandari ya Dar es Salaam mapema hii leo. 
 Wafanyakazi wa Mamlaka ya Bandari nchini wakiendelea na zoezi la upakiaji wa mbolea ya kupandia tani elfu 23 tayari kwenda kwa wakulima  mapema hii leo jijini Dar es Salaam.
Wafanyakazi wa Mamlaka ya Bandari nchini wakiendelea na zoezi la kufunga mbolea ya kupandia katika mifuko tayari kwa kupakiwa na kusafirishwa kwenda kwa wakulima.Picha na Eliphace Marwa - Maelezo

Na. Eliphace Marwa - Maelezo
Serikali imeingiza nchini jumla ya tani elfu 32 za mbolea ya kukuzia pamoja na tani elfu 23 za mbolea ya kupandia kupitia mfumo mpya wa uagizaji wa mbolea kwa pamoja, lengo likiwa ni kudhibiti bei kwa kuzingatia bei elekezi.
Akizungumza na waandishi wa habari Jijini Dar es Salaam wakati zoezi la upakuaji wa mbolea hiyo likiendelea Kaimu Mkurugenzi Mamlaka ya Udhibiti wa Ubora wa Mbolea Tanzania(TFRA) Bw. Lazaro Kitandu amesema kuwa mpaka sasa jumla ya tani elfu 55 za mbolea zimewasili nchini.
Hii ni awamu ya kwanza ya kuingiza mbolea nchini kupitia mfumo mpya ya uagizaji mbolea kwapamoja ambapo kampuni ya OCP S.A ya nchini Morocco imeingiza jumla ya tani elfu 23 za mbolea ya kupandia na Kampuni ya Premium Agro Chem imeingiza tani elfu 32 za mbolea ya kukuzia.
“Mpaka sasa zoezi la kupakua mbolea ya kupandia (DAP) tani elfu 23 linaendelea vizuri na mara baada ya kumaliza kupakua mbolea hii tutaanza zoezi la kupakua mbolea ya kukuzia (UREA) ambayo ni tani elfu 32,” alisema Bw. Kitandu.
Kitandu aliongeza kuwa Mheshimiwa Waziri wa kilimo juzi alipokuwa anaongea na waandishi wa habari mjini Dodoma na akasisitiza bei ambazo zimetolewa zisimamiwe na kila ngazi kwasababu taasisi peke yake haiwezi kuwa na watu kila mahali hivyo Tawala za mikoa, Serikali za mitaa mpaka Kijiji zitasaidia kusimamia bei ambazo zimetolewa. 
Pia Kitandu aliongeza kuwa kuhusiana suala la bei ya mbolea hiyo itatangazwa kupitia vyombo vya habari kama vile magazeti na televisheni na hivyo kutoa onyo kwa mawakala kujipangia bei kwa kuuza mbolea nje ya bei elekezi ya Serikali kwamba watachukuliwa hatua za kisheria kama kunyang’anywa leseni, kufungwa, faini au vyote kwa pamoja.
Aidha Kitandu alisisitiza kuwa mbolea hizi siyo mbolea za ruzuku kwani wakulima wengi wamekuwa wakichanganya mbolea hizi na mbolea za ruzuku na amefafanua kuwa mbolea hii imefanyiwa utaratibu wa kudhibiti toka kule inapotoka na hivyo serikali itahakikisha mbolea hii inauzwa kwa kulingana na bei ya soko la dunia.
Aidha Bw. Kitandu  aliwahakikishia wakulima kuwa  mbolea itasafirishwa mpaka vijijini kwa kutumia treni na malori kwa sehemu ambapo treni haiwezi kufika, na amewatoa hofu wakulima kuwa msimu unaoanza mwezi huu wameingiza tani 23,000 kwa mbolea ya kupandia (DAP) na tani 32,000 kwa mbolea ya kukuzia (UREA) ambapo watakuwa wanaagiza kwa awamu kwa miezi miwili miwili.

No comments:

Post a Comment

Post Bottom Ad