HABARI MPYA

Home Top AdPost Top Ad

Monday, 4 September 2017

POLISI MKOANI GEITA YAMNASA MTEKAJI WATOTO

Mtuhumiwa wa matukio ya utekaji, Samson Peter (18) mkazi wa Mtaa wa Kalifoinia, Kata ya Katoro wilaya ya Geita mkoa wa Geita muda mfupi baada ya kutiwa mbaroni na askari polisi.

POLISI mkoani Geita kwa kushirikiana na wenzao wa Mkoa wa Arusha wamemtia mbaroni mtuhumiwa wa utekaji watoto akiwa na mtoto mwenye umri wa miaka miwili katika nyumba ya kulala wageni ya Shitungulu, Katoro Wilaya na Mkoa Geita aliyekuwa akimshikilia akidai apewe Sh milioni nne.
Samson Peter amekamatwa usiku wa kuamkia jana baada ya timu maalumu ya Polisi ya askari tisa, watano kutoka Arusha wakiongozwa na Mkaguzi wa Polisi Amani na wa Geita askari wanne wakiongozwa na Mkaguzi wa Polisi, James, kuizingira nyumba ya wageni aliyokuwa amejificha mtuhumiwa na mtoto aliyemteka tangu Septemba Mosi.
Akithibitisha hilo, Kamanda wa Polisi Mkoa wa Geita, Mponjoli Mwabulambo alisema mtuhumiwa alikamatwa saa mbili usiku juzi katika nyumba ya kulala wageni iitwayo Shitungulu katika Mtaa wa California, Kata ya Katoro wilayani Geita akiwa chumba namba 11 na mtoto huyo Justine Ombeni (2) aliyemteka, akiwa hai na afya njema.
Kamanda Mwabulambo alisema mtoto huyo alitekwa Septemba Mosi saa nane mchana wakati akicheza na watoto wengine watatu mbele ya nyumba yao baada ya mtuhumiwa kufika na kuwagawia jojo watoto wengine watatu na kisha huyo wa nne kumchukua akiwaambia watoto wenzake akamnunulie juisi dukani.
Alieleza kuwa baada ya kuwalaghai watoto wengine, aliondoka na mtoto huyo na kutokomea kusikojulikana hadi wazazi walipotoa taarifa Kituo cha Polisi Geita na wakati baba anarudi nyumbani kutoka kuripoti Polisi zikiwa zimepita saa nne baada ya utekaji, alikuta ujumbe wa karatasi unaoonesha namba ya simu ya mtekaji ukielekeza awasiliane naye kwa simu hiyo.
Ujumbe huo alipatiwa kijana mwenye umri wa miaka 13 wa jirani ambaye bila kufahamu una lengo gani aliufikisha nyumbani kwa familia na ndipo ufuatiliaji ulipoanza wa mtoto kwa kuwasiliana kupitia simu hiyo ambayo katika mawasiliano, mtekaji alitoa masharti ya kutumiwa Sh milioni nne kupitia mtandao wa M-Pesa.
Wakati mtekaji huyo akitekeleza ukatili huo, tayari wakati huohuo alikuwa akisakwa mkoani Arusha kwa tuhuma pia za kuteka watoto wanne na kisha kujipatia Sh 300,000 kwa njia hiyo ya kupitia mtandao wa simu na kuwaachia watoto wawili kati ya wanne anaodaiwa kuwateka.
Hadi jana watoto wawili kati ya hao wanne hawajulikani waliko. Kwa mujibu wa taarifa za kipolisi, imedaiwa kuwa baada ya kutenda ukatili huo mkoani Arusha kati ya Juni na Agosti, mtuhumiwa alitoroka na kurudi mkoani Geita na kuendeleza ukatili huo hadi alipotiwa mbaroni na timu hiyo ya askari polisi waliokuwa wakitumia weledi na utaalamu wa ufuatiliaji mitandao ya simu.
Akisimulia huku akitokwa machozi, mama mzazi wa mtoto aliyetekwa, Elizabeth Ombeni alisema anaishukuru zaidi serikali na Jeshi la Polisi kwa kazi nzuri iliyoifanya kwa kurejesha amani na faraja katika familia hiyo iliyokuwa imetoweka kwa zaidi ya saa 36.
Kwa upande wake, baba mzazi wa mtoto, Ombeni Mshana alisema ushirikiano wa Polisi katika kutekeleza kazi hiyo uwe ni mfano wa maadili mema na kujituma kwa dhati katika ufuatiliaji na kupambana na uhalifu akiwashukuru polisi mikoa ya Geita na Arusha kwa kufanikisha uokozi huo.
Alisema baada ya kupewa vitisho kupitia ujumbe wa simu kutoka kwa mtuhumiwa ukimuonya kuwa akithubutu kuripoti au kushirikiana na polisi kumsaka atamkata mikono na miguu mtoto wake, ulimshtua sana na alikuwa ameamua kutuma kiasi cha fedha kilichoombwa na mtuhumiwa kwa simu.
Hata hivyo, alisema polisi walimzuia na kumtia moyo asitume fedha, na hadi mtuhumiwa anakamatwa alikuwa hajampatia fedha kiasi chochote. Alipotakiwa kuzungumzia tuhuma hizo, Samson Peter amekiri kuhusika na kuwa amekuwa akisukumwa na tamaa kupata fedha za matumizi kwa maisha ya anasa baada ya kukatisha masomo akiwa kidato cha tatu na alihitimu elimu ya msingi katika Shule ya Msingi Kilimani katika Kata ya Katoro.
Akizungumza na wanahabari baada ya kukamatwa, Peter amekiri kumteka mtoto Justine ili ajipatie fedha jaribio alilokiri kugonga mwamba na kuwa kati miezi miwili iliyopita, akiwa jijini Arusha pia aliteka watoto wanne akiwemo msichana mmoja na kupata Sh 300,000 kabla ya kurudi mkoani Geita.
Hata hivyo, baada ya wazazi wa watoto wengine wawili kushindwa kumpatia fedha kupitia mtandao, aliwatelekeza na kuondoka huku wengine wawili akiwarudisha maeneo aliokuwa amewateka ili warudi kwa wazazi wao kwa kuwaachia huru baada ya kumpatia fedha hizo kupitia mtandao wa simu.

Chanzo: Habari Leo

No comments:

Post a Comment

Post Bottom Ad