HABARI MPYA

Home Top AdPost Top Ad

Friday, 15 September 2017

MEYA CHAUREMBO: MANJI AMENYANG’ANYWA UDIWANI KWA MAKOSA YA MWAKA 2016

Meya wa Manispaa ya Temeke, Abdallah Chaurembo amesema aliyekuwa Diwani wa Mbagala Kuu (CCM), Yusuf Manji alivuliwa cheo hicho kwa kosa la kutohudhuria vikao sita vya mwaka 2016 bila kutoa taarifa.
Manji aliyekumbwa na mikosi ya kesi tangu mwaka huu uanze juzi aliachiliwa huru na Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu Dar es Salaam akiwa na wenzake watatu waliokuwa wakikabiliwa na kesi ya uhujumu uchumi kwa kukutwa wakiwa na mabunda 35 ya vitambaa vinavyotumika kutengeneza sare za Jeshi la Wananchi wa Tanzania(JWTZ) zenye thamani ya Sh 192.5 milioni.
Kesi hiyo imefutwa baada ya Mkurugenzi wa Mashtaka(DPP) kusema hana nia ya kuendelea nayo.
Mbali na kesi hiyo, Manji pia anakabiliwa na kesi ya matumizi ya dawa za kulevya aina ya heroin aliyosomewa Februari 17, katika Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu, Dar es Salaam.
Septemba 6, Meya Chaurembo aliwaambiwa waandishi wa habari jijini Dar es Salaam kuwa walimwondoa kwenye nafasi ya udiwani kwa kukosa sifa ikiwa pamoja na kutohudhuria mikutano sita ya Baraza na Kamati za Madiwani.
Hata hivyo, Manji alishaeleza kuhusiana na kutokubaliana na hatua ya kumvua udiwani na mara baada ya kuachiwa huru, aliulizia kuhusu malalamiko yake aliyowasilisha mahakamani hapo kuhusu udiwani wake yako vipiu lakini Hakimu Shaidi alimueleza kwa kuwa yuko huru ataenda kulishughulikia hilo.
Akizungumza jana kwa njia ya simu na gazeti hili, Chaurembo alisema makosa ya Manji yalitendeka mwaka 2016 kabla hata mikosi ya kukamatwa na kufunguliwa kesi haijaanza.
“Ungekuja ofisini kwa Mkurugenzi wa Manispaa uone ‘correspondence’ (barua) tulizokuwa tukiwasiliana na Manji ndiyo ujue kwamba tuliwasiliana naye kabla. Vikao ambavyo Manji hakuhudhuria ni vya mwaka 2016 kabla hata hajakamatwa kwa tuhuma za dawa za kulevya,” alisema Chaurembo.
Alisema mbali na kosa hilo, baadhi ya wananchi wa Kata ya Mbagala Kuu walishawasilisha malalamiko ya kukosa mwakilishi katika Baraza la Madiwani, huku chama chake cha CCM nacho kikiridhia avuliwe udiwani.
Hata alipoulizwa sababu za kumhukumu Manji kwa kosa alilofanya mwaka 2016, Chaurembo huku akimtaka mwandishi kwenda ofisi za Manispaa ya Temeke, alisema walikuwa wakiwasiliana na CCM kwanza.
“Wakati huo tulikuwa pia tunawasiliana na chama chake ambacho kilitupa ‘go ahead’ tuchukue sheria. Sheria ya Serikali za Mitaa ya mwaka 1982 inataja vikao vya madiwani vinane, vinne vya Baraza na vinne vya Kamati ya Madiwani. Diwani asipohudhuria vikao vitatu bila kutoa maelezo anavuliwa udiwani,” alisema Chaurembo.
“Manji hakuhudhuria vikao na hakutoa taarifa mpaka sisi tulipomtafuta na ndipo akajibu. Tukawasiliana na chama chake wakasema tuendelee na taratibu. Kuhusu kuadhibiwa kwa kosa la mwaka 2016, mtafute Mkurugenzi wa Manispaa atakwambia, mimi kwa sasa niko kijijini kwetu,” alisisitiza Chaurembo.
Mkurugenzi Mtendaji wa Manispaa ya Temeke, Nassib Mbaga alipotafutwa kwa njia ya simu alisema hawezi kuzungumzia suala hilo kwa sababu yuko safarini.
“Mimi niko safarini, nenda ofisini utapewa taarifa. Taratibu zote zilifuatwa lakini siwezi kukumbuka ni barua ya lini aliandikiwa au ya lini alijibu,” alisema Mbaga.
Manji aliyekuwa Mwenyekiti wa Klabu ya Yanga alikuwa pia akikabiliwa na kesi ya kuajiri wafanyakazi 25 wa kampuni yake ya Quality Group waliokuwa wakidaiwa kutokuwa na vibali vya kufanya kazi nchini.
Aprili 19 mwaka huu, wafanyakazi 16 kati ya hao ambao pia ni raia wa India, walihukumiwa kifungo cha miaka mitatu jela kila mmoja au kulipa faini ya Sh 22 milioni baada ya kupatikana na hatia kwa mashtaka matano yanayowakabili, ikiwemo kufanya kazi nchini kinyume cha sheria na kuzuia maofisa Uhamiaji kutimiza majukumu yao.

Chanzo: Mwananchi

No comments:

Post a Comment

Post Bottom Ad