HABARI MPYA

Home Top Ad

Post Top Ad

Friday, September 15, 2017

Makamba: Kila Mtanzania Anajukumu la Kuhifadhi Tabaka la Ozoni.

Waziri wa Nchi, Ofisi ya Makamu wa Rais Muungano na Mazingira January Makamba 

Na: Lilian Lundo, MAELEZO-Dodoma
Serikali imesema kila Mtanzania anajukumu la kuhifadhi Tabaka la Ozoni kwa kutotumia bidhaa zenye madhara kwa Tabaka hilo katika biashara na shughuli za kila siku za majumbani.

Hayo yameelezwa na Waziri wa Nchi, Ofisi ya Makamu wa Rais Muungano na Mazingira January Makamba kupitia taarifa aliyoitoa leo, kwa vyombo vya habari juu ya Siku ya Kimataifa ya Hifadhi ya Tabaka la Ozoni inayofanyika kila mwaka, Septemba 16.

"Kwa kuzingatia kauli mbiu ya mwaka huu ni muhimu tuzingatie kwamba juhudi za kila mmoja wetu zinatakiwa ili kupunguza na kuondosha madhara katika Tabaka la Ozoni yanayosababishwa na bidhaa tunazonunua na kutumia majumbani au sehemu za biashara ," amefafanua Makamba kupitia taarifa hiyo.

Makamba amesema kuwa kila mwananchi anatakiwa kuepuka kuingiza nchini gesi zilizopigwa marufuku na vifaa vinavyotumia gesi haribifu kama vile majokofu na viyoyozi vilivyokwisha tumika (mitumba) na ambavyo vinatumia vipoozi aina ya Chlorofluorocarbons (R11 na R12).

Vile vile amewataka Watanzania kununua bidhaa zilizowekwa nembo rasmi isemayo "Ozone friendly" ikiashiria haina wala haikutengenezwa na kemikali zinazomong'onyoa Tabata la Ozoni.

Aidha amewaasa Watanzania kuepuka kutupa hovyo majokofu ya zamani ama vifaa vya kuzima moto vyenye kemikali zinazomong'onyoa Tabaka la Ozoni aina ya " CFCs" na "halon". Ila wanapotaka kutupa wanatakiwa kupata ushauri wa kitaalamu kutoka kwa mafundi ama mamlaka zinazohusika.

Pia mafundi wa majokofu na viyoyozi wametakiwa kuhakikisha kuwa wananasa na kutumia tena vipoozi kutoka kwenye viyoyozi na majokofu wanayohudumia badala ya kuviacha huru visambae angani.

Mafundi hao wanatakiwa kutoa elimu kwa wateja wao kuhusu njia rahisi ya kutambua uvujaji wa vipoozi kutoka katika majokofu na viyoyozi wavyotumia.

Kitaifa, maadhimisho ya Siku ya Kimataifa ya Hifadhi ya Tabaka la Ozoni yatafanyika kwa njia ya uelimishaji Umma kuhusu Tabaka la Ozoni, faida zake, madhara ya kuharibika kwa Tabaka hilo na matumizi salama ya bidhaa zenye kemikali rafiki kwa Tabaka hilo.

Kauli mbiu ya mwaka huu katika kuadhimisha siku hiyo ni "Kutunza na Kulinda Viumbe Hai Duniani" ( Caring for All Life Under the Sun).

No comments:

Post a Comment

Post Bottom Ad