HABARI MPYA

Home Top Ad

Post Top Ad

Friday, September 15, 2017

Dkt. Harrison Mwakyembe: Tanzania iko Tayari kuwa Mwenyeji wa Tamasha la JAMAFEST 2019.

Na Benedict Liwenga-WHUSM, Kampala-Uganda.
Waziri wa Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo. Mhe. Dkt. Harrison Mwakyembe amesema kwamba, Tanzania iko tayari kuwa wenyeji wa Tamasha la Utamaduni na Sanaa Afrika Mashariki maarufu kama JAMAFEST kwa mwaka 2019.

Kauli hiyo ameitoa jana Mjini Kampala nchini Uganda wakati wa Ufungaji wa Tamasha hilo kwa mwaka 2017 ambapo wenyeji kwa mwaka huu walikuwa ni nchi ya Uganda.

Mhe. Mwakyembe amezipongeza nchi Wanachama wa Jumuiya ya Afrika Mashariki (EAC) ambazo zimehudhuria tamasha hilo kwa ushirikiano wa hali ya juu katika kubadilishana uzoefu na ujuzi juu ya masuala mbalimbali yanayohusu utamaduni na sanaa kwakuwa yameongeza mahusiano mapya ya karibu baina ya nchi hizo.

Waziri Mwakyembe aliezea kufurahishwa kwake kwa kujionea ngoma mbalimbali za kitamaduni toka kwa nchi wanachama ambazo zinaakisi uhalisia wa utamaduni wa nchi hizo, pia amefurahishwa na kwa kujionea bidhaa mbalimbali adimu toka kwa nchi hizo jambo ambalo amesisitiza kwamba nchi wanachama hazinabudi kuendelea kushirikiana katika kuzilinda tamaduni hizo na kuendelea kujifunza ujuzi mbalimbali wa kazi za sanaa.

“Nilipotembelea Maonyesho ya Tamasha hili pale katika viwanja vya Kololo nilifurahi sana kujionea ngoma za kitamaduni toka kwa vikundi mbalimbali vya nchi wanachama wa Jumuiya yetu ya Afrika Mashariki, hakika inapendeza sana, kwakweli tuzidi kuzilinda tamaduni zetu na kushirikiana kwa karibu zaidi”, alisema Mhe. Mwakyembe.

Akiongea kuhusu suala la Tanzania kukubali kuwa wenyeji wa Tamasha lijalo litakalofanyika mwaka 2019, Dkt. Mwakyembe alisema kwamba, Tanzania iko tayari kuwa wenyeji katika tamasha hilo lijalo na amezitaka nchi wanachama kujitahidi kushiriki pasipo kukosa wakiwa na bidhaa zao za kutosha huku akiwaahidi kuwa pindi wajapo Tanzania watafurahia mambo mengi na kujionea namna Watanzania wanavyo chapa kazi kutokana na kaulimbiu ya ‘HAPA KAZI TU’ iliyoasisiwa na Rais wa Awamu ya Tano wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Dkt. John Pombe Magufuli.

“Kwakuwa mwaka 2019 ni mzunguko wa Tamasha kama hili niwaambie kwamba, Tanzania iko tayari kuwa mwenyeji wa Tamasha hili na nawakaribisheni kwa dhati kabisa mje kujionea nchi yetu na namna tunavyofanya kazi kwa bidii, lakini pia mje na bidhaa nyingi zaidi kwa ajili ya kuwaonyesha Watanzania”, alisema Dkt. Mwakyembe.

Tamasha la JAMAFEST lilianzishwa mwaka 2013 nchini Rwanda na baadhi ya Viongozi wa Jumuiya ya Afrika Mashariki ambapo kwa mwaka huu tamasha hilo linafanyika mjini Kampala nchini Uganda ambapo kwa mwaka 2019 linatarajiwa kufanyika nchini Tanzania.
 Waziri wa Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo, Mhe. Dkt. Harrison Mwakyembe (Aliyevaa skafu) akiongea na Viongozi, Washiriki pamoja na wageni toka nchi mbalimbali (hawapo pichani) wakati wa Ufungaji wa Tamasha la Utamaduni na Sanaa Afrika Mashariki (JAMAFEST) kwa mwaka 2017 katika Ukumbi wa Taifa wa Maonyesho wa nchini Uganda, 14 Septemba, 2017.
Katibu Mtendaji wa Bodi ya Filamu Tanzania, Bibi Joyce Fissoo (aliyeshika bendera ya Tanzania) akiwaonyesha Washiriki pamoja na wageni toka nchi mbalimbali (hawapo pichani) Cheti cha Ushiriki wa Tamasha la Utamaduni na Sanaa Afrika Mashariki (JAMAFEST) kwa mwaka 2017 katika Ukumbi wa Taifa wa Maonyesho wa nchini Uganda, 14 Septemba, 2017.
 Naibu Waziri Mkuu ambaye  ni Waziri wa Wizara ya Mambo ya Afrika Mashariki ya Uganda Mhe. Ali Kirunda Kivejinja akabidhi Bendera ya Jumuiya ya Afrika Mashariki kwa Waziri wa Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo wa Tanzania Mhe. Dkt. Harisson Mwakyembe ikiashiria kuwa Jamuhuri ya Muungano wa Tanzania ni zamu yake kukabidhiwa dhamana ya kuandaa Tamasha la Nne (4) la Utamaduni na Sanaa la Jumuiya ya Afrika Mashariki (JAMAFEST) litakalofanyika mwaka 2019 jana usiku hafla hyo ilifanyika katika Jumba la Sanaa la Taifa jijini Kampala Nchini Uganda
 Waziri wa Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo, Mhe. Dkt. Harrison Mwakyembe akiwa ameibeba Bendera ya Jumuiya ya Afrika Mashariki (EAC) baada ya kukabidhiwa toka kwa Makamu wa Pili wa Waziri Mkuu wa Uganda na Waziri wa Afrika Mashariki, Kirunda Kivejinja kuashiria kwamba zamu ijayo kwa tamasha hilo ni Tanzania ambapo tukio hilo lilitokea wakati wa Ufungaji wa Tamasha la Utamaduni na Sanaa Afrika Mashariki (JAMAFEST) kwa mwaka 2017 katika Ukumbi wa Taifa wa Maonyesho wa nchini Uganda, 14 Septemba, 2017.
 Waziri wa Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo, Mhe. Dkt. Harrison Mwakyembe akiwa ameishika Bendera ya Jumuiya ya Afrika Mashariki (EAC) huku akiwaonyesha Viongozi, Washiriki pamoja na wageni toka nchi mbalimbali (hawapo pichani) wakati wa Ufungaji wa Tamasha la Utamaduni na Sanaa Afrika Mashariki (JAMAFEST) kwa mwaka 2017 katika Ukumbi wa Taifa wa Maonyesho wa nchini Uganda, 14 Septemba, 2017.
Wanamitindo toka Tanzania wakiwa Jukwaani wakionyesha mitindo yao mbalimbali ya mavazi iliyobuniwa na Watanzania mbele ya mgeni rasmi pamoja na Washiriki na wageni toka nchi mbalimbali (hawapo pichani) wakati wa Ufungaji wa Tamasha la Utamaduni na Sanaa Afrika Mashariki (JAMAFEST) kwa mwaka 2017 katika Ukumbi wa Taifa wa Maonyesho wa nchini Uganda, 14 Septemba, 2017.

(PICHA ZOTE NA BENEDICT LIWENGA-WHUSM)

No comments:

Post a Comment

Post Bottom Ad