HABARI MPYA

Home Top AdPost Top Ad

Monday, 4 September 2017

MAKALA MICHEZO: GADIEL MICHAEL ANAWEZA KUWA MSAADA WA NAFASI YA WINGA YANGA


Na. Honorius Mpangala.

Southampton ni moja ya klabu ambayo inaaminika kuwa na shule nzuri ya soka. Kuaminika huko kunatokana na matunda yaliyotokana na shule hiyo katika kukuza soka la vijana.

Katika klabu Southampton ndiko walikopita vijana kama Theo Walcott,Alex Oxlade-Chamberlain,Gareth Bale,Adam Lallana,Luke Shaw,Calum Chambers. Imani hiyo ya uwepo wa shule bora inatokana na uwezo wa vijana wanaoibuaka katika klabu Hiyo na kuhitajika sana wakati sa soko la usajili kwa wachezaji.

Licha ya kuwa na mmiliki mwanamke Katharina Liebherr,klabu hiyo imeweza kuimarika katika ufanyaji wa biashara na 
Kuhimili katika ligi kwa maana ya kutumia rasilimali zao ndani ya klabu.

Uwezo wa kasi aliyokuwa nayo Bale,Walcott na Chamberlain umetoka katika shule ya Southampton. Baada ya kufanya vyema katika klabu hiyo Ilikuwa ni Tottenham Hotspur waliamua kumsajili Bale. Wakati bale anasajiliwa ilikuwa tayari Arsenal walishamsajili Walcott. 

Bale alipofika katika klabu ya Tottenham alisajiliwa kama mlinzi wa kushoto.Alifanya vyema sana katika nafasi hiyo akiwa chini ya kocha Harry Rednap. Unaweza kusema Majeruhi ya nyota hufanikisha kumtoa kinda au kutoa nafasi kwa mchezaji mwenza katika nafasi moja.

Baada ya Bale kupata majeraha na kumweka nje kwa ya kikosi cha Tottenham,nafasi yake ilichukuliwa na Benoit Assou-Ekotto. Mkameruni huyo aliitendea vyema nafasi ile ya mlinzi wa kushoto kiasi kwamba ilitia shaka endapo Bale angelejea.

Hivyo ndivyo ilivyokuwa kurejea kwa Bale kulimfanya Rednap amtumie kama Kiungo wa pembeni kushoto. Bale alifanya vyema katika nafasi hiyo huku ile ya mlinzi ikikabidhiwa moja kwa moja kwa Ekotto.
Bale wa leo ni matokeo ya kiwango bora cha Ekotto kilichomfanya Kocha ambadilishe nafasi. Maamuzi ya Rednap ndiyo yaliyofanya Bale aje kununuliwa kwa kiasi cha pesa cha paundi milioni 85 kwenda Real Madrid.

Katika klabu ya Yanga kuna Gadiel Michael ambaye kwasasa amekuwa mlinzi bora kwa klabu na timu ya taifa.Kwa kipindi hiki ambacho Yanga wamepungua makali katika maeneo yao ya winga kulia na kushoto ingekuwa kamari nzuri endapo Mwalimu George Lwandamina angejaribu kumchezesha Gadiel kama winga na Nafasi ya ulinzi ikarejea kwa Mwinyi Haji Mngwali.

Haitakuwa Mara ya kwanza hili kutokea kwani wakati klabu ina Shadrack Nsajigwa na Fred Mbuna,ilimfanya Mwalimu kwa baadhi ya mechi kuwatumia wote wawili. Fred alicheza kama winga wa kulia vyema na kuacha eneo la ulinzi likibaki wa Nsajigwa.

Pia iliwahi fanyika kwa Amir Maftah na Nurdin Bakari wakigawana nafasi ya ulinzi na winga ya kushoto na wakacheza vyema.Wakati wa kocha Mbelgiji Thom Saintfit aliwahi watumia David Luhende na Staphano Mwasyika katika nafasi hiyo ya mlinzi na winga ya kushoto kwa baadhi ya Michezo.

Mtindo huo sio mgeni kwa wachezaji wetu wa kitanzania kwani wako wenye uwezo wa kucheza nafasi nyingi uwanjani na kukupa matokeo mazuri.

Kwa namna ninavyo mtazama Gadiel na mtindo wake wa kucheza namwona Bale tena katika miguu yake. Ana uwezo wa kukaa na mpira akiulinda vyema mambo ambayo hufanyika kwa wachezaji wa eneo la mbele. Kasi yake akikokota mpira na kushambulia ni kubwa na yenye matokeo ya kuleta hatari kwa wapinzani.

Faida ya kumtumia kama Winga itamfanya awe msaada kwa upande wake kukaba kuanzia eneo la wapinzani na kumpunguzia kazi kubwa mlinzi wake wa kushoto.

Maamuzi hayo kwa Lwandamina yatatoa changamoto ya nafasi kwa Emmanuel Martin na Geoffrey Mwashiuya na kuleta upinzani mkubwa baina yao.

Ni kamari lakini ninayoona itaweza kuleta matunda kwao na kupanua wigo wa kimatimizi kwa Gaiel.

©Honorius Mpangala 
0628994409

No comments:

Post a Comment

Post Bottom Ad